Tuesday, March 15, 2022

BALOZI MULAMULA ATAJA MAFANIKIO WIZARA YA MAMBO YA NJE

Na Waandishi Wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametaja maeneo 11 ambayo Wizara inajivunia katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita madarakani chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. 

Akiongea na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Balozi Mulamula amesema Wizara ya Mambo ya Nje katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita Wizara imetekeleza majukumu yake kwa mafanikio.

Balozi Mulamula ameyataja mafanikio hayo kuwa ni kusainiwa kwa makubaliano na mikataba ya ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa kufuatia ziara mbalimbali zilizofanywa na viongozi wa Kitaifa nje ya nchi na Wakuu wa nchi na Mashirika ya Kimataifa kutembelea nchini. 

“Ziara hizo pia zimewezesha upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu ambapo fedha kiasi cha Shilingi Trilioni 1.77 na Euro milioni 425 kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya zilipatikana, wakati huohuo Tanzania ilichaguliwa na nchi 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwa Makamu wa Rais wa Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo katika uchaguzi huo, Tanzania ilipita bila kupingwa, mara ya mwisho Tanzania kupata nafasi hiyo ilikuwa mwaka 1991,” amesema Balozi Mulamula.

Mafanikio mengine ni kufunguliwa kwa Balozi mpya mbili katika nchi za Austria na Indonesia na Konseli Kuu tatu katika miji ya Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Shanghai na Guangzhou nchini China, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa majengo katika balozi za Tanzania.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa wawekezaji kutoka nje ambapo wengi wameonesha dhamira ya kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali. 

Balozi Mulamula amesema Lugha ya Kiswahili kwa mara ya kwanza kiswahili kimetambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kuwekewa siku maalum ya kuadhimishwa duniani ambayo ni tarehe 7 Julai kila mwaka. Niwakumbushe kuwa, Kiswahili ni lugha ya kwanza ya kiafrika kupewa hadhi hiyo na UNESCO," Amesisitiza Balozi Mulamula.

Mafaniko mengine yaliyoainishwa na Mhe. Waziri wakati wa mkutano huo ni pamoja na kuondolewa kwa vikwazo 56 kati ya 64 vya kibiashara kufuatia maagizo ya Marais wa Kenya na Tanzania. Aidha, vikwazo vingine vinane viliondolewa na Mawaziri wa Biashara wa nchi hizi mbili walipokutana Zanzibar tarehe 13 Machi 2022.

Kadhalika, Waziri Mulamula amesema Wizara yake itaendelea kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje hususan kwenye masuala ya kukuza uchumi wa nchi kwa kuhamasisha uwekezaji kutoka nje, biashara na utalii. 

Balozi Mulamula amehitimisha na Suala la Watanzania waliokuwa wamekwama nchini Ukraine ambapo amesema serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha raia wake wanakuwa salama pamoja na changamoto hizo. 

“Napenda kuwafahamisha kuwa, zoezi la kuwaondoa Watanzania wote waliokuwepo nchini humo wakiwemo Wanafunzi limekamilika ambapo hadi sasa takribani Watanzania 300 wamefanikiwa kuondoka na kuelekea nchi jirani na baadhi yao wamerejea hapa nchini”, amesema Balozi Mulamula.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akisikiliza moja kati ya maswali yaliyoulizwa na baadhi ya waandishi wa habari (hawapo pichani) alipowasilisha taarifa ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na waandishi wa habari  alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita  




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.