Tuesday, March 1, 2022

TANZANIA , UNHCR WAKUTANA DAR ES SALAAM

 

1.     Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Hamad Masauni (kushoto), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (wa pili kushoto) wakiwa na Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Uhifadhi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bibi Gillian Doreen Triggs na Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Ushirikiano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Bw. Raouf Mazou wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na UNHCR unaofanyika jijini Dar es Salaam Machi 1-2 2022.

1.   Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (katikati) akifuatilia nyaraka za mkutano wa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na UNHCR unaofanyika jijiini Dar es Salaam, kushoto kwake ni Kamishna Msaidizi Uhifadhi wa UNHCR Bibi Gillian Triggs na Kamishna Msaidizi Uendeshaji wa UNHCR Bw. Raouf Mazou


1.  Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (kulia) akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Bw. Christopher Kadio wakati wa Mkutano wa pamoja kati  ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) unaofanyika jijini Dar es Salaam


1.   Washiriki wa mkutano wa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) wakifuatilia mkutano huo unaofanyika jijiini Dar es Salaam


1.   Washiriki wa mkutano wa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) katika picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania na UNHCR baada ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijiini Dar es Salaam


1.   Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (kulia) akizungumza jambo na Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Hamad Masauni baada ya kufungua Mkutano wa pamoja kati  ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) unaofanyika jijini Dar es Salaam



Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) wanakutana jijini Dar es Salaam kujadili utekelezaji wa majukumu ya kuwahudumia wakimbizi nchini na kuimarish ushirikiano kati ya pande mbili.

Mkutano huo wa majadiliano unafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 01 hadi  02 Machi 2022 unatokana na  mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Kamishina Mkuu wa UNHCR, Bw. Filippo Grandi yaliyofanyika New York, Marekani mwezi Septemba 2021.

Mkutano huo umefunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Hamad Masauni (Mb) na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania na UNHCR akiwemo Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani  Bw. Christopher Kadio.

Akifungua mkutano huo Mhe. Waziri Masauni aliihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu haki za wakimbizi kwa kuzingatia sheria za kimataifa na bila kusahau sheria za nchi.

Waziri Masauni amesisitiza umuhimu wa wadau kutoa misaada kwa ajili ya kuboresha huduma na miundombinu ya kuwahudumia wakimbizi pamoja na jamii inayozuunguka makambi ambayo kwa kawaida huwa inaathirika kutokana na ongezeko la watu.

Mhe. Masauni amesema  zoezi la kuwarejesha wakimbizi ni la hiyari na linafanyika kufuatia hali ya usalama nchini Burundi kuimarika.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ambaye anaongoza majadiliano hayo amesema  historia ya Tanzania ya kupokea na kuhifadhi wakimbizi sio ya kutiliwa shaka.

Amesema jukumu hilo limekuwa ni moja ya sera ya nchi na kusisitiza umuhimu wa UNHCR na Serikali kuimarisha ushirikiano ili kuendelea kutimiza jukumu hilo la kibinadamu kwa mafanikio makubwa, kwa sababu suala la wakimbizi halitarajiwi kumalizika katika kipindi kifupi kijacho.
 

Nao viongozi wa UNHCR wanaoshiriki Mkutano huo wakiongozwa na Kamishina Msaidizi wa Hifadhi, Bibi. Gillian Triggs na Kamishina Msaidizi wa Uendeshaji Bw. Raouf Mazou, Mratibu Mkazi wa UNHCR nchini, Bw. Ziatan  Milisic wameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kupokea na kuwahifadhi wakimbizi.

Walisema Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi tokea miaka mingi iliyopita na hadi sasa kuna wakimbizi 147,000 nchini ambao wamekuwa wakipatiwa huduma stahiki na hadi wengine, 162,000 kutoka Burundi kupatiwa uraia.  

Viongozi hao walielezea miradi mbalimbali inayotekelezwa na inayotarajiwa kutekelezwa na wadau kwa ajili ya kuboresha maisha ya waimbizi na jamii inayowazunguka. Miradi hiyo imejikita katika utoaji wa elimu bora, utunzaji wa mazingira, kuwajengea uwezo vijana na wanawake pamoja na kuboresha huduma mbalimbali kwa jamii zinazoishi karibu na makambi.

Walisema katika miaka ya karibuni UNHCR imetumia Dola za Marekani milioni 1.3 kwa ajili ya kuimarisha huduma mbalimbali ikiwemo usalama mkoani Kigoma. 

Mkutano huo wa majadiliano ya ngazi ya juu unajadili ajenda za hifadhi ya ukimbizi,  na jitihada za serikali za kuhudumia wakimbizi,  kinga , haki na mahusiano ya kiutendaji kati ya Serikali na UNHCR.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.