Monday, March 28, 2022

TANZANIA YASHIRIKI MAKABIDHIANO YA MAJUKUMU YA BARAZA LA AMANI NA USALAMA LA UMOJA WA AFRIKA

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Innocent Shiyo ameongoza ujumbe wa Tanzania katika hafla ya kupokea majukumu ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika yaliyokabidhiwa kwa Nchi 15 wanachama wapya, Tanzania ikiwemo na wajumbe wa Baraza hilo wanaomaliza muda wao.

Hafla hiyo ambayo imefanyika hivi karibuni jijini Maseru, Lesotho na kuratibiwa na Sekretarieti ya Umoja wa Afrika, ilitanguliwa na warsha iliyolenga kuwawezesha Wajumbe wa Baraza kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu majukumu ya Baraza hilo.

Wakati wa warsha hiyo ambayo ilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa wa Ufalme wa Lesotho, Mhe. Mats’epo Ramakoae, Wawakilishi wa Kudumu wa Nchi Wanachama 15 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika walibadilishana uzoefu kuhusu mamlaka na taratibu za Baraza hilo, vihatarishi kwa amani na usalama barani Afrika na namna ya kuimarisha ufanisi wa Operesheni za Kulinda Amani za Umoja wa Afrika. Aidha, maeneo ambayo yanakusudiwa kupewa kipaumbele na Baraza jipya pia yalijadiliwa.

Akizungumza baada ya warsha hiyo, Mhe. Balozi Shiyo alieleza kuwa, Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika na watu wa Afrika kwa ujumla wana matarajio makubwa kwa chombo hicho katika kuchangia na kuimarisha hali ya amani na usalama barani Afrika, Bara ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi. “Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa mchango wake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutumia Baraza la Amani na Usalama kutatua changamoto za kiusalama na kuimarisha amani na utulivu barani Afrika” alisema Balozi Shiyo.

Itakumbukwa kuwa,Tanzania ilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Februari 2022. Tanzania itahudumu kwenye Baraza la Amani na Usalama kwa kipindi cha miaka 2 kuanzia tarehe 01 Aprili 2022. Nchi 15 Wanachama wapya wa Baraza jipya la Amani na Usalama ni Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Gambia, Ghana, Morocco, Namibia, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini, Tanzania, Tunisia, Uganda na Zimbabwe.

Kwa mujibu wa Mkataba ulioanzisha Umoja wa Afrika, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ni chombo cha kudumu na cha maamuzi kuhusu masuala yote yanayohusu kuzuia, kukabiliana na kusuluhisha migogoro barani Afrika.

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Innocent Shiyo akikabidhiwa Bendera ya Taifa kutoka kwa Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania, Ethiopia, Bi. Elizabeth Rwitunga kama ishara ya kupokea rasmi majukumu ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi 15 zinazounda Baraza hilo. Hafla hiyo imefanyika hivi karibuni jijini Maseru, Lesotho. Tanzania ilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Februari 2022. Tanzania itahudumu kwenye Baraza  hilo kwa kipindi cha miaka 2 kuanzia tarehe 01 Aprili 2022.

Mhe. Balozi Shiyo (wa nne kushoto) akiwa na wajumbe wengine wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika mara baada ya wajumbe hao wapya 15 kukabidhiwa majumu ambayo yataanza kutekelezwa rasmi tarehe 01 Aprili 2022.

Picha ya pamoja

Wajumbe wengine wakiwa na Bendera za Nchi zao mara baada ya kukabidhiwa majukumu ya Baraza la Amani na Uslama la Umoja wa Afrika.

TANZANIA, LIECHTENSTEIN KUWEKEZA KATIKA KILIMO HAI

Na Mwandishi wetu, Dar

Tanzania na Liechtenstein zimekubaliana kuweka mpango mkakati wa kuwekeza katika kilimo hai na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo katika mikoa ya Morogogo na Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler ambaye yuko nchi kwa ziara ya kikazi.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubalia kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za Utalii, Viwanda, na Elimu, hususan kumuendeleza mtoto wa kike katika masomo ya sayansi na teknolojia.

“Tumekubaliana mara baada ya ziara yake tuweze kuangazia namna gani tunaweza kudumisha na kuendeleza maeneo mapya ya ushirikiano baina yetu kwa maslahi ya Tanzania na Liechtenstein,” Amesema balozi Mulamula.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler amesema Liechtenstein ina uhusiano imara na wa siku nyingi, na tumekuwa tukisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo hapa nchini Tanzania hivyo kuja kwetu hap ani kuja kuiona miradi hiyo na kutuwezesha kujadiliana kwa pamoja ni namna gani tunaweza kuendele kushirikiana katika miradi hiyo.  

"Katika kikao changu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania tumejadili mambo mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi zetu, lakini kubwa kabisa tumekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano," Amesema Waziri Hasler.

Waziri Hasler akiwa nchini atatembelea miradi mbalimbali ya kilimo hai inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Liechtenstein kupitia Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) katika mkoa wa Morogoro na Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mjumbe aliyeambatana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler akifafanua jambo wakati wa kikao 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Liechtenstein Mhe. Dominique Hasler na Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (kulia mwa Balozi Mulamula). Wengine ni Viongozi walioambatana na ujumbe wa Waziri Hasler pamoja na Afisa Mwandamizi kutoka wizarani 





Friday, March 25, 2022

NGORONGORO YAIKUTANASHA SERIKALI NA MABALOZI, WAKUU WA MASHIRIKA YA KIMATAIFA NA WADAU WA MAENDELEO

Na Waandishi Wetu, Dar

*Yasema inazingatia Haki za Binadamu na kuwawezesha wale watakaoondoka kwa hiyari katika maeneo hayo

Serikali imesema haitamzuia mtu yeyote anayetaka kuondoka kwa hiyari katika eneo la Ngorongoro kwenda kuishi popote nchini na kuwataka wadau wengine kutowazuia wanaotaka kuondoka katika eneo hilo.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damasi Ndumbaro ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo kuhusu mpango wa serikali wa kutafuta suluhu ya kudumu katika eneo la Ngorongoro na Loliondo na kuongeza kuwa itawawezesha wale wote wanaotaka kuondoka kwa hiyari katika maeneo hayo.

Dkt. Ndumbaro amewaeleza Mabalozi hao kuwa mpaka sasa jumla ya kaya 164 sawa na watu 915 wamejiandikisha kuondoka Ngorongoro kwa hiyari na kwenda kuishi katika maeneo mbadala watakayopewa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba ama kuwalipa fidia.

Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa Serikali imeamua kuchukua hatua hiyo ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza katika eneo la Ngorongoro ikiwa ni kuongeza kwa binadamu kutoka 8000 mwaka 1959 hadi kufikia 110,000 kwa sasa ikiambatana na ongezeko la mifugo kutoka mifugo 200,000 mwaka 1959 hadi kufikia mifugo 1,000,000 kwa sasa jambo linaloathiri ikolojia na uhifadhi, maendeleo ya utalii na maendeleo ya jamii ya wanaoishi Ngorongoro.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Fatma Rajabu amesema dhumuni la kuwaita Mabalozi hao pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa ni katika jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha Mabalozi na wadau wa Maendeleo wanapata taarifa sahihi kuhusu suala la Ngorongoro na Loliondo kutokana na kugubikwa na upotoshaji.

Ameongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeweka utaratibu wa kuzikutanisha Wizara za kisekta na  Mabalozi, Wakuu wa Masharika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo mara moja kila baada ya miezi 3 lengo likiwa ni kutoa fursa kwa Serikali kutoa ufafanuzi wa masuala mtambuka ya serikali na kuruhusu majadiliano yanayosaidia wadau hao kuwa na taarifa sahihi pamoja na kuwa na uelewa wa pamoja.

Akichangia mjadala huo, Balozi wa Ujerumani nchini, Mhe. Regina Hess ameunga mkono jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro ili kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damasi Ndumbaro akiongea na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo  (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiongea na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo  (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam  

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab akiongea na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damasi Ndumbaro (mwenye tai ya bluu) akiongoza mkutano kati ya Serikali na Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo  (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam. Wengine katika meza kuu ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Francis Michael pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab.

Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Norgaard Spandet akitoa maoni yake wakati wa mjadala kuhusu jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro

Balozi wa Ujerumani nchini, Mhe. Regina Hess akichangia mjadala kuhusu jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro


Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar akichangia mjadala kuhusu jitihada za Serikali za kulinda uhifadhi na mazingira katika eneo la Ngorongoro

Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Wadau wa Maendeleo wakifuatilia mkutano 

Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Wadau wa Maendeleo wakifuatilia mkutano 

Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Wadau wa Maendeleo katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mkutano wao leo Jijini Dar es Salaam



MKUTANO WA 15 WA BARAZA LA KISEKTA LA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA WAHITIMISHWA JIJINI DAR ES SALAAM


Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCAFS) leo tarehe 25 Machi 2022 umefikia tamati jijini Dar es Salaam.

Mkutano huu ambao umefanyika kwa kipindi cha siku 5 kuanzia tarehe 21 hadi 25 Machi 2022 umetimishwa katika ngazi ya Mawaziri ambapo awali, ulitangulia na Mkutano katika ngazi ya Wataalum Waandamizi uliofanyika tarehe 21 hadi 23 Machi 2022, na Makatibu Wakuu tarehe 24 Machi 2022. 

Miongoni mwa masuala yaliyojitokeza katika Mkutano huo ni pamoja na kujadili ripoti za; Usalama wa Chakula na Lishe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kupitia na kutathimini utekelezaji wa maagizo na maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa katika Mikutano ya awali ya Baraza la Mawaziri na Baraza la Kisekta, utekelezaji wa azimio la Malabo kuhusu Progaramu ya Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme - CAADP) pamoja na uwianishaji wa pembejeo za kilimo; maendeleo ya mifugo, uvuvi na ufugaji wa samaki katika Jumuiya.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo wa ngazi ya Mawaziri Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii Bw. Christophe Bazivamo ameeleza kuwa licha ya changamoto za Janga la UVIKO-Jumuiya imerekodi mafanikio makubwa katika utekelezaji wa makubaliano na maagizo ya Baraza la Kisekta na Baraza la Mawaziri. 

“Tumepiga hatua kubwa katika kuwezesha mazingira mazuri ya sekta ya kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji na upatikanaji wa pembejeo; kuimarisha utendaji wa minyororo ya thamani ya kilimo na biashara ya bidhaa za kilimo” Amesema Bazivamo. 

Kwa upande wake mwenyekiti wa mkutano huo na Katibu Mkuu wa Uvuvi, Kilimo na Uchumi wa Buluu wa Kenya Dkt. F.O. Owino akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uvuvi, Kilimo na Uchumi wa Buluu wa Kenya amepongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji mpango uwianishaji wa pembejeo za kilimo; maendeleo ya mifugo, uvuvi na ufugaji wa samaki katika Jumuiya. 

Vilevile Dkt. Owino amepongeza dhamira za nchi Wanachama wa Jumuiya ya kuweka katika mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya kilimo. Ameongeza kuwa uwekezaji huo utachochea ongezeko la ubora wa mazao na uzalishaji, sambamba na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo na hatimaye kukuza biashara ya kikanda na kimataifa ya mazao ya kilimo.

Bw. Bazivamo kwa niaba ya Mkutano huo amewashukuru Washirika wote Maendeleo wakiwemo USAID Kenya na Afrika Mashariki (USAID/KEA, Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA) na Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika lake la GIZ, Mpango wa Kuzuia na Kukabili Ugonjwa wa Mlipuko kwa msaada wao katika kuboresha sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula kwenye Jumuiya. 

Katika Mkutano huo Tanzania imewakilishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki ambaye pia aliongoza wa Ujumbe wa Tanzania, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Antony Peter Mavunde, Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi wa Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali. Aidha, Mkutano huo umehudhuriwa na nchi zote sita (6) Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki (Mb) ambaye pia alikuwa Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania akichangia hoja kwenye Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam. Machi 25, 2022
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Antony Peter Mavunde (Mb) akifuatilia Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam. Machi 25, 2022
Mkurugenzi Msaidizi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Benjamin Mwesiga (wakwanza kushoto) akifuatilia Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki akisaini ripoti ya Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam
Mawaziri walioshiriki Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki wakisaini ripoti ya Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Thursday, March 24, 2022

WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA UGANDA

Na Waandishi Wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amemuaga Balozi wa Unganda nchini Mhe. Richard Kabonero ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika tukio hilo Waziri Mulamula amempongeza Balozi Kabonero kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuendeleza na kudumisha uhusiano mzuri wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Uganda. 

Waziri Mulamula ametaja baadhi ya mafanikio ambayo yamepatika katika kipindi cha uwakilishi wake hapa nchini, kuwa ni pamoja na kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Choleani, Tanzania lenye urefu wa Kilomita 1443 na kukua kwa urari wa biashara kati ya Tanzania na Uganda.  

“Serikali kwa ujumla tunashukuru zaidi kwa ushirikiano uliotuonesha wakati wote ulipokuwa hapa kama Balozi na tunakuahidi kuudumisha na kuuendeleza ushirikiano huo kwa maslahi ya nchi zetu mbili (Tanzania na Uganda),” amesema Balozi Mulamula. 

Kwa upande wake Balozi Kabonero ameishukuru Serikali kwa kumpatia ushirikiano wakati wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake hapa nchini. 

“Naomba kuishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mlionipatia wakati wote nilipokuwa hapa kama balozi, kwa kweli nilifarijika sana kuwa nanyi……..naahidi kuwa balozi mwema wa Tanzania asante sana,” amesema Balozi Kabonero.

Tanzania na Uganda zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, nishati, elimu, pamoja na usafirishaji.

Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameshiriki katika Mkutano wa Nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ulifanyika kwa njia ya mtandao na kuongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angloa na Mwenyekiti wa ICGLR Balozi Tete Antonio.

Pia Waziri Mulamula ameshiriki kufunga Mkutano wa Mabalozi (Wastaafu) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiongea na Balozi wa Unganda nchini Mhe. Richard Kabonero ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zawadi Balozi wa Unganda nchini ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi Mhe. Richard Kabonero katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Unganda nchini aliyemaliza muda wake wa uwakilishi Mhe. Richard Kabonero pamoja na maafisa kutoka Ubalozi wa Uganda na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki   

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akishiriki katika Mkutano wa Nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ulifanyika kwa njia ya mtandao. Mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angloa na Mwenyekiti wa ICGLR Balozi Tete Antonio. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akionge na Mabalozi (wastaafu) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam




 

Wednesday, March 23, 2022

WAZIRI MULAMULA AFUNGUA MKUTANO WA WANAWAKE KATIKA DIPLOMASIA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo tarehe 23 Machi 2022 amefungua mkutano wa Wanawake katika Diplomasia (Women in Diplomacy) unaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati anafungua mkutano huo Waziri Mulamula amehimiza umuhimu wa kutumia Diplomasia katika kuleta amani na maridhiano katika jamii. “Ujumbe wangu kwenu katika siku hii muhimu ni kuwa, Diplomasia itumike sehemu yoyote kuanzia biashara, ngazi ya familia na katika shughuli zetu za kila siku” alisema Waziri Mulamula.

Waziri Mulamula alihitimisha hotuba yake kwa kuwapongeza waanzilishi wa Women in Diplomacy pamoja na washiriki kwa kuwa ni jukwaa muhimu la kujifunza na kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali katika eneo la Diplomasia na Uongozi. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifungua Mkutano wa Women in Diplomacy uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Waandaaji na Wagini waalikwa kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Women in Diplomacy uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifurahia jambo wakati akizungumza na Balozi Gertrude Mongela kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Women in Diplomacy

TANZANIA YAFAFANUA MSIMAMO WAKE KUHUSU MGOGORO WA URUSI NA UKRAINE

Na Mwandishi Wetu, Dar 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu sababu ya kupiga kura ya kutofungamana na upande wowote katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine huku ikisisitiza pande zote mbili kutafuta suluhu katika meza ya mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ametoa ufafanuzi huo wakati akifanya mahojiano na mojawapo ya vyombo vya Habari kutoka China na kuongeza kuwa Sera ya Tanzania kuhusu namna ya kutatua changamoto za migogoro inapojitokeza ni kwa kutumia njia za kidiplomasia.

Balozi Mulamula amesisitiza kuwa Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijabadilika tangu uhuru na kuongeza kuwa Tanzania inaamini hakuna mgogoro ambao hauwezi kutatulika  hasa panapokuwepo na utashi na nia njema ya kumaliza mgogoro na kwamba njia ya kidiplomasia ndio chaguo sahihi kwa Tanzania kuhusu namna bora ya kumaliza mgogoro  kati ya Urusi na Ukraine.

“Sisi msimamo wetu na Sera yetu na msingi wetu wa Sera yetu ya Mambo ya Nje ni kutofungamana na pande zozote, hivyo kutokupiga kura ni kuonesha msimamo wa Tanzania,” amesema Balozi Mulamula

Alipoulizwa endapo Tanzania imeathirika na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine, Balozi Mulamula amesema madhara yanayotokana na vita hiyo yanajionesha dhahiri huku akitaja baadhi ya madhara hayo kwa baadhi ya wanafunzi wa kitanzania waliokuwa wanasoma nchini Urusi kukatisha masomo yao na kurejea nchini wakisubiria vita kumalizika pamoja na ongezeko la bei ya petroli na gesi duniani.

Kutokana na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi Tanzania ililazimika kuwaondoa raia wake nchini Ukraine hususan wanafunzi takribani 300 waliokuwa wakisomea masuala ya udaktari nchini humo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mahojiano na moja ya vyombo vya Habari vya China. Mahojiano hayo yalifanyika kwa njia ya mtandao Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akihojiwa na mmoja wa waandishi wa habari kutoka China

Tuesday, March 22, 2022

MKUTANO WA 15 WA BARAZA LA KISEKTA LA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA KUFANYIKA DAR ES SALAAM


Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Maafisa Waandamizi umeanza kufanyika leo tarehe 21 Machi 2021 katika Hoteli ya Four Points, jijini Dar es Salaam. Mkutano huu wa siku tano (5) utakaofanyika kwa njia ya mseto (video na ana kwa ana) kuanzia tarehe 21 hadi 25 Machi 2022, unatarajiwa kuangazia masuala mbalimbali katika sekta ya kilimo yanayolenga kuhakikisha maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula ndani ya Jumuiya. 

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw. Christophe Bazivamo alibainisha umuhimu wa Mkutano huo kuangazia maeneo ya msingi ambayo yakifanyiwa kazi na nchi wanachama, Jumuiya itafikia lengo la kuwa na maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula. Ameyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni; kuweka na kutekeleza mikakati ya kuboresha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, kuwawezesha na kuwahimiza wanawake na vijana kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye sekta ya kilimo na kuhimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye kilimo ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.

“Nimatumaini yangu haya machache niliyo yabainisha hapa, na mengi ya muhimu ambayo wataalamu mtajadili kwa kina katika mkutano huu yatachangia kwa kiasi kikubwa kuchochea kasi ya ukuaji wa kilimo na kuleta mabadiliko chanya katika ustawi wa pamoja na kuboresha maisha Wanaafrika Mashariki” alisema Bw. Bazivamo

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mkutano huo Dkt. Mary Mwale kutoka Jamhuri ya Kenya akirejea takwimu zilizotolewa na Ripoti ya tatu ya Mpango Kamili wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme - CAADP) ya mwaka 2022 amewahimiza wataalamu wa kilimo katika Jumuiya kuzisaidia Serikali kuongeza nguvu na ubunifu katika kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo ambayo imeajiri asilimia 80 ya Idadi ya watu wote katika Jumuiya. 

Ripoti ya miaka mitatu ya CAADP iliyotolewa mwezi Machi 2022 imebainisha kuwa ukanda wa Afrika Mashariki isipokuwa Jamhuri ya Rwanda hazikufikia malengo yaliyoafikiwa kwenye mpango wa Afrika wa kufikia mabadiliko ya kilimo, uzalishaji mali, usalama wa chakula na lishe, ukuaji wa uchumi, na ustawi kwa wote. 

Jumuiya tuna kazi kubwa ya kufanya kwenye Sekta ya Kilimo, tunawajibu mkubwa wa kuhakikisha maendeleo ya kilimo yanakuwa endelevu na yenye tija ni muhimu pia kukumbuka kuwa 70% ya viwanda vya Jumuiya ya Afrika Mashariki vinategemea sekta ya kilimo, vikiwemo vya uzalishaji wa pembejeo za kilimo; wakati huo huo 65% ya bidhaa zinazouzwa katika Jumuiya zinatokana na kilimo na bidhaa za kilimo. alisema Dkt. Mwale

Mkutano huu wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika katika ngazi tatu; ngazi ya Wataalamu Waandamizi tarehe 21 na 23 Machi, Ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 24 Machi, na mwisho ngazi ya Mawaziri tarehe 25 Machi 2022. 

Mkutano huu umehudhuriwa na nchi zote sita (6) wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Bw. Patrick Gwediagi (wakwanza kushoto) ambaye pia ni Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Wataalamu Waandamizi akifuatilia Mkutano huo, uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw. Christophe Bazivamo akifungua Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Meza kuu wakifuatilia Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Bw. Hassan Mnondwa Afisa Biashara katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
 Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam
Dkt. Mary Mwale kutoka Jamhuri ya Kenya akiongoza Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.

Monday, March 21, 2022

TANZANIA, EU ZAKUTANA KUJADILI EPA

Na Mwandishi wetu, Dar

Serikali ya Tanzania imekutana na Umoja wa Ulaya (EU) kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) kati ya Umoja huo na Tanzania.

Akiongea wakati wa kikao cha wataalamu kutoka Tanzania na EU kilichofanyika Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema kikao hicho kinalenga kujadili makubaliano yaliyokwama awali kutokana na Tanzania kutokuwa tayari kuridhia baadhi vipengele vilivyomo kwenye mkataba huo.

Prof. Kahyarara amesema Tanzania haikukubaliana na baadhi ya vipengele vya mkabata wa EPA na kuona kuwa ni vigumu kuingia katika makubaliano ya mkataba huo kabla ya kurekebisha vipengele hivyo.

“Tumekaa na wataalamu wetu na wenyewe wamekuja na wataalamu wao, tutapitia kipengele kimoja baada ya kingine na tunaamini tutafika mwisho na kama tulivyo waambia wenzetu wa EU tunaona faida ya kufanya biashara na wao kwa maslahi ya pande zote mbili,” amesema Prof. Kahyarara  

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti amesema majadiliano hayo yanalenga kuangalia vipengele vya mkataba ambavyo Tanzania ilionesha mashaka  katika kikao kilichopita ili kuvipatia ufumbuzi na kusonga mbele kwa pamoja hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania sasa inatoa kipaumbele katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

“Itakumbukwa kuwa Tanzania inatekeleza diplomasia ya uchumi na wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya wanania ya kuja kuwekeza Tanzania na Afrika Mashariki, hivyo tukikamilisha majadiliano haya itakuwa ni jambo lenye maslahi kwa pande zote,” Amesema Balozi Fanti.  

Kikao cha leo kinatokana na mazungumzo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyafanya alipokuwa katika ziara ya kikazi nchini Ubelgiji ambapo alikutana na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Bw. Charles Michael mwezi Februari 2022.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti akiongea na washiriki wa kikao (hawapo pichani), kulia ni Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara katika kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti akiongea na washiriki wa kikao, kulia ni Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara katika kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam


Kikao kikiendelea 

Washiriki kutoka Tanzania na Umoja wa Ulaya wakiwa katika picha ya pamoja