Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki inaratibu ziara ya wiki mbili ya Mwekezaji Diapora kutoka
nchini Canada, Bw. Joseph Katallah ambaye ameonesha nia ya kuwekeza katika
miundombinu ya barabara.
Bw. Katallah anashirikiana na
Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani inayomilikiwa na Bw.
Rodney Zubrod ambayo imebuni teknolojia mpya ya ujenzi wa barabara za lami na madaraja yanayotumia teknolojia
hiyo. Pia teknolojia hiyo hutumia mabaki ya uchafu wa migodini na viwandani
hususani viwanda vinavyotengeneza alumina na vioo. Uchafu huo kitaalamu huitwa matope
mekundu.
Aidha, kampuni hiyo
imefanikiwa kuwa na bidhaa nyingine zaidi ya barabara katika nchi za Canada,
Uingereza na Uholanzi ambapo wametengeneza vifaa vya kuzimia moto, kupiga
plasta na kuzuia kutu kwenye majengo na matanki ya kuhifadhia bidhaa
mbalimbali.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi
wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago ameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na
Uchukuzi imefanikiwa kuwakutanisha wawekezaji hao na sekta za ujenzi nchini kwa
lengo la kuinadi teknolojia hiyo mbadala ya geopolymer na matumizi yake ambayo
imefanikiwa kwa kiasi kikubwa nchini Canada, Marekani na Uingereza.
Akaongeza kuwa Bw. Katallah ni
mmoja wa wanadiaspora ambaye amehamasika kurudisha ubunifu wake nyumbani.
Pamoja na kuonesha nia ya kuwekeza katika miundombinu ya barabara pia amewekeza
katika miradi ya kilimo, ujenzi wa shule (iitwayo shamba darasa kwa vijana
walioishia darasa la saba hadi kidato cha sita) pamoja na ujenzi wa barabara ya
mfano inayotumia teknolojia ya “nano” mkoani Singida.
Kadhalika uwezo wa teknolojia
hiyo mbadala ya Geopolymer kutumia uchafu wa migodini na viwandani ni sehemu ya
mikakati ya utunzaji wa mazingira. Bila kuathiri taratibu za ujenzi unatumika
sasa imeelezwa kuwa teknolojia hiyo mpya italeta unafuu wa gharama za ujenzi
kufuatia uwepo wa rasilimali za kutosha nchini na hivyo kuhitaji utaalamu na
vifaa.
Idara za ujenzi zilizokutana
na wawekezaji hao ni pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tarehe 28 Machi
2022; Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini –TARURA tarehe 30 Machi 2022; Ofisi
ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) tarehe 30 Machi 2022 na
Wakala wa Barabara Tanzania - TANROADS wanatarajia kukutana na wawekezaji hao
tarehe 1 Aprili 2022.
Pamoja na Mwekezaji huyo Diaspora anayeishi nchini Canada Wizara kupitia idara ya Diaspora inaendelea kuhamasishaji Diaspora wengine wenye
malengo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini na inawahakikishia ushirikiano
katika hatua za kurasimisha uwekezaji.
Mazungumzo yakiendelea. =================== Kikao kati ya Wawekezaji na Wakala wa barabara Vijijini na Mijini - TARURA kilichofanyika tarehe 30 Machi 2022 jijini Dodoma. |
Kikao kikiendelea |
Kikao kikiendelea. |