Thursday, April 7, 2022

BALOZI MULAMULA AZISIHI NCHI ZA EAC KUISHI KWA AMANI

Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amezisihi nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishi  kwa amani ili kuepukana na mauaji kama ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyotokea nchini Rwanda 1994.

Waziri Mulamula ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam katika kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Tanzania inaungana na Rwanda kukumbuka tukio hilo baya lililoacha makovu kwa rai wa Rwanda.

"Tunashukuru na tunathamini hatua zilizochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame kuijenga nchi na kuponya majeraha na makovu ya mauaji yale, ni tukio baya lilitokea, tunaomba lisijirudie tena katika nchi zetu,” amesema Balozi Mulamula.

Aidha balozi Mulamula ameongeza kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zina mikataba inayotuongoza kuzuia mauaji na kuishi kwa amani. 

Kwa upande wake Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba amesema wananchi wa Rwanda wanakumbuka tukio baya la kuuawa kwa ndugu zao lakini wanajivunia hatua zilizochukuliwa na viongozi wao na mafanikio yaliyopo leo nchini humo.

"Mauaji ya Kimbari yalituumiza sana kwa kupoteza ndugu zetu wasio na hatia lakini leo hii tunajivunia hapa tulipofika, kama taifa tumeendelea kujenga uzalendo na umoja,"amesema Balozi Karamba.

Nae Mratibu Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), nchini Tanzania, Zlatan Millisic alisema shirika hilo linatoa pole kwa kumbukizi hiyo mbaya katika historia ya Rwanda na kusema leo kumbukizi hiyo imetumika kuelimisha dunia kuwa chuki ni mbaya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika kumbukizi ya mauaji ya Kimbari, leo Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba akihutubia Wanyarwanda paomja na wageni mbalimbali waliojitokeza katika kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari

Balozi wa Comoro nchini, Mhe. Ahmed El Badaoui Mohamed Fakih akitoa hotuba yake katika kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994

Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić akitoa salamu za UN katika kumbukimbizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari 











Tuesday, April 5, 2022

MKUU WA MAJESHI YA ULINZI ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI AFRIKA KUSINI

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amewataka Watumishi wa Serikali wanaopata fursa ya kuiwakilisha nchi nje kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii huku wakijua wao ni wawakilishi wa nchi kwenye maeneo waliyopangiwa.


Jenerali Mabeyo ametoa rai hiyo hivi karibuni alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kwa lengo la kuwasalimia Watumishi wa Ubalozi huo.


Mkuu huyo wa Majeshi amesema kuwa, watumishi wa kada mbalimbali wanaopangiwa kufanya kazi kwenye Balozi za Tanzania au Mashirika ya Kikanda na Kimataifa wanatakiwa kutumia fursa hiyo kuiwakilisha nchi vizuri kwa kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa maslahi mapana ya Taifa.


“Nawapongeza kwa kuendelea kuiwakilisha nchi yetu vizuri hapa Afrika Kusini lakini nawahimiza mchape kazi kwa bidii na kuwa wazalendo kwa nchi yenu wakati wote”, alisisitiza Jenerali Mabeyo.


Kuhusu hali ya nchi, Jenerali Mabeyo amewaeleza Watumishi hao kwamba, hali ya nchi na mipaka yote ni salama na kuwahimiza kuendelea kuiombea nchi na Viongozi wote akiwemo Mhe. Rais ili hali ya amani na utulivu iliyopo iendelee kuwepo.


Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi amemshukuru Jenerali Mabeyo kwa kutenga muda wake na kuutembelea Ubalozi huo na kuielezea hatua hiyo kuwa ni heshima kubwa kwake binafsi na Watumishi wote wa Ubalozi.


Kadhalika, alimweleza kuwa hali ya ushirikiano wa Tanzania na Afrika Kusini ni nzuri ambapo nchi hizi zinaendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara, utalii, elimu, uwekezaji na ushirikiano katika kukuza lugha ya kiswahiili. 


Aliongeza kusema moja ya jukumu kubwa la Ubalozi ni kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Hivyo, Ubalozi unaendelea kukamilisha mpango mkakati wa kutekeleza dhana hiyo ili kuiwezesha Tanzania kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo nchini humo zikiwemo za biashara, uwekezaji na masoko kwa bidhaa za Tanzania.


Mhe. Jenerali Mabeyo alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao ulihusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambao ulifanyika jijini Pretoria kuanzia tarehe 01 hadi 03 Aprili 2022.

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi akimpokea Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo alipotembelea Ubalozi huo hivi karibuni. Jenerali Mabeyo alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao ulihusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambao ulifanyika jijini Pretoria kuanzia tarehe 01 hadi 03 Aprili 2022. 

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi akizungumza kumkaribisha Jenerali Mabeyo (hayupo pichani) Ubalozini.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Mhe. Jenerali Venance Mabeyo akizungumza na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini (hawapo pichani) alipoutembelea Ubalozi huo hivi karibuni. Kushoto ni ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola. Jenerali Mabeyo na wajumbe wengine kutoka Tanzania walikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa SADC
Mhe. Jenerali Mabeyo akizungumza
Mkutano kati ya Jenerali Mabeyo na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ukiendelea
Sehemu ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini wakimsikiliza Jenerali Mabeyo (hayupo pichani) alipowatembelea Ubalozini hapo
Sehemu nyingine ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini
Mhe. Balozi Milanzi akimkabidhi Jenerali Mabeyo zawadi ya saa kama ukumbusho kwa kutembelea Ubalozini hapo
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Milanzi
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Milanzi na Mhe. Balozi Kayola
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika nchini humo hivi karibuni


Monday, April 4, 2022

WAZIRI MULAMULA AFANYA MAZUNGUMZO NA WABUNGE WA EALA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Naibu Waziri Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk leo tarehe 4 Aprili 2022 wamekutana na kufanya mazungumzo na Wabuge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wa Tanzania yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

Akizungumza na Wabunge hao Waziri Mulamula amewapongeza kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kupitia chombo hicho muhimu katika Jumuiya, ya kuhakikisha Jumuiya inaendelea kustawi zaidi. Vilevile, Waziri Mulamula ametoa wito kwa wabunge hao kuendele kuwa wamoja katika kutetea, kufuatilia na kulinda maslahi ya Taifa na Jumuiya kwa ujumla. 

Wabunge hao ambao walifanya ziara ya kikazi Wizarani wameeleza kuridhishwa na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha,kupitia Wizara wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwasilisha kwa wakati ada ya unachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Ziara hiyo ililenga kubadilishana mawazo na uzoefu baina yao na Viongozi wa Wizara sambamba na kutoa mrejesho wa maendeleo ya masuala mbalimbali muhimu yanayoendelea katika Jumuiya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wa Tanzania yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akifuatilia mazungumzo na Wabuge wa Bunge la Afrika Mashariki wa Tanzania yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (wannne kushoto) Naibu Waziri Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (watatu kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Wabuge wa Bunge la Afrika Mashariki
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Dr. Abdullah Hasnuu Makame akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo kati ya Wabunge wa EALA, Waziri Mhe. Mulamula na Naibu Waziri Mhe. Mbarouk yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
 Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Adam Kimbisa akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo kati ya Wabunge wa EALA, Waziri Mhe. Mulamula na Naibu Waziri Mhe. Mbarouk yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

WAZIRI VICKY FORD AZINDUA MPANGO WA ‘SHULE BORA’ KIBAHA

Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford amezindua mpango wa elimu unaojulikana kama ‘Shule Bora’ Kibaha mkoani Pwani.

Mhe. Ford amesema mpango wa ‘Shule Bora’ utasaidia kuboresha elimu nchini Tanzania na utawasaidia zaidi ya watoto milioni nne, ambapo nusu yao watakuwa ni watoto wa kike.

“Elimu ni kipaumbele kwa Rais Samia pamoja na Waziri wa Mkuu wa Serikali ya Uingereza……….ni lengo la Serikali ya Uingereza kuisaidia watoto zaidi ya milioni 15 hapa Tanzania kupata elimu, lakini tumeanza na hawa wachache lakini pia tumezingatia usawa wa kijinsia ambapo nusu ya sehemu ya msaada huu utamnufaisha mtoto wa kike,” amesema Mhe. Ford.

Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa msaada wa pound milioni 180 zilizotolewa na Serikali ya Uingereza utasaidi sana kuboresha sekta ya elimu nchini kupitia mpango wa elimu wa 'Shule Bora'.

Prof. Mkenda amesema pamoja na mambo mengine, kuwa msaada wa Serikali ya Uingereza kupitia mpango huu wa elimu utasaidia sana kuboresha mazingira ya elimu nchini ikiwa ni pamoja nan miundombinu ya shule, vitabu na sheria pamoja na mitaala inayotumika kufundishia.

“………….‘Shule Bora’ itaiwezesha Serikali yetu kufanya mapitio ya Sera ya elimu ya 1978, kuboresha Sheria ya Elimu, kuboresha mitaala ya elimu, kuangalia idadi ya walimu pamoja na wakufunzi na wahadhiri,” amesema Prof. Mkenda

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Tamisemi, Mhe. David Silinde amemhakikishia Waziri Ford kuwa fedha zote za mpango wa elimu wa ‘Shule Bora’ zitatumika kama ilivyokusudiwa ili kuwawezesha watoto wa kitanzania kunufaika na elimu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akimkaribisha Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford katika viwanja vya shule ya msingi Mkoani ambapo mpango wa elimu wa 'Shule Bora' umezinduliwa 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiangalia baadhi ya vitu vilivyotengenezwa na watoto wa Shule ya Msingi Mkoani kabla ya uzinduzi wa mopango wa elimu wa 'Shule Bora'

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiangalia baadhi ya vitu vilivyotengenezwa na watoto wa Shule ya Msingi Mkoani kabla ya uzinduzi wa mpango wa elimu wa 'Shule Bora'


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford wakizindua mpango wa elimu wa 'Shule Bora' 


Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na wageni (hawapo pichani) baada ya uzinduzi wa mpango wa 'Shule Bora'





MKUTANO MAALUM WA 47 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA EAC NGAZI YA WATAALAM UMEFUNGULIWA JIJINI ARUSHA

Mkutano Maalum wa 47 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 4 hadi 6 Aprili 2022.

Mkutano huu unafanyika katika mpangilio ufuatao; tarehe 4 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Wataalam, tarehe 5 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu na tarehe 6 Aprili 2022 Mkutano Ngazi ya Mawaziri.

Pamoja na mambo mengine Mkutano Ngazi ya Wataalamu unaandaa taarifa ya masuala ya Fedha na Utawala itakayowasilishwa kwenye mkutano wa Makatibu Wakuu na baadae kwenye mkutano wa Mawaziri.


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Justin Kisoka (kushoto) akichangia hoja katika Mkutano  Maalum wa 47 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Ngazi ya Wataalam unaofanyika leo tarehe 4 Aprili 2022 jijini Arusha, Tanzania.
Kulia ni Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota akifatilia mkutano huo.


Mkutano ukiendelea, kulia ni ujumbe wa Tanzania ukifuatilia majadiliano katika mkutano huo.

Meza kuu ikiongoza Mkutano.

Mkurugenzi Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caroline Chipeta akifatilia majadiliano katika mkutano.

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania

Ujumbe kutoka taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ukifuatilia majadiliano.

 

WAZIRI FORD ARIDHISHWA NA UTOAJI HUDUMA ‘ENGENDERHEALTH’

Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford ameonesha kuridhishwa na utoaji wa huduma katika kituo cha afya EngenderHealth Tanzania kilichopo Yombo Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Ford ameoneshwa kuridhishwa na utoaji wa huduma jumuishi kwa familia, mama, watoto, vijana na watu wenye ulemavu wakati alipofanya ziara katika kituo cha EngenderHealth Tanzania ambacho kinafadhiliwa na Serikali ya Uingereza.

“Nimeridhika na utoaji wa huduma katika kituo hiki hasa baada ya kuongea na akina mama, vijana na watu wenye ulemavu kwa nyakati tofauti maelezo yao kwangu yanaonesha huduma ni nzuri na zinaridhisha,” amesema Waziri Ford

Pia nimeona mazingira ya kituo hiki pamoja na kuongea madaktari, wauguzi na watoa huduma kwa kweli wamenifariji kazi yao ni nzuri na nawaomba waendelee kufanya kazi kwa bidi bila kuchoka, ameongeza Waziri Ford

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa EngenderHealth Tanzania, Dkt. Moke Magoma ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ufadhili wa baadhi huduma katika kituo hicho na kuahidi kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidi na weledi katika kuwahudumia watanzania wanaotumia kituo hicho.

“Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya wafanyakazi wa kituo hiki tunakushukuru sana kwa ufadhili wa huduma za wahanga wa unyanyasaji na Watoto na watu wenye ulemavu huduma hii imekuwa na msaada mkubwa sana katika jamii, tunakuahidi kufanya kazi kwa bidi na weledi,” amesema Dkt. Magoma

Baadhi ya akina mama waliokuwa katika kituo hicho kwa ajili ya matibabu na huduma mbalimbali wameomba kuongezewa watumishi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa Pamoja na kujengewa kituo nmumuishi ambacho kitaweza kusaidia upatikanaji wa huduma zote katika eneo moja.

Kituo cha EngenderHealth Tanzania kanafadhiliwa na Serikali ya Uingereza katika huduma za mama, mtoto, vijana na wenye ulemavu hasa wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia, unyanyasaji wa watoto. 

Huduma nyingine zinazotolewa kituoni hapo ni pamoja na huduma jumuishi kwa familia, mama, Watoto, vijana na wenye ulemavu.

Waziri Ford yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 3 - 5 Aprili 2022.    

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akisalimiana na uongozi wa kituo cha Afya cha EngenderHealth mara baada ya kuwasili kituoni hapo Yombo Vituka Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na akina mama waliokuwa katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka wakati wakisubiria huduma za afya  





Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na mmoja wa wauguzi katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiongea na mmoja wa wauguzi katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka 

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibian Mhe. Vicky Ford akiwa katika kituo cha huduma ya macho, masikio na utengamao kwa mtoto  katika kituo cha afya cha EngenderHealth  Yombo Vituka 


Mhe. Zungu akutana na Rais Mwenza wa Bunge la Pamoja la EU na OACPS

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge la Umoja wa Ulaya yamekubaliana kuimarisha ushirikiano miongoni mwao na miongoni mwa wabunge wao. Hayo yameafikiwa tarehe 02 Aprili 2022 kwenye makao makuu ya Bunge la Umoja wa Ulaya nchini Ufaransa, wakati wa mazungumzo baina ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu na  Rais mwenza wa Bunge la Pamoja la Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS), Mhe. Prof. Carlos Zorrinho). 

Mazungumzo hayo yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 41 wa Bunge  la OACPS na EU  ambapo Mhe. Zungu anaongoza ujumbe wa Tanzania, viongozi hao walikubaliana pia kupitia Mabunge yao kuhakikisha kuwa uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na baina ya Bunge la Tanzania na Bunge la Umoja  wa Ulaya unaimarishwa zaidi.

Aidha, Mhe. Zungu alitumia fursa hiyo kumwalika Mhe. Zorrinho pamoja na  baadhi ya Wabunge wa Bunge la EU kuitembelea Tanzania na kujionea wenyewe hatua mbalimbali zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suhuhu Hassan katika kusukuma maendeleo ya Tanzania. Rais huyo mwenza wa Bunge la Pamoja la Ulaya na ACP alipokea mwaliko huo kwa furaha  na kuahidi kufanya ziara hiyo nchini siku zijazo akiambatana na baadhi wa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya. Alieleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi za kipaumbele kwa Umoja wa Ulaya na Bunge hilo linafurahishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tanzania kusimamia ajenda za maendeleo na ustawi wa jamii, hususan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha demokrasia na haki za binadamu.

Mhe. Zungu alimwomba mwenyeji wake huyo kuwahamasisha wawekezaji wa Ulaya waendelee kuja kuwekeza nchini kwenye masuala ya uchimbaji wa gesi na maeneo mengine, kwani Tanzania imebarikiwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji.

Viongozi hao walihitimisha mazungumzo yao kwa kusisitiza umuhimu wa kuongeza ushawishi wa mabunge yao kutoa miongozo itakayoimarisha ushirikiano baina ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, Carribean na Pacific pamoja na masuala yanayohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha amani eneo la ukanda wa maziwa makuu hususan nchini Msumbiji. Professa Zorrinho alieleza kuwa EU ina imani kubwa zaidi na Tanznaia katika masuala ya usuluhishi wa migogoro na kukuza amani duniani.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Zungu aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na kwenye Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga na maafisa wengine waandamizi wa Ubalozi na Bunge.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu  (kushoto) akisalimiana na Mhe. Professa Carlos Zorrinho, Rais mwenza wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU (kulia) wakati wa kikao chao kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili,2022 wakati wa Mkutano wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU unaoendelea Strassbourg.


 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mussa Assan Zungu (aliyesimama) akichangia katika moja ya kikao cha Bunge la Pamoja la OACPS na EU kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg, Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022. Mhe.Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu  (katikati kulia) akiwa katika kikao chake na Mhe. Professa Carlos Zorrinho, Rais mwenza (co-President) wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU (wa pili kushoto) wakati wa kikao chao kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022 wakati wa Mkutano wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU unaoendelea Strasbourg. Kulia mwa Mhe. Zungu ni Mhe. Jestas Nyamanga, Balozi wa Ubalozi wa Jamhuri wa Muungano nchini Ubelgiji na kwenye Umoja wa Ulaya (kulia) na maofisa wengine kutoka Bunge la Tanzania na Bunge la EU.


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu,  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Dkt George Pinto Chikoti, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya OACPS (kulia) na Mhe Balozi Jestas Abuok Nyamnaga (kushoto) nje ya ukumbi kunakofanyika Mkutano wa 60 wa Bunge la OACPS unaofanyika katika ofisi za Bunge la EU jijini Strasbourg, Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 29 Machi, 2022. Mhe. Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mussa Assan Zungu  (aliyesimama kulia) akibadilishana mawazo na mmoja wa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya wakati wa Mkutano wa 41 wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU uliofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022. Mhe. Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.