Na Mwandishi wetu, Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amezisihi nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuishi kwa amani ili kuepukana na mauaji kama ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyotokea nchini Rwanda 1994.
Waziri Mulamula ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam katika kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa Tanzania inaungana na Rwanda kukumbuka tukio hilo baya lililoacha makovu kwa rai wa Rwanda.
"Tunashukuru na tunathamini hatua zilizochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame kuijenga nchi na kuponya majeraha na makovu ya mauaji yale, ni tukio baya lilitokea, tunaomba lisijirudie tena katika nchi zetu,” amesema Balozi Mulamula.
Aidha balozi Mulamula ameongeza kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zina mikataba inayotuongoza kuzuia mauaji na kuishi kwa amani.
Kwa upande wake Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba amesema wananchi wa Rwanda wanakumbuka tukio baya la kuuawa kwa ndugu zao lakini wanajivunia hatua zilizochukuliwa na viongozi wao na mafanikio yaliyopo leo nchini humo.
"Mauaji ya Kimbari yalituumiza sana kwa kupoteza ndugu zetu wasio na hatia lakini leo hii tunajivunia hapa tulipofika, kama taifa tumeendelea kujenga uzalendo na umoja,"amesema Balozi Karamba.
Nae Mratibu Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), nchini Tanzania, Zlatan Millisic alisema shirika hilo linatoa pole kwa kumbukizi hiyo mbaya katika historia ya Rwanda na kusema leo kumbukizi hiyo imetumika kuelimisha dunia kuwa chuki ni mbaya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika kumbukizi ya mauaji ya Kimbari, leo Jijini Dar es Salaam |
Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba akihutubia Wanyarwanda paomja na wageni mbalimbali waliojitokeza katika kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari |
Balozi wa Comoro nchini, Mhe. Ahmed El Badaoui Mohamed Fakih akitoa hotuba yake katika kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 |
Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić akitoa salamu za UN katika kumbukimbizi ya miaka 28 ya mauaji ya Kimbari |