Wednesday, April 27, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAJIPANGA KUWAJENGEA UWEZO WATUMISHI WAKE

Na Waandishi wetu, Dodoma

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imejipanga kuwajengea uwezo wa kazi watumishi wake ili kuwawezesha kutekeleza kwa vitendo Diplomasia ya Uchumi.


Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Joseph Sokoine wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo Jijini Dodoma


“Tumekuwa na kikao cha Baraza la Wafanyakazi kama ilivyo kwa mujibu wa Sheria, kikao kilijadili pamoja na mambo mengine, bajeti ya Wizara kwa mwaka mpya wa fedha 2022/2023, kuboresha utendaji kazi wa Wizara pamoja na maslahi ya watumishi.


“Katika masuala tuliyojadili leo katika kuboresja maslahi ya wafanyakazi ni pamoja na eneo la mafunzo ili kuendelea kuwajengeauwezo watumishi wetu wa kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo,” amesema Balozi Sokoine  


Kwa upande wake Katibu wa TUGHE ngazi ya Taifa, Bw. Amani Msuya ameupongeza uongozi wa Wizara kwa kuyapa kipaumbele maslahi ya watumishi na kuwataka Watumishi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii na maarifa yote kwa maslahi mapana ya Taifa.


Naye Mwenyekiti wa TUGHE wa tawi la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Pilly Sukwa amesema kuwa kikao cha baraza kimejadili masuala ya Bajeti pamoja umuhimu wa kuboresha zaidi maslahi ya watumishi wa Wizara ili kuwaongezea morali ya kazi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwa tija na ufanisi zaidi.


“Katika eneo langu mimi kama mwenyekiti wa TUGHE hapa Wizarani ni kuhakikisha kuwa maslahi ya watumishi ikiwemo mishahara na maslahi mengine yamezingatiwa. Ninaishukuru Wizara mambo yote haya yamezingatiwa wakati wa mkutano huu wa Baraza,” amesema Bi. Sukwa.


Baraza la Wafanyakazi wa Wizara limefanyika kwa lengo kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2021/2022 na Makadirio ya Makisio ya Bajeti kwa Mwaka 2022/2023.


Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara, Balozi Joseph Sokoine akizungumza wakati wa kufungua Mkutano wa Baraza hilo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper jijini Dodoma tarehe 27 Aprili 2022. Pamoja na mambo mengine Mkutano huo ulipokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2021/2022 na Makadirio ya Makisio ya Bajeti ya Mwaka 2022/2023.
Balozi Sokoine (katikati) akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kushoto kwa Balozi Sokoine ni  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab akifuatiwa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Bw. Alex Mfungo. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara, Bi. Pilly Sukwa akifuatiwa na Katibu wa TUGHE, Bw. Hassan Mnondwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab naye akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakishiriki mkutano huo. Kutoka kulia ni Bw. Japhary Kachenje, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara, Balozi Caroline Chipeta, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria cha Wizara, Bw. Swalehe Chondoma, Mhasibu Mkuu wa Wizara na Balozi Agnes Kayola, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda.
Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Pilly Sukwa akizungumza wakati wa Mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi
Katibu wa TUGHE ngazi ya Taifa, Bw. Amani Msuya naye akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Sokoine (katikati walioketi) akiwa katika picha  na Ssehemu ya Wajumbe wa Baraza hilo
Picha ya pamoja  
Picha ya pamoja
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Justine Kisoka akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Mwaka 2021/2022 na Makadirio ya Makisio ya Bajeti ya Mwaka 2022/2023 kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi
Mjumbe wa Baraza ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi, Bw. Magabilo Murobi akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi
Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Abel Maganya naye akichangia hoja wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi.

 

Tuesday, April 26, 2022

JAMHURI YA KOREA YAAHIDI KUENDELEA KUSAIDIA MIRADI YA MAENDELEO NCHINI


Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea Mhe. Chung Eui-yong ameelezea kuwa Serikali ya nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara na reli, usafiri wa majini, kuendeleza kilimo, uchumi wa buluu, uvuvi katika bahari kuu na teknolojia ya habari na mwasiliano.

Waziri Chung ameeleza haya alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masahriki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ambaye yupo ziarani nchini Korea. 

Vilevile, Waziri Mulamula na Mwenyeji wake Mhe.Chung Eui-yong katika mazungumzo yao wamejadili kuhusu kuendelea kudumisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa hayo rafiki. Vilevile wamekubaliana kuendelea kuibua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Waziri Mulamula akiwa nchini humo anatarijia atashiriki sherehe za maadhimisho ya miaka 30 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea yatakayofanyika jijini Seoul tarehe 29 Aprili 2022. Tanzania na Korea zilianzisha uhusiano wa Kidiplomasia Aprili 29,1992. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Liberata na Rais wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA) Dkt. Sohn Hyuk-Sang wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Shirika hilo (kulia) na ujumbe wa Tanzania (kushoto)
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Liberata akiwa katika mazungumzo na Rais wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA) Dkt. Sohn Hyuk-Sang (wakwanza kulia) yaliyofanyika jijini Seoul, Korea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata akimkabithi picha ya wanyama wa mbugani (yakuchorwa) Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban Ki-moon wakiwa katika mazungumzo alipomtembelea ofisini kwake jijini Seoul, Korea.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea Mhe. Chung Eui-yong akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula walipokutana kwa mazungumzo jijini Seoul, Korea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban Ki-moon wakiwa katika mazungumzo alipomtembelea ofisini kwake jijini Seoul, Korea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea Mhe. Chung Eui-yong wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Seoul, Korea
Balozi wa Tanzania nchini Korea Mhe.Togolani Mavula akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Caesar Waitara akifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea Mhe. Chung Eui-yong alipomtembelea ofisini kwake jijini Seoul, Korea. 

TANZANIA KUENDELEA KUULINDA MUUNGANO ILI KUWAENZI WAASISI WAKE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka watanzania kuendelea kuwaenzi waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuulinda, kuuheshimu na kuusherehekea kwa kuwa una manufaa makubwa kwao ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.


Mhe. Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya Miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na wananchi kwa ujumla.


Mhe. Dkt. Mpango ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye sherehe hizo amesema kuwa, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao waasisi wake ni Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ni tunu ya taifa inayotakiwa kulindwa, kuheshimiwa na kusherehekewa kwani amani, umoja, usalama na mshikamano uliopo miongoni mwa watanzania unatokana na Muungano huo.


Pia, ameongeza kusema kuwa, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 58 ni mengi na ya kujivunia katika sekta zote za uchumi, utamaduni, siasa, elimu na ajira.


“Tutaendelea kuulinda Muungano wetu kwani una manufaa makubwa kwetu sisi kama taifa moja. Tunaposherehekea miaka 58 ya Muungano tunayo mengi ya kujivunia, biashara kati ya Watanzania imeimarika, raia wetu wanaweza kuishi popote bila tatizo lolote tuna amani na utulivu unaowawezesha wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii bila kikwazo chochote, alisema Mhe. Dkt. Mpango.


Halikadhalika Mhe. Mpango amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni wa kipekee duniani, umeendelea kuijengea heshima Tanzania tangu enzi za kupigania ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika hadi sasa.


“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuheshimika duniani kutokana na mchango wake kwenye medani za kimataifa. Tangu harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika Tanzania ilikuwa mstari wa mbele hadi sasa Tanzania imeendelea kuchangia vikosi vya kulinda amani kwenye nchi mbalimbali duniani na kushiriki kwenye usuluhishi wa migogoro. Tanzania itaendelea kunufaika kama nchi moja na fursa zote zinazotokana na mashirika ya kikanda na kimataifa ikiwemo SADC, EAC na Soko Huru la Biashara Huru barani Afrika “aliongeza kusema Mhe. Dkt. Mpango.


Wakati wa Maadhimisho hayo, Makamu wa Rais alizindua Kitabu Maalum cha Historia ya Muungano ambacho aliagiza kisambazwe kwenye Shule, Vyuo na Taasisi mbalimbali ili kuwawezesha wananchi hususan vijana kuuelewa Muungano.


Awali akizungumza kumkaribisha Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema maadhimisho ya mwaka 2022 ambayo ni ya kipekee yataambatana na midahalo na makongamano ya uelimishaji kuhusu Muungano ili kuhakikisha kila Mtanzania hususan vijana wanauelewa Muungano ambao ni tunu na urithi wa Wanzania.


Aidha, akitoa salamu kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdula amesema Mhe. Rais Mwinyi ameahidi kuendelea kuusimamia na kuulinda Muungano kwa nguvu zake zote na kwamba Muungano upo salama kwenye mikono yake na ya Mhe. Rais Samia.


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa Muungano upo salama na kwamba tayari kero za Muungano 18 kati ya 25 zimetatuliwa.


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ni moja ya Wizara za Muungano imeshiriki maadhimisho hayo yenye kaulimbiu isemayo “Miaka 58 ya Muungano: Uwajibikaji na Uongozi Bora; Tushiriki Sensa ya Watu na Anuani ya Makazi kwa Maendeleo Yetu”.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 26 Aprili 2022
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa sherehe za miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika jijini Dodoma tarehe 26 Aprili 2022
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akiwa miongoni mwa viongozi wa Serikali walioshiriki maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika jijini Dodoma tarehe 26 Aprili 2022
Sehemu ya Mabalozi na Wakuu wa Mashirika waliopo nchini wakiwa kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab akishiriki maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika Dodoma tarehe 26 Aprili 2022
Sehemu ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mwenye bendera ni Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Wizara, Bw. Salifius Mligo akifuatiwa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Alex Mfungo 
Sehemu nyingine ya Wakurugenzi wa Wizara kama wanavyoonekana kwenye picha. Wa kwanza kulia ni Bi. Lilian Kimaro, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika akifuatiwa na Balozi Caroline Chipeta, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria na Bi. Rosemary Jairo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama. 
Wakurugenzi kutoka Wizarani wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Wa kwanza kulia mwenye bendera mkononi ni Bw. Magabilo Murobi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi akifuatiwa na Bw. Justine Kisoka, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango
Sehemu nyingine ya washiriki kutoka Wizarani wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Mhe. Makamu wa Rais Dkt. Mpango akizindua kitabu maalum cha historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mhe. Makamu wa Rais akimkabidhi nakala ya kitabu mwakilishi wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania
Mhe. Makamu wa Rais akimkabidhi Mzee Hasanieli Mrema nakala ya kitabu. Mzee Mrema ni mmoja wa  wazee waliochanganya mchanga kuashiria kuasisiwa kwa Muungano
Mhe. Balozi Mbarouk akifurahia  jambo na Balozi Fatma mara baada ya maadhimisho kumalizika
Mhe. Balozi Mbarouk kwa pamoja na Balozi Fatma wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara walioshiriki maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania
Balozi Fatma akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi na Watumishi wa Wizara nje ya Ofisi Ndogo za Wizara zilizopo Chuo Kikuu cha Dodoma ambazo zilipambwa kipekee kwa ajili ya kuadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Picha ya pamoja
Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma (katikati) akiwa na sehemu ya timu ya Wakurugenzi Wanawake wa Wizara ya Mambo ya Nje wakifurahia miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Wa kwanza kushoto ni Balozi Caroline Chipeta, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Bi. Tagie Daisy Mwakawago, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora, Balozi Naimi Aziz, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika. Wa kwanza kulia ni Bi. Lilian Kimaro, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika akifuatiwa na Balozi Agnes Kayola, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda na Bi. Rosemary Jairo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama. 

 

Monday, April 25, 2022

WAZIRI MULAMULA ZIARANI NCHINI KOREA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameanza zaira ya kikazi katika Jamhuri ya Korea. Ziara hii ya siku tano inatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 25 hadi 29 Aprili 2022.

Ziara hii sambamba na kuboresha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, inalenga kujadili na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika sekta mbalimbali ikiwemo uchumi wa buluu, usafirishaji na uchukuzi, utamaduni na sanaa, teknolojia, elimu na biashara.

Waziri Mulamula akiwa nchini Korea, kwa nyakati tofauti anatarajia kuonana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo Waziri wa Mambo Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea Mhe. Chung Eui-Yong, Wanadiplomasia, viongozi wa Taasisi za Elimu na Mafunzo na Jumuiya ya Diapora. 

Vilevile, Waziri Mulamula akiwa jijini Seoul, Korea anatarajiwa kushiriki katika hafla ya siku ya maadhimisho ya Miaka 58 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maadhimisho haya hufanyika kila mwaka tarehe 26 Aprili.

Sambamba na hilo Waziri Mulamula atashiriki kwenye maadhimisho ya miaka 30 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Korea yatakofanyika jijini Seoul tarehe 29 Aprili 2022.

Waziri Mulamula katika ziara hii ameambatana na Watendaji mbalimbali wa Serikali akiwemo Dkt. Aboud S. Jumbe Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Balozi Caesar C.Waitara Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Magese Emmanuel Bulayi Mkurugezi wa Idara ya Uvuvi katika Wizara ya Uvuvi na Mhandisi Aaron Kisaka Mkurugenzi wa Idara ya Usafirishaji katika Wizara ya Uchukuzi na Ushafirishaji. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na ujumbe wa Tanzania aliombana nao katika ziara yake ya kikazi inayoendelea Jumhuri ya Korea. Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Korea. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Korea Mhe. Togolani Edriss Mavura baada ya kumkabidhi kifungashio chenye maudhui ya kutangaza Utalii wa Tanzania katika Ofisi za Ubalozi jijini Seoul, Korea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na ujumbe wa Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Chuo Kiku cha Wanawake cha EWHA (EWHA Womans University) walipotembelea Chou hicho kilichopo jijini Seoul, Korea. 
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Caesar C.Waitara akifuatilia mazungmzo yaliyokuwa yakiendelea kwenye ziara inayoendelea katika Jamhuri ya Korea. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Dkt. Aboud S. Jumbe akifafanua jambo kwenye ziara ianayoendelea Jamhuri ya Korea. 

Friday, April 15, 2022

DIASPORA AWAVUTIA WATAFITI WA MALIGHAFI ZA UJENZI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

Mtanzania anayeishi nchini Canada, ambaye ameonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini, Bw. Joseph Katallah amewavutia watafiti wa malighafi za ujenzi ambao ni wahadhiri katika fani za kemia, mazingira, sayansi na uhandisi wa raslimali za ujenzi kutoka Kampasi mbalimbali za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). 

Haya yamejiri leo terehe 14 Aprili 2022 wakati wa kikao kilichoongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaaam. Kikao hicho kilitokana na ombi la watafiti hao kutaka kukutanishwa na Diaspora huyo ambaye ameleta teknolojia ya “geopolymer” inayoweza kutumika katika ujenzi wa barabara.

Watalaamu hao kutoka UDSM wamejikita katika kutafiti malighafi za udongo wa mfinyanzi (clay), miamba madini, hewa ya ukaa (CO2) na taka za viwandani na sekta ya kilimo ambazo wanazitumia kuzalisha bidhaa na vifaa mbalimbali vya ujenzi bila kuhusisha matumizi ya saruji (Portland cement). Teknolojia hiyo ambayo ni asili ya “geopolymer” imepata mapokezi mazuri miongoni mwa wataalamu wa sekta ya ujenzi kupitia uwekezaji wa Bw. Katallah, inatajwa kuwa ni rafiki wa mazingira, inazalisha bidhaa za bei nafuu, zinazodumu kwa muda mrefu zikiwa pia na uwezo wa kukabiliana na madhara ya chumvi na fangasi vinayoathiri majengo mengi yaliyojengwa kwa saruji.

Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya timu ya watafiti wenzake, Dkt. Aldo Kitalika ambaye pia aliongoza ujumbe wa Wataalamu hao kwenye mazungumzo, alieleza jinsi alivyovutiwa na uzoefu na ujuzi wa Bw. Katallah katika sekta ya ujenzi na kueleza utayari wao wa kushirikiana naye kupitia tafiti ili kuongeza tija zaidi katika sekta ya ujenzi. 

“Tumevutiwa sana na teknolojia ya geopolymer ambayo kimsingi ni sehemu ya tafiti zetu tulizozifanya kwa kupima aina tofauti za malighafi za ujenzi ikiwemo udongo wa mfinyanzi (clay), madini ujenzi na taka za mimea kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu kama vile mikoa ya Iringa, Njombe, Dodoma, Pwani, Manyara, Kilimanjaro, Mwanza, Ruvuma, Tanga, Morogoro na mingine mingi.” amesema Dkt. Kitalika.

Timu hiyo ya watafiti ilionesha wasilisho lenye bidhaa kifani (prototypes) kama vile matofali ya ujenzi wa aina mbalimbali, matofali yanayohimili joto kali (refractory bricks), vigae (tiles), vyungu vya maua, vyungu kwa ajili ya matumizi ya viwandani (crucibles), na meza za jikoni (kitchen counter tops).

Bw. Katallah amekuwa nchini kwa wiki kadhaa kwa madhumuni ya uwekezaji kwa kushirikiana na Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani inayomilikiwa na Bw. Rodney Zubrod, ambaye ni mbunifu wa teknolojia ya geopolymer.Teknolojia hiyo hutumia mabaki ya uchafu wa viwanda na migodi yenye kutengeneza alumina na vioo. Uchafu huo hujulikana kitaalamu kama matope mekundu.

Umoja wa watafiti hao unaundwa na Dkt. Aldo Kitalika (DUCE), Dkt. Makungu Madirisha (Mwalimu Nyerere, Mlimani), Bw. Said Abeid (MRI, Dodoma), Dkt. Regina Mtei (Mwalimu Nyerere, Mlimani), Dkt. Petro Mabeyo (DUCE), Dkt. Silvia Mushi (DUCE) na Dkt. Elianaso Elimbinzi (MUCE). 

Mazungumzo hayo ni sehemu ya muendelezo wa utekelezaji wa mikakati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Kitengo cha Diaspora ya kuhamasisha Diaspora wenye malengo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini ili kutekeleza diplomasia ya uchumi.


Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Tagie Daisy Mwakawago akisitiza jambo kwenye kikao kilichoratibiwa na Wizara baina ya Bw. Joseph Katallah (Mwekezaji, Mtanzania anayeishi nchini Canada na ) na timu ya watafiti kutoka UDSM kilichofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaaam.
Timu ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakifuatalia mada iliyokuwa ikitolewa na Daipora (Mtanzania anayeishi nchini Canada) Bw. Joseph Katallah (hayuko pichani) kwenye mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaaam.
Mazungumzo yakiendelea
Bw. Joseph Katallah Mtanzania anayeishi nchini Canada akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Timu ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (hawapo pichani) yaliyofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Tagie Daisy Mwakawago (watano kushoto) na Bw. Joseph Katallah (wane kulia) Mtanzania anayeishi nchini Canada na Timu ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja. Waengine (wapili na watatu kulia) ni Maafisa wa Kitengo cha Diaspora
Dkt. Madirisha Makungu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo baina ya timu ya watafiti ya UDSM na Bw. Joseph Katallah yaliyofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaaam.