Friday, June 10, 2022

OACPS YATENGA EURO MILIONI 157 KUKOPESHA WAKULIMA KUONGEZA MNYORORO WA THAMANI MAZAO YA KILIMO

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akizungumzia maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 8 na 9 Juni 2022 ambapo alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula katika mkutano huo.

 

 


 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (aliyekaa katikati) akiwa na Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 8 na 9 Juni 202. Kushoto aliyekaa ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga na kulia aliyekaa ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani Bi Agnes Kiama.



 

Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) umetenga kiasi cha Euro milioni 157 kukopesha wadau wa kilimo katika nchi wanachama kwa masharti nafuu ili kuwekeza kwenye sekta ya kilimo na hivyo kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya kilimo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amesema hilo ni azimio mojawapo lililofikiwa katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 8 na 9 Juni 2022 ambapo alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.

Amesema kuwa wadau wa kilimo kutoka Tanzania wanaotaka mikopo hiyo ya masharti nafuu watatakiwa  kuomba fedha hizo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na kuweza kushiriki kikamilifu katika mkakati huo wa kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo

“ Mkutano umeazimia kuanzisha mkakati wa kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya kilimo, na ili kufanikisha azimio hilo Jumuiya imetenga Euro milioni 157 ambazo zitatoka kama mikopo ya masharti nafuu kwa wakulima ndani ya jumuiya yetu ya OACPS” alisema Balozi Sokoine na kuongeza kuwa wadau wa kilimo kutoka Tanzania wataweza kuomba fedha hizo kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji.

Amesema kuwa Ubalozi ukikamilisha taratibu za uombaji na utoaji wa mikopo hiyo utatoa kwa walengwa ili wafanye maombi ya mikopo hiyo.

Akiongelea mazimio mengine, Balozi Sokoine amesema kuwa ni kuidhinishwa kwa Tanzania katika nafasi ya Uenyekiti wa Kamati ya masuala ya Uvuvi kwa miaka miwili kuanzia 2022 hadi 2024 na hivyo kuwa mwenyeji wa  Mkutano wa Mawaziri wa masuala Uvuvi  unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2024.

“Hatua hii ni fursa kubwa kwa Tanzania katika kusimamia utekelezaji wa ajenda yake ya uchumi wa buluu na kukuza ushirikiano baina ya nchi za OACPS katika sekta ya uvuvi” alisema. 

Amesema Mkutano huo umejadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara ndani ya jumuiya wakati wa kuingiza bidhaa katika soko la Ulaya na kuja na mikakati  ya kutatua changamoto hizo kwa kufaya tathmini ya kina ili kuzielewa changamoto husika na kuanzisha mfumo wa utoaji tahadhari mapema kwa wafanyabiashara.

 Amesema azimio lingine ni kuanzisha Jukwaa Maalum la Wafanyabiashara ndani ya Jumuiya kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara, kubadilishana uzoefu na kukuza mtandao wa masoko ya bidhaa na huduma na kuongeza kuwa   Mkutano pia umeazimia kuunganisha nguvu ya Diaspora kwa kuanzisha jukwaa maalum la kuwezesha Diaspora kukaa pamoja na kubadilishana uzoefu kwenye masuala mbalimbali ikiwemo fursa za uwekezaji ndani ya Jumuiya na kutoa maoni na kufanyiwa kazi.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri la nchi wanachama wa OACPS ni chombo cha maamuzi cha Jumuiya hiyo ambacho kinahusika na utekelezaji wa maazimio yanayopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali. Baraza hilo linaundwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka kwa Nchi wanachama na hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili utekelezaji wa maazimio  yaliyofikiwa kutoka katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo.

 

 


Thursday, June 9, 2022

TANZANIA YAIKARIBISHA JUMUIYA YA OACPS KUADHIMISHA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI

Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine akimkabidhi kitabu cha kujifunzia lugha ya Kiswahili Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mwenyekiti wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS Mhe. Slyvie Baipo Temon uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022

 

Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine akimkabidhi kitabu cha kujifunzia kiswahili Balozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabalozi nchini Ubelgiji Mhe. Daniel Emery Dede wakati wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS jijini Brussels

Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine akimkabidhi kitabu cha kujifunzia kiswahili Katibu Mkuu wa  Jumuiya ya OACPS Bw. Georges Robelo Pinto Chikoti wakati wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (waliokaa katikati) katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za OACPS uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022. Waliokaa kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga na kulia ni mwakilishi wa Idara ya Ulaya na Marekani Bi. Agnes Kiama.


Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki walioshiriki Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) uliofanyika Brussels Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022.

Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) uliofanyika Brussels Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022 wakiendelea na mkutano huo.




 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amezikaribisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika Julai 7 2022.

Akitoa mwaliko huo katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, Balozi Sokoine amesema Lugha ya Kiswahili imeendelea kukua na hivyo kuwa na wazungumzaji wengi katika sehemu nyingi duniani.

Amesema Tanzania inajivunia uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni  (UNESCO) wa kuitambua na kuipa  Siku Maalum lugha ya Kiswahili hasa ikizingatiwa kuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa Tanzania.

Amesema Maadhimisho hayo yanatarajiwa kukuza zaidi na kuongeza matumizi ya lugha hiyo duniani.

"Leo hii Kiswahili sio lugha ya Taifa ya Tanzania pekee au katika nchi nyingine za Afrika bali pia ni lugha inayozungumzwa na watu wengi katika Afrika Mashariki, Kati na Kusini," alisema Balozi Sokoine. 

Ameongeza  kuwa Kiswahili sasa kinafudishwa katika zaidi ya vyuo vikuu 100 duniani na ni miongoni mwa lugha za kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika.

"Kwa niaba ya Ubalozi wa Tanzania hapa Brussels na Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu  tunawaalika rasmi nchi wanachama wa OACPS kuungana na Tanzania na  wadau wengine wa Kiswahili kuadhimisha kwa mara kwanza Siku ya Kiswahili duniani," alisema Balozi Sokoine.

Tanzania na Balozi zake zitaungana na wadau wa Kiswahili duniani  kuadhimisha kwa mara ya kwanza  Siku ya Kiswahili duniani. 

Katika Mkutano huo Balozi Sokoine alipata fursa ya kukabidhi vitabu vya awali vya kujifunzia lugha ya Kiswahili vilivyoungwa na Baraza la Kiswahili Tanzania kwa Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Mhe. Slyvie Baipo Temon  na  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabalozi nchini Ubelgiji ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati nchini Ubelgiji Mhe. Daniel Emery Dede.

Julai 7 ya kila mwaka ilitangazwa na UNESCO kuwa siku maalum ya Maadhimisho ya Kiswahili  duniani.

 


MKUTANO WA SADC WA WIZARA ZINAZOSHUGHULIKIA MASUALA YA JINSIA WAFANYIKA MALAWI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ameongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha ngazi ya Makatibu Wakuu wa Wizara zinazoshughulikia masuala ya Jinsia na Wanawake kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilichofanyika hivi karibuni jijini Lilongwe, Malawi.


Pamoja na mengineyo, kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali yakiwemo; Maboresho ya Program za SADC za masuala ya Jinsia kwa mwaka 2021/2022; Mpango wa Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika nyanja mbalimbali za Kikanda; Utekelezaji wa Mkakati wa Kikanda wa SADC; Mfumo wa Kukabiliana na Unyanyasaji wa Kijinsia wa mwaka 2018-2030; Wanawake katika Siasa na nafasi za maamuzi na hatua kuelekea Usawa wa Kijinsia kwenye Sekretarieti ya SADC.

Kikao hili kitafuatiwa na Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Jinsia na Wanawake wa Nchi Wanachama wa SADC. 


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zaynab  Chaula akishiriki Kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara zinazoshughulikia masuala ya Jinsia kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)  kilichofanyika hivi karibuni Lilongwe - Malawi. Wengine katika picha ni ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mkutano huo. Pichani ni Balozi Agnes R. Kayola, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Grace Mwangwa, Mkurugenzi Msaidizi na Bw. Timotheo Mgonja, Afisa Mkuu kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Picha ya pamoja ya wajumbe walioshiriki  
Kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara zinazoshughulikia masuala ya Jinsia kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)  kilichofanyika hivi karibuni Lilongwe - Malawi.hicho

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zaynab  Chaula  akizungumza jambo na Bi. Roselyn Makhumula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jinsia, Watoto, Watu wenye Ulemavu na Ustawi wa Jamii wa Jamhuri ya Malawi ambaye pia ni Mwenyekiti katika kikao hicho cha Makatibu Wakuu.


 

TANZANIA, SAUDI ARABIA ZAAHIDI USHIRIKIANO KATIKA ELIMU

Na Mwandishi Wetu, Dar

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ufalme wa Saudi Arabia zimeahidi kuendelea kushirikiana na kukuza sekta elimu kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Balozi Alsheryan amemhakikishia Balozi Mbarouk kuwa Saudi Arabia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya elimu ambapo kwa mwaka 2022 Saudi Arabia imetoa fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 80 wa kada mbalimbali. 

“Serikali yetu kwa kutambua mchango wa elimu, imetoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 80 wa kitanzania, hivyo ni rai yangu kwa watanzania kuchangamkia fursa hizo pindi zitakapotangazwa,” alisema Balozi Alsheryan

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ameahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Saudi Arabia katika kukuza na kuendeleza ushirikiano imara baina ya mataifa hayo uliodumu kwa muda mrefu. 

“Uhusiano wa Tanzania na Saudi Arabia umezidi kuimarika, pia tumefurahishwa na fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wetu na tunaahidi kutumia fursa hiyo kwa maendeleo ya taifa letu” amesema Balozi Mbarouk.

Ushirikiano wa Tanzania na Saudia Arabia ni wa muda mrefu ambapo mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana katika Nyanja za nishati na gesi, madini, utalii na kilimo, afya, elimu na kiutamaduni.


Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa Saudi Arabia hapa nchini