Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) uliofanyika Brussels Ubelgiji tarehe 7-9 Juni 2022 wakiendelea na mkutano huo. |
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amezikaribisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika Julai 7 2022.
Akitoa mwaliko huo katika Mkutano wa 114 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo, Balozi Sokoine amesema Lugha ya Kiswahili imeendelea kukua na hivyo kuwa na wazungumzaji wengi katika sehemu nyingi duniani.
Amesema Tanzania inajivunia uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wa kuitambua na kuipa Siku Maalum lugha ya Kiswahili hasa ikizingatiwa kuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa Tanzania.
Amesema Maadhimisho hayo yanatarajiwa kukuza zaidi na kuongeza matumizi ya lugha hiyo duniani.
"Leo hii Kiswahili sio lugha ya Taifa ya Tanzania pekee au katika nchi nyingine za Afrika bali pia ni lugha inayozungumzwa na watu wengi katika Afrika Mashariki, Kati na Kusini," alisema Balozi Sokoine.
Ameongeza kuwa Kiswahili sasa kinafudishwa katika zaidi ya vyuo vikuu 100 duniani na ni miongoni mwa lugha za kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika.
"Kwa niaba ya Ubalozi wa Tanzania hapa Brussels na Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu tunawaalika rasmi nchi wanachama wa OACPS kuungana na Tanzania na wadau wengine wa Kiswahili kuadhimisha kwa mara kwanza Siku ya Kiswahili duniani," alisema Balozi Sokoine.
Tanzania na Balozi zake zitaungana na wadau wa Kiswahili duniani kuadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Kiswahili duniani.
Katika Mkutano huo Balozi Sokoine alipata fursa ya kukabidhi vitabu vya awali vya kujifunzia lugha ya Kiswahili vilivyoungwa na Baraza la Kiswahili Tanzania kwa Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Mhe. Slyvie Baipo Temon na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabalozi nchini Ubelgiji ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati nchini Ubelgiji Mhe. Daniel Emery Dede.
Julai 7 ya kila mwaka ilitangazwa na UNESCO kuwa siku maalum ya Maadhimisho ya Kiswahili duniani.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.