Thursday, June 16, 2022

TANZANIA NA SWEDEN ZAAHIDI KUONGEZA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO

  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Sweden, Bw. Magnus Nilsson pembezoni mwa  Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika tarehe tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland

Mazungumzo ya viongozi hao yalihusu ushirikiano baina ya mataifa yao hususan kwenye sekta za biashara, mageuzi katika mifumo ya taasisi za umma, haki za wanawake na watoto.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana kufuatia misaada mbalimbali iliyotolewa na Serikali ya Sweden,  Waziri Mulamula amesema sekta ya nishati imepiga hatua kubwa nchini ambapo mashirika yote yanayosimamia sekta hiyo yameboresha utendaji wake pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Bw. Nilsson alieleza kuwa Sweden itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria baina yake na Tanzania pamoja na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano. 

Aidha, Bw. Nilsson ameahidi kuwa Serikali ya Sweden itaendelea kusaidia eneo la mageuzi ya kisekta ikiwa ni pamoja na kuziunganisha taasisi za Tanzania na Sweden zianzishe ushirikiano kwa lengo la kupeana uzoefu na kujenga uwezo.

Kadhalika, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mkazo katika masuala ya watoto, usawa wa jinsia na uhuru katika masuala ya siasa. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kushoto) amefanya mazungumzo wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sweden. Bw. Magnus Nilsson (kulia) pembezoni mwa Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic uliofanyika nchini Finland tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Sweden, Bw. Magnus Nilsson (wa pili kulia) akizungumza na Mheshimiwa Waziri Mulamula (hayupo pichani). Pamoja naye ni ujumbe alioambana nao alipokuwa nchini Finland kushiriki Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Mkutano ukiendelea, kushoto ni ujumbe wa Tanzania ulioambana na Mhe. Waziri Mulamula.

Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Finland mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Grace Alfred Olutu na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mazungumzo.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.