Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa,
licha ya wanachama wa Jumuiya ya Madola kufanya kazi nzuri katika kuimarisha
misingi ya demokrasia, amani na utawala bora katika nchi zao, bado kuna changamoto
nyingi zinazohitaji kutafutiwa ufumbuzi ili misingi hiyo ya maisha iweze
kufanya kazi kwa ukamilifu wake.
Ametoa kauli hiyo leo
tarehe 23 Juni 2022 jijini Kigali katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
Jumuiya ya Madola kilichukuwa kinajadili masuala ya demokrasia, amani na
utawala bora.
Waziri Mulamula
alizitaja baadhi ya changamoto hizo na kusisitiza umuhimu wa familia ya Jumuiya
ya Madola kuziangalia kwa makini na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu, kuwa ni
pamoja na migogoro isiyoisha, ukosefu wa usalama na udhaifu wa vyombo
vinavyosimamia masuala ya utawala wa sheria.
Balozi Mulamula katika
maelezo yake alitambua jitihada zinazofanywa na jumuiya za kikanda na kimataifa
za kutumia njia za kidiplomasia kuzuia migogoro na kuzisihi nchi za jumuiya
hiyo kongwe kurejea katika misingi yake ya awali, ili kuhakikisha kuwa amani na
utulivu vinatawala muda wote kwenye nchi hizo.
Aidha, Waziri Mulamula
alitumia mkutano huo wa Mawaziri wa Mambo ya Nje, kuzishauri nchi wanachama
kuangalia uwezekano wa kutumia taratibu za kujitathmini zinazotumika kwenye
jumuiya nyingine za kujipima kiutawala bora.
Alitoa mifano ya taratibu
hizo kuwa ni pamoja na Mpango wa Nchi za Afrika za Kujitathmini Kiutawala Bora
(APRM); mpango wa hiyari wa nchi zinazotekeleza malengo ya Maendeleo Endelevu
(SDGs) wa kujipima utekelezaji wa malengo hayo; mpango wa nchi wanachama wa
Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu wa kujitathmini kila baada ya
kipindi fulani.
Aliwafahamisha Mawaziri
wenzake kuwa, Tanzania imefanyiwa tathmini hivi karibuni na Baraza la Umoja wa
Mataifa la Haki za Binadamu na kupitia tathmini hiyo, Tanzania ilipata fursa ya
kueleza mazuri yaliyofanyika kuhusu utawala bora na haki za binadamu. Alisema
pia kuwa nchi yake ilipata fursa ya kujifunza mazuri ya nchi nyingine kuhusu
utawala bora.
Balozi Mulamula
alitihitimisha hotuba yake kwa kuwakumbusha Mawaziri kuhusu programu zilizobuniwa
na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola na umuhimu wa kuzihuisha na kuzipa nguvu.
Progaramu hizo ni pamoja na misaada katika uchaguzi ikiwa ni pamoja na
kuhamasisha nchi wanachama kuendesha chaguzi za huru na haki, kutoa misaada ya
kiufundi katika uandaaji wa sera, misaada katika programu za mabadiliko ya
sheria, kuunda taasisi imara za kitaifa za kusimamia masuala ya haki za
binadamu na kuzijengea nchi uwezo wa kutoa haki bila upendeleo.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.