Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Norway zaweka msisitizo wa kuimarisha ushirikiano kwenye Diplomasia ya Uchumi ili kuinua shughuli za maendeleo kwa mataifa hayo na kuboresha huduma kwa jamii.
Hayo yamesemwa wakati wa mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Norway, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim. Mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 17 Juni 2022 wakati wa ziara ya Mhe. Mulamula nchini Norway.
Waziri Mulamula alieleza kuwa Tanzania kupitia sera yake ya taifa na sera ya mambo ya nje imeweka mipango imara ili kuhakikisha inainua sekta za uzalishaji hususani sekta ya kilimo, biashara na utalii. Hivyo, maeneo hayo ni ya kipaumbele kwenye ushirikiano wake na mataifa mengine.
Hata hivyo, Tanzania kupitia sekta ya kilimo inaweza kuzalisha mazao ya biashara na hivyo kuongeza nafasi ya ajira kwa vijana sambamba na kuinua wanawake kiuchumi. Pia katika suala hilo akafafanua umuhimu wa kuwawezesha wanawake kwani wamekuwa mstari wa mbele kuzalisha mashambani na kuwa tegemeo kwa chakula cha familia na malezi kwa ujumla.
Aidha, akafafanua umuhimu wa ushirikishwaji na kujenga uwezo kwa makundi hayo mawili sambamba na uwezeshaji katika teknolojia ili kuyafikia malengo ya kitaifa ya uzalishaji na kuyafikia masoko ya bidhaa ya kimataifa.
Naye Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Norway alieleza kuwa Serikali yake kwasasa imeelekeza ushirikiano na mataifa mengine katika biashara badala ya utoaji wa misaada. Mabadiliko haya ni sehemu ya jitihada katika kuhakikisha mataifa rafiki ya Norway yanapiga hatua kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili za ushirikiano.
Kadhalika, Mhe.Tvinnereim alipongeza kwa jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha utendaji kazi. Moja ya mafanikio ya wazi katika hilo alisema ni kufikiwa kwa makubaliano kati ya serikali na Kampuni ya Equinor ya Norway inayojishughulisha na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi.
Pia akaongeza kusema Norway inafurahishwa na mikakati iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza uchumi wa bluu na kwamba ipo tayari kushirikiana katika hilo ili kuyafikia malengo yaliyowekwa kwakuwa inao uzoefu mkubwa katika sekta hiyo.
Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Norway, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim akizungumza na Mhe. Balozi Mulamula katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Norway tarehe 16 Juni 2022 jijini Oslo, Norway. |
Mazungumzo yakiendelea, Mhe. Tvinnereim na ujumbe wake. |
Mhe. Tvinnereim akimkabidhi zawadi ya kitabu cha Diplomasia, Mhe. Balozi Mulamula. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.