Wednesday, June 29, 2022

TANZANIA NA CUBA KUFUNGUA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Rodriguez Parrilla walipokutana kwa mazungumzo tarehe 29 Juni 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya Mhe. Parrilla kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Mhe. Waziri Balozi Liberata Mulamula.

Akifafanua dhumuni la ziara hiyo, Mhe. Balozi Mulamula ameeleza kuwa ziara hii inafanyika kwa lengo la kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo.  Maeneo mapya ya ushirikiano yanatarajiwa kufunguliwa katika sekta za kilimo, utalii, usimamizi wa masuala ya zimamoto na ukoaji, viwanda na biashara, na utamaduni na michezo.

“Urafiki na misingi ya kitaifa iliyowekwa na waasisi wa mataifa yetu imetuwezesha kuangalia namna bora ya kuimarisha ushirikiano wetu wa kidiplomasia katika kukuza sekta za maendeleo,” alisema Mhe. Balozi Mulamula.

Pia akaeleza umuhimu wa ushirikiano katika ya Tanzania na Cuba hususan wakati huu ambapo dunia inapitia changamoto mbalimbali ili kujenga mshikamano imara katika utatuzi wa changamoto hizo.

Vilevile akasisitiza umuhimu wa kuimarisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya mataifa hayo mawili ili maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa yaweze kusimamiwa na kupewa ufuatiliaji wa karibu kwa manufaa ya pande zote mbili.

Naye Mhe. Parrilla ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua ofisi ya Ubalozi nchini Cuba pamoja na mapokezi mazuri ya Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne.

Kadhalika, amefurahishwa kusikia habari za Filamu ya Tanzania the Royal Tour iliyonadiwa kwake na Mhe. Waziri Mulamula katika mazungumzo yao. Mhe. Parrilla aliahidi kuiangalia filamu hiyo ili kujifunza mazingira ya asili ya kitanzania na vivutio vya utalii vilivyotangazwa kupitia filamu hiyo.

Katika hatua nyingine viongozi hao wamekubaliana kuboresha utendaji wa kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha, Pwani ili malengo ya uwekezaji pamoja na yale ya kudhibiti malaria yaweze kufikiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Parrilla katika ofisi ndogo za Wizara tarehe 29 Juni 2022 jijini Dar es Salaam. 

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola, Afisa Mambo ya Nje, Bi. Salma Rajab na Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Seif Kamtunda wakifuatilia mazungumzo.


Mazungumzo yakiendelea.

Picha ya pamoja Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Parrilla
Mhe.Waziri Mulamula akimkabidhi zawadi ya picha ya Tingatinga Mhe. Parrilla.







No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.