Serikali ya Tanzania
imechangia kwa kiasi kikubwa jitihada za kuleta amani barani Afrika hususan
eneo la ukanda wa maziwa makuu, kupitia ushiriki wake katika kutatua migogoro
na kuchangia vikosi vya kulinda amani.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Fatma Mohammed Rajab alipozungumza leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi
wa warsha kuhusu Utatuzi wa Migogoro iliyotolewa na Wizara kwa Wajumbe wa
Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa lengo la kuwajengea
uwezo.
Amesema kuwa, kwa miaka mingi
Tanzania imeendeelea kushirikishwa kwenye utatuzi wa migogoro na kuchangia vikosi
vya kulinda amani kutokana na kuaminika kwake kikanda na kimataifa kwenye eneo
hilo na hii inatokana na hali ya amani
na utulivu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii iliyopo nchini.
“Jukumu la Wizara ni kusimamia
uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbalimbali na mashirika ya kikanda na
kimataifa kwa lengo la kulinda maslahi ya nchi. Ni kutokana na kutekeleza jukumu
hilo, Tanzania imeendelea kuaminika na kushirikishwa katika utatuzi wa migogoro
mbalimbali Afrika. Hiki ni kielelezo cha kuaminika”, amesema Balozi Rajab.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa amesema
kuwa viongozi wakiwemo Wabunge wanayo nafasi kubwa katika kuchangia amani
kupitia nafasi zao kwa kutoa elimu ya uzalendo kwa wananchi kwa kuwaelimisha
kutojiingiza kwenye masuala yanaweza kusababisha migogoro na uvunjifu wa amani
ndani ya jamii.
“Kila mmoja wetu atumie nafasi
yake kuzuia migogoro katika jamii ikiwemo ile inayosababishwa na siasa. Wizara
iendelee kutoa semina hizi na Kamati itaendelea kutoa ushirikiano na ushauri
unaohitajika kwa Wizara”, alisisitiza Mhe. Kawawa.
Akiwasilisha mada kuhusu “Utatuzi,
Udhibiti na Usuluhishi wa Migogoro” Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia
cha jijini Dar es Salaam, Dkt. Ally Masabo amesema ujenzi wa imani na kujiamini
kwa wananchi na siasa safi ni njia mojawapo ya kudhibiti migogoro ndani ya
jamii. Pia ameongeza kuwa, Tanzania ipo mstari wa mbele katika utatuzi wa
migogoro na uchangiaji wa vikosi vya ulinzi wa amani kutokana na ukweli kwamba
eneo lote linaloizunguka Tanzania likiwa salama nchi inanufaika zaidi.
“Tanzania ni nchi ya 13
ulimwenguni katika kuchangia walinzi wa amani na ya sita Afrika. Hii inatokana
na imani ya Tanzania kwamba amani ni chanzo cha maendeleo. Tanzania inaamini
kwamba nchi zinazotuzunguka zikiwa salama nchi inanufaika kuliko zikiwa katika
migogoro” amesema Dkt. Masabo.
Wakichangia mada hiyo, Wajumbe
hao wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wamepongeza utaratibu
wa Wizara wa kutoa semina za aina hiyo kwao na kuongeza kuwa, ipo haja kwa
Serikali kuwa na Program za uelimishaji umma kuanzia ngazi za chini kuhusu
umuhimu wa amani na madhara yanayotokana na migogoro katika jamii.
Pia wamesisitiza elimu ya
kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kwa kufanya kazi na kujishughulisha
itolewe kwa wingi ili kuepuka migogoro inayosababishwa na wananchi kutojishughulisha
na kusubiri Serikali iwanyie kila kitu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa akifafanua jambo wakati wa majadiliano kwenye mafunzo hayo. |
Mkurugenzi wa Idara wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akitoa neno la shukurani kwa jumbe wa kamati hiyo. |
Mhe. Cosato Chumi akichangia hoja wakati wa majadiliano, kulia ni Mhe. Janeth Masaburi akifatilia mafunzo. |
Sehemu ya Wajumbe wa kati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, kutoka kushoto ni Mhe. Bonnah Kamol na Mhe. Fakharia Shomar Khamis wakifuatilia uwasilishaji wa mada ya migogoro. |
Mhe. Abeid Ramadhani akichangia hoja wakati wa majadiliano kwenye mafunzo hayo. |
Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia, Dkt. Ally Masabo akiwasilisha mada ua udhibiti wa migogoro kwa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. |
Mafunzo yakiendelea, wa kwanza kulia ni Mhe. Stella Ikupa akifuatilia majadiliano. |
Mhe. Zahor Mohamed Haji akifafanua juu ya umuhimu wa mafunzo hayo kwa Waheshimiwa Wabunge na umuhimu wa kulinda kauli zao ili kuepuka kuwa vyanzo vya migogoro katika jamii na Taifa kwa ujumla. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.