Friday, June 24, 2022

UJUMBE WA JIMBO LA HAUT KATANGA WAFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na ujumbe kutoka jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walipotembelea Ofisi za Wizara jijini Dodoma. Ujumbe huo wa watu tisa unaongozwa na Gavana wa jimbo hilo Mhe. Jacques Kyabula Katwe

Ujumbe kutoka jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeanza zaira ya siku 4 ya kikazi nchini. Ujumbe huo wa watu tisa unaongozwa na Gavana wa jimbo hilo Mhe. Jacques Kyabula Katwe

Pamoja na masuala mengine ziara hiyo inalenga kujionea na kujifunza namna Tanzania inavyoendesha shughuli za kilimo cha mazao ya biashara na chakula. 

Ujumbe huo umeanza zaira yake nchini kwa kutembelea Taasisi mbalimbali za serikali sambamba na kuonana na kufanyamazungumzo na viongozi waandamizi wa Serikali ikiwemo Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko na Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab. Vilevile walipata fursa ya kutembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Akizungumza kwa nyakati tofauti Gavana Jacques Kyabula Katwe ameeleza kuwa ziara yake nchini imetokana na kutuvitiwa kwake na namna Tanzania ilivyopiga hatua ya maendeleo katika sekta mbalimbali hususan kilimo na usimamizi wa madini.

“Kwa muda mrefu nimekuwa nikifuatalia maendeleo ya kilomo cha Tanzania kiasi cha kuweza kujitosheleza kwa chakula na pia kubakiwa na ziada ya kuuza kwa nchi za nje zenye uhitaji, nikasema sasa niwakati muafaka wa kutembelea Tanzania ili mimi pamoja na timu yangu tuweze kujifunza na kuanzisha ushirikiano katika sekta ya kilimo”. Alisema Gavana Katwe

Balozi Fatma Rajab akizungumza na Gavana huyo pamoja na ujumbe wake walipomtembelea Ofisini kwakwe jijini Dodoma ameleeza kuwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na DRC umeendelea kuimarika daima hivyo niwakati muafaka kwa pande zote mbili kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara. 

“Tumekuwa tukishirikiana baina yetu, lakini pia kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambako sote ni wanachama na sasa ninayo furaha kubwa pia kona tuko wote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tuendelea kuboresha mazingira ya biashara ili watu waendeshe shughuli zao kwa urahisi na uhuru zaidi na kuweza kujiongezea kipato chao binafsi lakini pia pato la Serikali za pande zote mbili”. Amesema Balozi Fatma Rajab.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe alieleza kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara yake ipo tayari kushirikiana na Jimbo la Haut Katanga katika kuendeleza kilimo. Aliongeza kusema pamoja na Tanzania kuiuzia chakula DRC bado Tanzania haiiangali nchi hiyo kama soko bali kama mbia wa maendeleo. 

“Tupo tayari kushirikiana na DRC katika kilimo, tutafanya kila litakalowezekana kuwaongezea ujuzi ili kwa pamoja tuzalishe chakula cha kutosha; naamini Tanzania na DRC tukiungana kwa dhati katika kilimo tunaweza kuzalisha chakula kwa wingi zaidi na kuweza kulisha sehemu kubwa ya Dunia” Alisema Waziri Bashe

Waziri Biteko kwa upande wake amweleza Gavana Katwe kuwa Tanzania ipotayari kuendelea kushirikiana na DRC katika biashara ya madini. Aliendelea kueleza kuwa Tanzania ipo mikono wazi muda wote kupokea fursa za biashara za madini kutoa DRC. Aidha amemhakikishia Gavana Katwe kuwa Tanzania haina urasimu katika biashara na hiyo inawakaribisha wafanyabiashara kutoka DRC kuja nchini kuuza au kuongeza dhamani ya madini kwa kuwa uwezo huo kwa sasa Tanzania tunao.

Gavana Jacques Kyabula Katwe na ujumbe wake waliwasili nchini tarehe 22 Juni 2022 na kupokelewa na Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Dkt. Anselim Mosha. Wengine waliombatana na ujumbe huo kutoka nchini DRC ni Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Saidi Juma Mshana na Konseli Mkuu wa Tanzania jijini Lubumbashi Selestine Kakele. 
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (kushoto) na Gavana wa jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe (kulia) wakisalimiana alipotembelea Ofisi ya Wizara ya Kilimo jijini Dodoma
Gavana wa jimbo la Haut Katanga la DRC Mhe. Jacques Kyabula Katwe (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Dkt. Anselim Mosha (kushoto) alipowasili katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe na Gavana wa jimbo la Haut Katanga Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji mbalimbali wa Serikali kwenye Ofisi za Wizara ya Kilimo jijini Dodoma.
Gavana wa jimbo la Haut Katanga la DRC akiwa katika picha pamoja na Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali ya Tanzania Bungeni jijini Dodoma.
Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko na Gavana wa jimbo la Haut Katanga Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe na ujumbe wake wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji mbalimbali wa Serikali ya Tanzania jijini Dodoma
Gavana wa jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe (wa kwanza kulia) akiwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipotembelea Bunge hilo tarehe 23 Juni 2022. 
Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko (kulia) na Gavana wa jimbo la Haut Katanga la DRC Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe (kushoto) wakisalimiana alipotembelea Ofisi ya Wizara ya Madini jijini Dodoma
Gavana wa jimbo la Haut Katanga la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mheshimiwa Jacques Kyabula Katwe akielezea jambo wakati wa mazungumzo baina yake Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Madini

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.