Friday, June 17, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE, CRDB PLC ZASAINI MAKUBALIANO KUTENGENEZA MFUMO WA DIASPORA DIGITAL HUB

Na Mwandishi wetu, Dar

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Benki ya CRDB Plc wamesaini Hati ya Makubaliano ya kutengeneza Mfumo wa Kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora, (Diaspora Digital Hub).

Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Akiongea katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo Jijini Dar es Salaam, Balozi Sokoine amesema mfumo huo wa kidigitali utaisaidia Serikali kuwatambua, kuwasajili na kuwawezesha Diaspora wa Tanzania waliopo sehemu mbalimbali ulimwenguni kupata huduma mbalimbali na kushiriki kidigitali katika shughuli mbalimbali za maendeleo, biashara, uchumi na uwekezaji.

“Ushirikiano wa Wizara na Benki ya CRDB Plc ni wa muda mrefu na wenye mafanikio mengi katika kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo ya Tanzania. Wizara ina imani kuwa kupitia udhamini wa shilingi milioni 100 kutoka CRDB za kutengeneza mfumo wa Diaspora Digital Hub utaboresha huduma mbalimbali zenye kukidhi mahitaji ya Diaspora kote ulimwenguni,” amesema Balozi Sokoine

Balozi Sokoine ameongeza kuwa, mfumo huo pamoja na mambo mengine, utafungua uwezekano wa fursa zaidi za ushirikiano kati ya Wizara na Benki ya CRDB katika kazi ya uendelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya Balozi za Tanzania nje ya nchi.

Balozi Sokoine ameyataja baadhi ya mafanikio ya mfumo huo ambayo ni kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Tanzania kuhamasisha taasisi na watumishi wake kutumia ipasavyo mifumo ya kidigitali katika kutoa huduma ili kuendana na mabadiliko ya dunia na kuongeza tija katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela amesema CRDB inaamini kuwa kuanza kwa Mfumo wa Kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub) utakuwa na manufaa mengi kwa Serikali na Benki ya CRDB kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kusaidia kufahamu idadi ya Diaspora walioko ulimwenguni na kutunza taarifa za watanzania walioko nje.

“Diaspora Digital Hub itasaidia pia kupata taarifa za fursa za uwekezaji nchini na kuwatambua wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini, kuisaidia Serikali katika zoezi la sensa litakalo fanyika mwezi Agosti, 2022, kusaidia kupata taarifa sahihi za pamoja na kuisaidia Wizara kupanga bajeti yake” amesema Bw. Nsekela

Bw. Nsekela ameongeza kuwa mfumo huo wa kidigitali utaisaidia Benki ya CRDB kuboresha zaidi huduma zake na kuwafikia wateja wengi wakiwemo Diaspora waliopo ulimwenguni.

“CRDB inaahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kuhakikisha mfumo wa kidigitali wa Diaspora Digital Hub unakamilika kwa wakati,” amesema Bw. Nsekela

Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akizungumza katika hafla hiyo amesema Mfumo wa kidigitali wa Diaspora Digital Hub utakapokamilika utaiwezesha Serikali kuwa na kanzidata ya uhakika kuhusu Diaspora kote ulimwenguni.

“Mfumo huu pia utaiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa njia ya kidigitali ambapo uratibu wa masuala mbalimbali yanayotolewa katika mfumo huo utafanyika papo kwa papo.

Balozi Bwana aliongeza kuwa kupitia mfumo huo Serikali itaweza kufahamu kwa ufasaha idadi ya Diaspora, ujuzi, elimu walizonazo na mengine mengi. Kadhalika, Diaspora wenyewe wataweza kupata kupitia mfumo huo huduma mbalimbali kwa ajili ya mahitaji yao.

Ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Benki ya CRDB ni wa muda mrefu tangu 2010 wakati Kitengo cha Diaspora kilipoanzishwa. Ushirikiano huo umewezesha Benki ya CRDB PLC kuwa ya kwanza kuanzisha utoaji wa huduma kwa Diaspora ambapo hadi sasa zaidi ya Diaspora 30,000 wananufaika na huduma ya Tanzanite Account.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiongea katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela akiongea wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza 'Diaspora Digital Hub' leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiongea katika hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora  


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela wakisaini Hati ya makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela wakionesha Hati ya makubaliano baina ya Wizara na CRDB ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora baada ya kumaliza kusaini hati hiyo




Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela wakibadilishana Hati ya Makubaliano ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora



Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Fedha katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Swalehe Chondoma wakifuatilia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Plc, Bw. AbdulMajid Nsekela katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi kutoka Wizarani na wafanyakazi wa Benki ya CRDB baada ya kusainiwa kwa Hati ya makubaliano 



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.