Helsinki, 14 Juni 2022
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amewasili nchini Finland kwa ziara ya siku 3 kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic (NORDIC-AFRICA) unaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.
Mkutano
huo umeanza na hafla ya ufunguzi iliyofanyika tarehe 13 Juni 2022, ambapo mgeni
rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto.
Akiwakaribisha
wajumbe wa mkutano huo Mhe. Haavisto alisisitiza umuhimu wa kuimarisha
ushirikiano katika kujiletea maendeleo baina ya nchi hizo marafiki.
Aidha,
mkutano huu utahusisha nchi 5 za Nordic ambazo ni Finland mwenyeji wa mkutano
wa sasa, Sweden, Norway, Iceland na Denmark na nchi za Afrika 25 marafiki wa
Nordic.
Mkutano
huo wa Mawaziri wa Mambo ya Nje utahusisha Mabalozi wa nchi shiriki za Afrika
zinazowakilisha katika nchi za Nordic na Mabalozi wa nchi za Nordic
wanaowakilisha katika Nchi shiriki za Afrika.
Wazo la
kuanzisha mkutano huu lilianza mwaka 2000 ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika
nchini Sweden mwaka 2001. Baada ya hapo mikutano kama hii inafanyika kwa
kupokezana kutoka Bara la Afrika na upande wa Nordic.
Mwaka
2019 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huu ambapo nchi takribani 34
zilishiriki katika mkutano.
Wakati
huo huo Mhe. Waziri Mulamula ametumia fursa ya ziara hiyo kutembelea Makao
Makuu ya Ofisi ya Mpango wa usimamizi wa migogoro nchini Finland na kukutana na
uongozi wa mpango huo. Lengo la likiwa kujadili masuala ya amani na usalama
katika ukanda wa Afrika Mashariki na ukanda wa kusini mwa Afrika.
Katika
mazungumzo yake Waziri Mulamula ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuwa mstari
wa mbele katika kusimamia masuala ya amani na usalama ili kuwezesha nchi za
ukanda huo kufanya shughuli za kiuchumi na kuinua maendeleo ya taifa na
wananchi kwa ujumla.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.