Thursday, June 2, 2022

TANZANIA KUENDELEA KUCHANGIA OPERESHENI ZA ULINZI WA AMANI

Na Mwandishi wetu, Dar

Katika jitihada za kuwaunga mkono walinda amani, Tanzania imeahidi kuendelea kuchangia zaidi katika operesheni za ulinzi wa amani duniani ili kuendelea kunufaika na matunda ya amani.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipohutubia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.   

“Walinda amani wa Umoja wa Mataifa ni kiungo muhimu katika mfumo wa amani na usalama wa dunia kwani wamejitolea maisha yao kutumikia katika hali ngumu ili mamilioni ya watu ulimwenguni waishi kwa amani,” amesema Balozi Mulamula. 

Balozi Mulamula ameongeza kuwa nchi nyingi duniani zimekuwa zikifanya kazi kwa bidii ili kutekeleza na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo 2030, amani ni sehemu muhimu katika azma hiyo. 

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuendelea kupaza sauti katika kuhakikisha amani inapatikana duniani kama kaulimbiu ya mwaka huu inavyosisitiza, ni juu yetu kuchukua jukumu hili kwa pamoja, kutafuta misingi ya pamoja, kuzingatia umuhimu wa mazungumzo na upatanishi kama njia ya kutatua migogoro kwa njia za amani.

“Tanzania inajivunia kushika nafasi ya 13 kwa mchango mkubwa katika operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa duniani. Hadi Machi mwaka huu, Tanzania imechangia walinda amani 1,485 katika nchi za  Lebanon, Afrika ya Kati, Sudan Kusini  na DRC ambapo matokeo chanya ya uwepo wao katika nchi hizi yameonekana,” ameongeza Balozi Mulamula.

Awali akihutubia maadhimisho hayo kwa Niaba ya Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić ameipongeza Tanzania kwa kuungana na Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani.

“Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika jitihada za kuendelea kuchangia walinda amani katika mataifa mbalimbali ikiwemo DRC, Lebanon na Sudani Kusini, Amesema Bw. Milišić na kuongeza kuwa amani ni ustawi wa maendeleo kwa taifa lolote lile duniani. 

Pamoja na mambo mengine, Bw. Milišić amesema Umoja wa Mataifa unatambua mchango wa Tanzania katika kulinda amani ndani ya nchi na amani katika mataifa mengine.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongoza viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mabalozi katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa  katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiweka ua katika  mnara wa Mashujaa uliopo Mnazi mmoja wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić  pamoja na baadhi wa viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiimba nyimbo ya taifa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa  

Meza kuu wakifuatilia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa  

Sehemu ya Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wakifuatilia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa 

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić akiwasilisha hotuba yake katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa

Mabalozi pamoja na maafisa waandamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama katika picha ya pamoja 




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.