Wednesday, March 23, 2022

WAZIRI MULAMULA AFUNGUA MKUTANO WA WANAWAKE KATIKA DIPLOMASIA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo tarehe 23 Machi 2022 amefungua mkutano wa Wanawake katika Diplomasia (Women in Diplomacy) unaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati anafungua mkutano huo Waziri Mulamula amehimiza umuhimu wa kutumia Diplomasia katika kuleta amani na maridhiano katika jamii. “Ujumbe wangu kwenu katika siku hii muhimu ni kuwa, Diplomasia itumike sehemu yoyote kuanzia biashara, ngazi ya familia na katika shughuli zetu za kila siku” alisema Waziri Mulamula.

Waziri Mulamula alihitimisha hotuba yake kwa kuwapongeza waanzilishi wa Women in Diplomacy pamoja na washiriki kwa kuwa ni jukwaa muhimu la kujifunza na kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali katika eneo la Diplomasia na Uongozi. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifungua Mkutano wa Women in Diplomacy uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Waandaaji na Wagini waalikwa kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Women in Diplomacy uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifurahia jambo wakati akizungumza na Balozi Gertrude Mongela kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Women in Diplomacy

TANZANIA YAFAFANUA MSIMAMO WAKE KUHUSU MGOGORO WA URUSI NA UKRAINE

Na Mwandishi Wetu, Dar 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu sababu ya kupiga kura ya kutofungamana na upande wowote katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine huku ikisisitiza pande zote mbili kutafuta suluhu katika meza ya mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) ametoa ufafanuzi huo wakati akifanya mahojiano na mojawapo ya vyombo vya Habari kutoka China na kuongeza kuwa Sera ya Tanzania kuhusu namna ya kutatua changamoto za migogoro inapojitokeza ni kwa kutumia njia za kidiplomasia.

Balozi Mulamula amesisitiza kuwa Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijabadilika tangu uhuru na kuongeza kuwa Tanzania inaamini hakuna mgogoro ambao hauwezi kutatulika  hasa panapokuwepo na utashi na nia njema ya kumaliza mgogoro na kwamba njia ya kidiplomasia ndio chaguo sahihi kwa Tanzania kuhusu namna bora ya kumaliza mgogoro  kati ya Urusi na Ukraine.

“Sisi msimamo wetu na Sera yetu na msingi wetu wa Sera yetu ya Mambo ya Nje ni kutofungamana na pande zozote, hivyo kutokupiga kura ni kuonesha msimamo wa Tanzania,” amesema Balozi Mulamula

Alipoulizwa endapo Tanzania imeathirika na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine, Balozi Mulamula amesema madhara yanayotokana na vita hiyo yanajionesha dhahiri huku akitaja baadhi ya madhara hayo kwa baadhi ya wanafunzi wa kitanzania waliokuwa wanasoma nchini Urusi kukatisha masomo yao na kurejea nchini wakisubiria vita kumalizika pamoja na ongezeko la bei ya petroli na gesi duniani.

Kutokana na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi Tanzania ililazimika kuwaondoa raia wake nchini Ukraine hususan wanafunzi takribani 300 waliokuwa wakisomea masuala ya udaktari nchini humo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mahojiano na moja ya vyombo vya Habari vya China. Mahojiano hayo yalifanyika kwa njia ya mtandao Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akihojiwa na mmoja wa waandishi wa habari kutoka China

Tuesday, March 22, 2022

MKUTANO WA 15 WA BARAZA LA KISEKTA LA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA KUFANYIKA DAR ES SALAAM


Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Maafisa Waandamizi umeanza kufanyika leo tarehe 21 Machi 2021 katika Hoteli ya Four Points, jijini Dar es Salaam. Mkutano huu wa siku tano (5) utakaofanyika kwa njia ya mseto (video na ana kwa ana) kuanzia tarehe 21 hadi 25 Machi 2022, unatarajiwa kuangazia masuala mbalimbali katika sekta ya kilimo yanayolenga kuhakikisha maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula ndani ya Jumuiya. 

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw. Christophe Bazivamo alibainisha umuhimu wa Mkutano huo kuangazia maeneo ya msingi ambayo yakifanyiwa kazi na nchi wanachama, Jumuiya itafikia lengo la kuwa na maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula. Ameyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni; kuweka na kutekeleza mikakati ya kuboresha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, kuwawezesha na kuwahimiza wanawake na vijana kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye sekta ya kilimo na kuhimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye kilimo ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.

“Nimatumaini yangu haya machache niliyo yabainisha hapa, na mengi ya muhimu ambayo wataalamu mtajadili kwa kina katika mkutano huu yatachangia kwa kiasi kikubwa kuchochea kasi ya ukuaji wa kilimo na kuleta mabadiliko chanya katika ustawi wa pamoja na kuboresha maisha Wanaafrika Mashariki” alisema Bw. Bazivamo

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mkutano huo Dkt. Mary Mwale kutoka Jamhuri ya Kenya akirejea takwimu zilizotolewa na Ripoti ya tatu ya Mpango Kamili wa Maendeleo ya Kilimo Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme - CAADP) ya mwaka 2022 amewahimiza wataalamu wa kilimo katika Jumuiya kuzisaidia Serikali kuongeza nguvu na ubunifu katika kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo ambayo imeajiri asilimia 80 ya Idadi ya watu wote katika Jumuiya. 

Ripoti ya miaka mitatu ya CAADP iliyotolewa mwezi Machi 2022 imebainisha kuwa ukanda wa Afrika Mashariki isipokuwa Jamhuri ya Rwanda hazikufikia malengo yaliyoafikiwa kwenye mpango wa Afrika wa kufikia mabadiliko ya kilimo, uzalishaji mali, usalama wa chakula na lishe, ukuaji wa uchumi, na ustawi kwa wote. 

Jumuiya tuna kazi kubwa ya kufanya kwenye Sekta ya Kilimo, tunawajibu mkubwa wa kuhakikisha maendeleo ya kilimo yanakuwa endelevu na yenye tija ni muhimu pia kukumbuka kuwa 70% ya viwanda vya Jumuiya ya Afrika Mashariki vinategemea sekta ya kilimo, vikiwemo vya uzalishaji wa pembejeo za kilimo; wakati huo huo 65% ya bidhaa zinazouzwa katika Jumuiya zinatokana na kilimo na bidhaa za kilimo. alisema Dkt. Mwale

Mkutano huu wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika katika ngazi tatu; ngazi ya Wataalamu Waandamizi tarehe 21 na 23 Machi, Ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 24 Machi, na mwisho ngazi ya Mawaziri tarehe 25 Machi 2022. 

Mkutano huu umehudhuriwa na nchi zote sita (6) wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Bw. Patrick Gwediagi (wakwanza kushoto) ambaye pia ni Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Wataalamu Waandamizi akifuatilia Mkutano huo, uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Huduma za Jamii katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw. Christophe Bazivamo akifungua Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Meza kuu wakifuatilia Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
Bw. Hassan Mnondwa Afisa Biashara katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa kwenye Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.
 Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam
Dkt. Mary Mwale kutoka Jamhuri ya Kenya akiongoza Mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.

Monday, March 21, 2022

TANZANIA, EU ZAKUTANA KUJADILI EPA

Na Mwandishi wetu, Dar

Serikali ya Tanzania imekutana na Umoja wa Ulaya (EU) kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) kati ya Umoja huo na Tanzania.

Akiongea wakati wa kikao cha wataalamu kutoka Tanzania na EU kilichofanyika Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema kikao hicho kinalenga kujadili makubaliano yaliyokwama awali kutokana na Tanzania kutokuwa tayari kuridhia baadhi vipengele vilivyomo kwenye mkataba huo.

Prof. Kahyarara amesema Tanzania haikukubaliana na baadhi ya vipengele vya mkabata wa EPA na kuona kuwa ni vigumu kuingia katika makubaliano ya mkataba huo kabla ya kurekebisha vipengele hivyo.

“Tumekaa na wataalamu wetu na wenyewe wamekuja na wataalamu wao, tutapitia kipengele kimoja baada ya kingine na tunaamini tutafika mwisho na kama tulivyo waambia wenzetu wa EU tunaona faida ya kufanya biashara na wao kwa maslahi ya pande zote mbili,” amesema Prof. Kahyarara  

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti amesema majadiliano hayo yanalenga kuangalia vipengele vya mkataba ambavyo Tanzania ilionesha mashaka  katika kikao kilichopita ili kuvipatia ufumbuzi na kusonga mbele kwa pamoja hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania sasa inatoa kipaumbele katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

“Itakumbukwa kuwa Tanzania inatekeleza diplomasia ya uchumi na wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya wanania ya kuja kuwekeza Tanzania na Afrika Mashariki, hivyo tukikamilisha majadiliano haya itakuwa ni jambo lenye maslahi kwa pande zote,” Amesema Balozi Fanti.  

Kikao cha leo kinatokana na mazungumzo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyafanya alipokuwa katika ziara ya kikazi nchini Ubelgiji ambapo alikutana na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Bw. Charles Michael mwezi Februari 2022.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti akiongea na washiriki wa kikao (hawapo pichani), kulia ni Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara katika kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti akiongea na washiriki wa kikao, kulia ni Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara katika kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam


Kikao kikiendelea 

Washiriki kutoka Tanzania na Umoja wa Ulaya wakiwa katika picha ya pamoja


Friday, March 18, 2022

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA DKT. STERGOMENA L. TAX AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA KAWAIDA WA SADC UNAOFANYIKA LILOLONGWE, MALAWI

   Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) akiongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa kawaida wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Lilongwe Malawi (Machi 18 – 19,2022). Kushoto kwa Dkt. Tax ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor (Mb) Mbarouk,akifuatiwa na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) na Mipango na Naibu Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb)


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) pamoja na ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alioongozana nao wakifuatilia Mkutano wa kawaida wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaoendelea Lilongwe,Malawi

    Sehemu ya Mawaziri wa Mawaziri wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa katika mkutano.


Mawaziri wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC )wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa kawaida wa Mawaziri wa SADC uofanyika Lilongwe Malawi Machi 18 – 19,2022