Friday, July 12, 2024

WAZIRI MAKAMBA AZUNGUMZA NA KATIBU MTENDAJI WA SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba leo tarehe 12 Julai 2024 jijini Lusaka, Zamba amekutana kwa mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Elias Mpedi Magosi.

 

Katika mazungumzo yao ambayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC uliomalizika leo jijini hapa, Mhe. Makamba amempongeza Mhe. Magosi kwa kazi kubwa inayofanywa na Sekretarieti hiyo katika kusimamia utekelezaji wa mipango, itifaki, na mikataba mbalimbali iliyopitishwa au kuridhiwa na nchi wanachama wa SADC.

 

Kadhalika viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Sekretarieti hiyo ikiwemo masuala ya uratibu na usimamizi wa Kituo cha SADC cha Kupambana na Ugaidi chenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam na matayarisho yanayoendelea wakati Tanzania ikijiandaa kuchukua Unyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama kuanzia mwezi Agosti 2024.

 

Akizungumza kuhusu usimamizi wa Kituo hicho, Mhe. Magosi amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Tanzania ya kukisimamia kikamilifu Kituo hicho tangu kianzishwe mwezi Februari 2022 na  kwamba kwa mujibu wa makubaliano, Sekretarieti ya SADC inajiandaa kupokea jukumu hilo la kuendelea kukisimamia hapo mwezi Oktoba 2024 ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa kwa nchi wanachama na kanda kwa ujumla.

 

Viongozi wengine kutoka Tanzania walioambatana na Mhe. Makamba kwenye kikao hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba  akizungumza na  Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Elias Mpedi Magosi. Mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 12 Julai 2024 jijini Lusaka, Zambia pembezoni mwa Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC. Kulia kwa Mhe. Makamba ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Elias Mpedi Magosi akizungumza na Mhe. Makamba (hayupo pichani)
Mkutano ukiendelea

Mhe. Makamba katika mazungumzo na Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Magosi (hayupo pichani) Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Sillo na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Balozi Dkt. Samweli Shelukindo

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Sillo kulia akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule wakishiriki mazungumzo kati ya Mhe. Makamba na Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Magosi

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akishiriki mazungumzo
Mhe. Makamba akiwa na Mhe. Magosi baada ya mazungumzo kati yao kumalizika

Mhe. Makamba akifafanua jambo kwa Mhe. Magosi

 

Thursday, July 11, 2024

WAZIRI MAKAMBA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 26 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai, 2024.

 

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika kuanzia tarehe 08 hadi 09 Julai 2024, pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa ikiwemo Mapitio ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 25 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda; na Uimarishaji wa Demokrasia katika Kanda.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe amewakaribisha nchini Zambia wajumbe wa mkutano huo ambao agenda yake kuu ni kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi wanachama wa SADC na kuandaa mikakati ya pamoja ya kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana kwenye maeneo ya changamoto.

 

Aidha, akizungumzia hali ya amani na usalama kwenye maeneo yenye  changamoto hususan eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lesotho na eneo la Kaskazini mwa Msumbiji, Mhe. Haimbe amesema hali sasa inatia moyo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuendelea kujitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha amani, usalama na utulivu wa kudumu vinapatikana  kwenye maeneo hayo ili kuwa na maendeleo endelevu ya kiuchumi katika kanda.

 

Kadhalika amezipongeza misheni za ulinzi wa amani za SADC iliyopo DRC na ile iliyopo Kaskazini mwa Msumbiji kwa kujitoa kikamilifu katika kuhakikisha amani na usalama kwenye maeneo hayo vinarejea mbali na changamoto kadhaa wanazopitia.

 

Kuhusu misheni ya ulinzi wa amani ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambayo inamaliza muda wake wa operesheni mwezi Julai 2024, Mhe. Haimbe ameipongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika ya kupambana na vitendo vya ugaidi na kurejesha hali ya amani kwa wananchi wa Jimbo la Cabo Delgado lililopo Kaskazini mwa Msumbiji.

 

“Napongeza misheni ya SAMIM kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika. Japo wanamaliza operesheni huko Kaskazini mwa Msumbiji, bado mapambano dhidi ya ugaidi na uhalifu wa kuvuka mipaka katika Nchi zote wanachama wa SADC yataendelea. Hivyo naziomba nchi zote wanachana kuendelea kushirikiana na kuandaa mikakati ya pamoja kukabiliana na vitisho hivi” alisisitiza Mhe. Haimbe.

 

Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi amesema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na kiuchumi ili hatimaye kuwa na Kanda tulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu.

 

Pia aliongeza kusema bado jitihada za pamoja zinahitajika katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda ikiwemo ugaidi, vitendo vya uhalifu wa kuvuka mipaka na rushwa. Kadhalika, Mhe. Makosi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri anayemaliza muda wake Mhe. Haimbe kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chote na kumkaribisha na kumwahidi ushirikiano Mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. January Makamba.

 

Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kukuza na kulinda amani na usalama katika kanda ya SADC. Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2024.

 

Mbali na Mhe. Makamba, ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Daniel Sillo, Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe,  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda,  Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na Usalama.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo (kulia) akiwa na  Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe wakishiriki  Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kushoto) kwa pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda (katikati) na Katibu Mkuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Mnyepe (kulia) wakishiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi  rasmi Mkutano huo iliyofanyika tarehe 11 Julai 2024  katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mulungushi uliopo jijini Lusaka, Zambia
Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi naye akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Shelukindo akiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri. Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri
Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jenerali Mathew Mkingule akishiriki Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa SADC

Meza kuu

Mkutano ukiendelea

Mhe. Waziri Makamba akizungumza na viongozi mbalimbali kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC

Picha ya pamoja