Wednesday, January 22, 2025

WAZIRI KOMBO AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA IFAD KANDA YA MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (IFAD), Bi. Sara Mbago-Bhunu.

 

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dodoma, Januari 22, 2025, viongozi hao pamoja na mambo mengine walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Mfuko huo ili kuwawezesha wananchi wa Tanzania hususan wale waliopo vijijini kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini kupitia program zinazotekelezwa na mfuko huo hapa nchini zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji, ambapo pia Bi. Mbago-Bhunu alitumia fursa hiyo kumtambulisha Mkurugenzi na Mwakilishi mpya wa Mfuko huo hapa nchini, Bw. Sakphouseth Meng.

 

Kwa upande wake,  Mhe. Waziri Kombo ameupongeza Mfuko huo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika program za kuendeleza sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji  hapa nchini hususan kwa maeneo ya vijijini na kuwaomba kukamilisha program ambazo tayari zinaendelea nchini chini ya ufadhili wa mfuko huo ikiwemo ile ya ununuzi wa Boti za Uvuvi kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Amesema, lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi imara wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo IFAD katika kukuza na kuimarisha sekta za kilimo, uchumi wa buluu na ufugaji ili kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo endelevu.

 

Naye, Bi. Mbago-Bhunu alimshukuru Mhe. Balozi Kombo kwa ushirikiano ambao Mfuko huo umeendelea kuupata kutoka Serikalini na kwamba Mfuko huo utaendelea kutekeleza majukumu yake hapa nchini ikiwemo kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi hususan waliopo kwenye maeneo ya vijijini kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi na tija zaidi kwa maendeleo endelevu.

 

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi pamoja na wajumbe wengine walioambata Bi. Mbago-Bhunu.

 

Mfuko wa IFAD unatekeleza miradi mbalimbali hapa nchini kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia miongozo mbalimbali ikiwemo Program ya Nchi kuhusu Fursa za Kimkakati ya mwaka 2022 hadi 2027 (COSOP 2022-2027) unaokwenda sambamba na  Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Ushirikiano katika Maendeleo Endelevu  na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Tanzania.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (IFAD), Bi. Sara Mbago-Bhunu alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma hivi karibuni. Pamoja na mambo mengine viongozi hao walijadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Mfuko huo katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Pia Bi. Mbago-Bhunu alitumia nafasi hiyo kumtambulisha Mkurugenzi na Mwakilishi mpya wa Mfuko huo hapa nchini, Bw. Sakphouseth Meng (wa pili kulia) ambaye aliongozana nae kwenye ziara hiyo. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (IFAD), Bi. Sara Mbago-Bhunu akizungumza wakati wa kikao kati yake na Mhe. Balozi Kombo ambaye hayupo pichani
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Kulia) akiwa na Bi. Mbago-Bhunu (kushoto) na Bw. Meng wakati wa kikao kati ya ujumbe huo kutoka IFAD na Mhe. Waziri Kombo ambaye hayupo pichani
Mkurugenzi na Mwakilishi mpya wa Mfuko huo hapa nchini, Bw. Sakphouseth Mengakizungumza wakati wa kikao hicho
Mhe. Balozi Kombo akiwa katika picha ya pamoja na Bi. Mbago-Bhunu na Bw. Meng mara baada ya mazungumzo yao
Mhe. Waziri Kombo akiagana na Bi. Mbago-Bhunu mara baada ya mazungumzo yao
Picha ya pamoja







 

Monday, January 20, 2025

Uhusiano baina ya Tanzania-Czech kung’ara






Uhusiano wa kiuchumi baina ya mataifa umeelezwa kuwa ndio uhusiano imara na bora zaidi ukilinganisha na nyanja nyingine za uhusiano duniani kwa sasa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Czech, Mhe. Jan Lipavský wakati wanazungumza na waandishi wa habari jijini Prague Januari 17, 2025.

Waziri Kombo amesema kuwa Tanzania na Czech zina uhusiano mzuri na imara wa kidiplomasia ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo tokea miaka ya 60 na kwamba jukumu walilo nalo ni kuhakikisha kuwa uhusiano huo unaimarishwa na kuboreshwa ili uendane na mahitaji ya sasa ya kiuchumi. 

Waziri Kombo ambaye alikuwa nchini Czech kwa ziara ya kikazi ya siku tatu amesema ziara yake nchini humo ambayo ni ya kwanza kwa Mwaka 2025 inaonesha dhamira ya dhati kwa Czech na kutoa ujumbe mzito kwa nchi hiyo kupanua wigo wa ushirikiano na Tanzania katika maeneo ya kimkakati kama vile uwekezaji, biashara, utalii, miundombinu, afya na elimu.

Waziri Kombo alieleza kuwa jukumu kubwa la Serikali zote duniani hivi sasa ni kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi na zile zinazosimamia masuala ya uwekezaji ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, hivyo ziara yake inalenga sio tu kushawishi kampuni zenye nguvu nchini Czech kwenda kuwekeza Tanzania bali pia kuharakisha ukamilishwaji wa makubaliano ambayo kwa namna moja au nyingine yanapunguza kasi ya uwekezaji na biashara baina ya mataifa hayo.

Kufuatia azma hiyo, Waziri Kombo na mwenyeji wake wamekubaliana kuharakisha uwekaji saini wa Mkataba wa Anga ili kuruhusu safari za ndege za moja kwa moja baina ya mataifa hayo kwa lengo la kupanua sekta ya utalii ambayo ni sekta muhimu kwa mapato ya Tanzania. Idadi ya watalii kutoka Czech imekuwa ikiongezeka kila mwaka huku nchi hiyo ikifanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya utalii visiwani Zanzibar.

Mkataba mwngine muhimu katika kuchagiza biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo ni Mkataba wa Kuepuka Utozaji wa Kodi Mara mbili ambapo pande zote zilikiri kuwa mkataba huo umefikia hatua nzuri na masuala yaliyosalia yatakamilushwa ili uweze kusainiwa mapema mwaka huu.

Waziri Kombo amesema Tanzania ni nchi yenye amani, utulivu na rasilimali za kutosha na kumuomba Waziri mwenzake awashawishi wafanyabiashara wengi wa Czech kuja kuwekeza Tanzania kama alivyo fanya mfanyabiashara mwenzao wa kampuni ya Airplanes Africa Limited kwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza ndege aina ya skyleader - 600 chenye makao makuu mkoani Morogoro. 

Amesema Tanzania inajivunia uwekezaji huo ambao utakuwa kichocheo kikubwa kwa sekta ya utalii ya Tanzania kwa sababu ndege hizo zina uwezo wa kutua kwenye mazingira magumu yaliyopo katika mbuga na hifadhi za taifa.

Eneo lingine ambalo Waziri Kombo ameiomba Czech kushirikiana na Tanzania ni sekta ya uchukuzi hasa katika ujenzi na uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya SGR ambapo Czech imepiga hatua kubwa kwenye sekta hiyo. Amesema ujenzi wa SGR unaendelea nchini kwa lengo la kuunganisha Tanzania na nchi jirani, na kuiomba Czech ishiriki moja kwa moja tofauti na sasa inauza vifaa kupitia kampuni nyingine iliyopewa zabuni.


Ziara hii ni moja ya mikakati ya Waziri Kombo ya kutembelea nchi ambazo zinaonekana ni wadau muhimu katika utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi na kupitia ziara hiyo alitembelea kampuni mbalimbali na kuzungumza na wafanyabiashara wakubwa ambao wamevutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania.

Tuesday, January 14, 2025

TANZANIA NA JAPAN ZAJIDHATITI KUSAIDIA WAKULIMA NCHINI



Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa wakionesha mkataba wa shilling bilioni 377 uliosaniwa kwa lengo la kusaidia wakulima kupitia mikopo

· Mkataba wa shilingi bilioni 377 wasainiwa kusaidia wakulima

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Japan zimetia saini mkataba wa shilingi bilioni 377 kugharamia utelelezaji wa mradi wa Kilimo na Maendeleo Vijijini (Agriculture and Rural Development Two Step Loan) ambao umekusudiwa kuwanufaisha moja kwa moja wakulima kupitia mikopo midogo midogo. 

Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa huku ikishuhudiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Hiyasuki Fuji kwenye hafla iliyofanyika Januari 14, 2025 katika Ofisi ndogo ya Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam. 

Kiasi hicho cha fedha kilichotolewa kwa Tanzania kwa mfumo wa mkopo wa masharti nafuu na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la maendeleo (JICA) kinalenga kuwezesha vyama, vikundi vya wakulima na mkulima mmoja mmoja kupata mikopo ya muda mfupi, wa kati na mrefu kwa mazao ya ngano, mahindi, mpunga, alizeti na kilimo cha bustani. 

Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini wa mkata huo Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameeleza kuwa, kupatikana kwa fedha hizo kunatokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Japan. 

"Katika kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuifungua nchi kwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na uchumi, leo tunaona manufaa yake. Kiasi hiki cha fedha kitaelekezwa moja kwa moja kwa wakulima ili kikaongeze kasi ya mageuzi katika sekta ya kilimo itakayohusisha kuongeza uzalishaji, ubora na thamani ya mazao". Alieleza Waziri Dkt. Nchemba

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Fuji ameeleza kuwa kiasi hicho cha fedha za mkopo wa masharti nafuu kimetolewa kuunga mkono dhamira na juhudi za Serikali ya Tanzania ya kuwakomboa wakulima kiuchumi kupitia kazi zao. 

“Tunatambua kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya kilimo. Japan tunaamini kiasi hiki cha fedha kitaenda kuongeza kasi ya kuiboresha sekta ya kilimo ili iweze kuwaongezea kipato wakulima na kuwatoa katika umaskini". Alisema Wazir Fuji.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi ambaye alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo katika hafla hiyo, alieleza kuhusu namna utekelezaji wa diplomasia ya uchumi chini ya uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan unavyovutia wadau wa maendeleo kusaidia katika sekta mbalimbali nchini. 


“Mambo haya mazuri tunayoyashuhudia leo ni matokeo ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuifungua nchi kwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Jumuiya ya Kimataifa, ni wajibu wetu kuendelea kumuunga mkono Rais wetu kwenye utekelezaji wa diplomasia ili aendelee kuleta maendeleo nchini”. Alisema Mhe.Chumi


Katika hatua nyingine kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Japan limefanyika tarehe 14 Januari 2025 jijini Dar es Salaam ambapo limefunguliwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud S. Kigahe ambaye pia aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kongamano hilo.


Kongamano hilo lililenga kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara wa Japan na Tanzania kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha ubia, ili kuimarisha na kukuza biashara na uwekezaji hapa nchini kwa manufaa ya pande zote mbili. 
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa wakitia saini mkataba wa shilingi bilioni 377 unaolenga kusaidia wakulima kupitia mikopo katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam




Kongamano la biashara na uwekezaji likiendelea jijini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akihutubia kwenye hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililofanyika jijini Dar es Salaam Januari 14, 2025
 Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda akihutubia kwenye hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Japan lililofanyika jijini Dar es Salaam Januari 14, 2025
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Bi.Felista Rugambwa akifuatilia Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Japan lililofanyika jijini Dar es Salaam Januari 14, 2025 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi na Balozi wa Tanzania nchini Japan Mhe. Baraka Luvanda wakifurahia jambo kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Japan lililofanyika jijini Dar es Salaam Januari 14, 2025 
Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Japan likiendelea jijini Dar es Salaam Januari 14, 2025 

Picha ya pamoja

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo wakati wa hafla ya kutia saini mkataba wa shilingi bilioni 377 unaolenga kusaidia wakulima kupitia mikopo katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akihutubia mara baada ya kusaini mkataba wa shilling bilioni 377 unaolenga kuwasaidia wakulima kupitia mikopo
Picha ya pamoja