Wednesday, January 22, 2025

WAZIRI KOMBO AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA IFAD KANDA YA MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (IFAD), Bi. Sara Mbago-Bhunu.

 

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dodoma, Januari 22, 2025, viongozi hao pamoja na mambo mengine walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Mfuko huo ili kuwawezesha wananchi wa Tanzania hususan wale waliopo vijijini kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini kupitia program zinazotekelezwa na mfuko huo hapa nchini zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji, ambapo pia Bi. Mbago-Bhunu alitumia fursa hiyo kumtambulisha Mkurugenzi na Mwakilishi mpya wa Mfuko huo hapa nchini, Bw. Sakphouseth Meng.

 

Kwa upande wake,  Mhe. Waziri Kombo ameupongeza Mfuko huo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika program za kuendeleza sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji  hapa nchini hususan kwa maeneo ya vijijini na kuwaomba kukamilisha program ambazo tayari zinaendelea nchini chini ya ufadhili wa mfuko huo ikiwemo ile ya ununuzi wa Boti za Uvuvi kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Amesema, lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi imara wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo IFAD katika kukuza na kuimarisha sekta za kilimo, uchumi wa buluu na ufugaji ili kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo endelevu.

 

Naye, Bi. Mbago-Bhunu alimshukuru Mhe. Balozi Kombo kwa ushirikiano ambao Mfuko huo umeendelea kuupata kutoka Serikalini na kwamba Mfuko huo utaendelea kutekeleza majukumu yake hapa nchini ikiwemo kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi hususan waliopo kwenye maeneo ya vijijini kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi na tija zaidi kwa maendeleo endelevu.

 

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi pamoja na wajumbe wengine walioambata Bi. Mbago-Bhunu.

 

Mfuko wa IFAD unatekeleza miradi mbalimbali hapa nchini kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia miongozo mbalimbali ikiwemo Program ya Nchi kuhusu Fursa za Kimkakati ya mwaka 2022 hadi 2027 (COSOP 2022-2027) unaokwenda sambamba na  Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Ushirikiano katika Maendeleo Endelevu  na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Tanzania.



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (IFAD), Bi. Sara Mbago-Bhunu alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma hivi karibuni. Pamoja na mambo mengine viongozi hao walijadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Mfuko huo katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Pia Bi. Mbago-Bhunu alitumia nafasi hiyo kumtambulisha Mkurugenzi na Mwakilishi mpya wa Mfuko huo hapa nchini, Bw. Sakphouseth Meng (wa pili kulia) ambaye aliongozana nae kwenye ziara hiyo. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (IFAD), Bi. Sara Mbago-Bhunu akizungumza wakati wa kikao kati yake na Mhe. Balozi Kombo ambaye hayupo pichani
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Kulia) akiwa na Bi. Mbago-Bhunu (kushoto) na Bw. Meng wakati wa kikao kati ya ujumbe huo kutoka IFAD na Mhe. Waziri Kombo ambaye hayupo pichani
Mkurugenzi na Mwakilishi mpya wa Mfuko huo hapa nchini, Bw. Sakphouseth Mengakizungumza wakati wa kikao hicho
Mhe. Balozi Kombo akiwa katika picha ya pamoja na Bi. Mbago-Bhunu na Bw. Meng mara baada ya mazungumzo yao
Mhe. Waziri Kombo akiagana na Bi. Mbago-Bhunu mara baada ya mazungumzo yao
Picha ya pamoja







 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.