Saturday, March 8, 2025

WANAWAKE DODOMA WAUNGANA KUSHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE KIMATAIFA





Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Makao Makuu Dodoma pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, wameungana na wanawake kutoka ofisi mbalimbali za umma na binafsi jijini Dodoma kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake duniani kwa mwaka 2025.

 Maadhimisho hayo, ambayo hufanyika kila Machi 8, yameandaliwa kwa lengo la kutambua mchango wa wanawake katika jamii na kuhimiza usawa wa kijinsia.

Maadhimisho hayo kimkoa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, yakiwa na kaulimbiu isemayo: "Wanawake na Wasichana Tuimarishe Haki, Usawa na Uwekezaji."

Kaulimbiu hiyo inalenga kusherehekea mafanikio ya wanawake, kujadili changamoto wanazokabiliana nazo, na kutafuta njia za kuimarisha haki, usawa, na uwekezaji kwa maendeleo endelevu.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mheshimiwa Alhaj Jabir Shekimweri, ambaye alisisitiza umuhimu wa haki za wanawake na ushiriki wao katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha, alieleza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika elimu, uchumi, na uongozi.

Mheshimiwa Shekimweri alitoa wito kwa jamii kuendelea kupinga ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi stahiki kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa taifa. “Tukiwekeza kwa wanawake na wasichana, tunaiwekeza jamii katika maendeleo endelevu. Haki na usawa si jambo la hiari bali ni msingi wa maendeleo ya taifa letu,” alisema Shekimweri.

Pia, amewahimiza wadau kushirikiana kuwawezesha wanawake kiuchumi na kielimu na kusisitiza kuwa haki inapaswa kwenda sambamba na wajibu, akiwataka wanawake na wasichana kuwa mstari wa mbele kutumia fursa zinazotolewa kwa nidhamu, bidii, na maadili mema.

Aliongeza kuwa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ni muhimu katika kudumisha maadili ya Kitanzania, huku akihimiza jamii kutumia teknolojia kwa maendeleo chanya.

Katika maadhimisho hayo, wanawake kutoka sekta mbalimbali walishiriki uzoefu wao na kutoa hamasa kwa wenzao juu ya njia bora za kufanikisha malengo yao. Pia, vikundi vya ujasiriamali vilipata nafasi ya kuonyesha bidhaa zao, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uwekezaji kwa wanawake na kuwawezesha kiuchumi.

Maadhimisho hayo yaliambatana na michezo mbalimbali, ambapo washindi walitunukiwa medali na vikombe kama ishara ya kutambua juhudi zao na mchango wao katika jamii. Kaulimbiu ya mwaka huu inaendelea kuwa mwangaza kwa wanawake na wasichana kote nchini, ikiwahimiza kuimarisha haki, usawa, na uwekezaji kwa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu ya taifa.

 

Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mheshimiwa Alhaj Jabir Shekimweri, akitoa hotuba kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika kimkoa, jijini Dodoma, katika viwanja vya Chinangali Park.
 




















No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.