Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Maendeleo na Diaspora, Mhe. Neale Richmond
Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Maendeleo na Diaspora, Mhe. Neale Richmond, ametembelea Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Ireland, hususan katika sekta ya usafirishaji wa bidhaa kupitia bandari hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Richmond alieleza nia ya Ireland ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na Tanzania kwa kuhakikisha mifumo ya usafirishaji wa bidhaa inaboreshwa ili kuongeza kasi ya biashara kati ya mataifa hayo mawili.
Katika ziara hiyo, Mhe. Richmond alipata fursa ya kutembelea miundombinu ya bandari na kujionea shughuli za upokeaji na usafirishaji wa mizigo, pamoja na kujadiliana na wadau mbalimbali juu ya fursa za uwekezaji.
Aidha, Waziri Richmond alikutana na kuzungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wawakilishi wa sekta binafsi, na uongozi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), ambalo hutumia bandari hiyo kuhifadhi na kusafirisha chakula kwenda katika maeneo mbalimbali.
Mazungumzo hayo yalijikita katika uimarishaji wa njia bora za usafirishaji wa bidhaa za kilimo na chakula, ili kuongeza tija kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa pande zote mbili.
Katika ziara hiyo Mhe. Richmond aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Mbelwa Kairuki, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika- Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme.
Ziara hii inaonesha nafasi muhimu ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika Ukanda wa Afrika Mashariki na inatarajiwa kusaidia kuvutia wawekezaji zaidi kutoka Ireland, huku serikali ikiendelea kuweka mazingira rafiki kwa biashara na uwekezaji.
Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Maendeleo na Diaspora, Mhe. Neale Richmond (kushoto) pamoja na Balozi wa Ireland nchini Mhe. Nicola Brennan.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.