Friday, March 14, 2025

WAZIRI WA IRELAND ATEMBELEA KIWANDA CHA KERRY GROUP





Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Maendeleo na Diaspora, Mhe. Neale Richmond





Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Maendeleo na Diaspora, Mhe. Neale Richmond, ametembelea Kiwanda cha Kerry Group kilichopo jijini Dar es Salaam


Kampuni ya Kitaifa ya Kerry Group yenye makao yake nchini Ireland, imewekeza katika kiwanda hicho kama sehemu ya mkakati wake wa kupanua shughuli zake barani Afrika, hususani katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Kiwanda cha Kerry Group kinajihusisha na uzalishaji wa viambato vya ladha kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi na hivyo kuchangia ukuaji wa sekta ya uzalishaji wa chakula nchini.

Kiwanda hicho mbali ya kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini kimetoa ajira kwa Watanzania, kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa gharama nafuu, ubunifu wa bidhaa na ushirikiano wa kibiashara na wadau wa ndani.

Akiwa Kiwanda hapo Mhe. Neale Richmond alibainisha kuwa Ireland ina nia ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi na Tanzania, huku akieleza kuwa uwekezaji wa Kerry Group ni kielelezo cha Nia hiyo na ni sehemu ya mafanikio yatokanayo na ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa haya mawili.

Aidha, Waziri Richmond alieleza kuwa Kerry Group imejikita kuleta maendeleo endelevu kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira, jambo linaloendana na sera za kimataifa za uzalishaji wenye tija na rafiki kwa mazingira.

Alisema Ireland itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha sekta ya viwanda inakua kwa kasi na kuleta manufaa kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza ambaye pia anawakilisha Ireland Mhe. Mbelwa Kairuki, aliikipongeza Kiwanda cha Kerry Group kwa mchango wake katika sekta ya viwanda nchini na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kiwanda hicho.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuvutia wawekezaji zaidi kutoka Ireland na mataifa mengine.

Waziri Richmond yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku Tatu kuanzia tarehe 14-16 Machi, 2025.
 
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Maendeleo na Diaspora, Mhe. Neale Richmond (kulia) pamoja na Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza ambaye pia anaiwakilisha Ireland, Mhe.Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto)
 
 
 


 Balozi wa Tanzania nchini Ireland ambaye pia anaiwakilisha Ireland, Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto) pamoja na Mkurugenzi idara ya Ulaya na Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (kulia)
 

 Balozi wa Ireland nchini Mhe. Nicola Brennan 
 


 


 





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.