Tuesday, March 8, 2016

Waziri Mahiga akutana na Waziri wa Uingereza wa masuala ya Afrika


Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akimkaribisha Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. James Duddridge, mara baada ya kuwasili katika ofisi za Wizara ambapo waliweza kufanya mazungumzo. 
Mhe. Waziri Mahiga akiendelea na Ukaribisho kwa Mhe. Balozi Diana Melrose ambaye aliambatana na Mhe. Waziri James Duddridge katika mazungumzo hayo.
Mhe. Waziri Mahiga akiwa katika mazungumzo na Mhe. Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika ambapo katika mazungumzo yao waliweza kujadili masuala ya maendeleo hususan katika sekta ya uwekezaji na biashara pamoja na kuangalia namna Serikali ya Uingereza inavyoweza kushirikiana na Tanzania katika kukuza uchumi na kuimarisha viwanda.
Mhe. Balozi Diana Melrose pamoja na afisa aliyeambatana naye wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Waziri Mahiga na Mhe. Waziri James Duddridge.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Joseph Sokoine wa kwanza kushoto, akiwa pamoja na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Mona Mahecha na Msaidizi wa Waziri Bw. Thobias Makoba kulia wakifuatilia mazungumzo pia.
Mhe. Waziri Mahiga akiagana na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika mara baada ya kumaliza mazungumzo.

Balozi Mahiga ala kiapo cha utii katika Bunge la Afrika Mashariki

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akila kiapo mbele ya Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, akiwa kama Waziri anayehusika na Shughuli za Ushirikiano wa Afrika Masahiriki kutoka Tanzania. Tukio hilo la kuapishwa kwa Waziri Mahiga limeshuhudiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndungai (hawapo pichani), hafla hiyo imefanyika leo mchana jijini Dar es Salaam. 
Sehemu ya Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wakishuhudia Balozi Mahiga akila kiapo (hayupo pichani).
Sehemu ya watumishi kutoka Serikalini wakifuatilia tukio hilo la uapisho. Mstari wa nbele katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Habari na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga.
Sehemu nyingine ya viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango, na kulia ni Katibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. Adam Issara.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.) wa kwanza kushoto, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. Daniel Kidega    na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndungai kwa pamoja wakiimba wimbo wa Afrika Mashariki kabla ya Kuapishwa kwa Waziri Mahiga (hayupo pichani). 
Wabungu wa Bunge la Afrika Mashariki nao wakiimba Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Shughuli za Kibunge zikiendelea  mara baada ya kumalizika kwa tukio la Uapisho wa Balozi Mahiga
Picha na Reginald Philip


Waziri Mahiga afungua Mkutano wa Pili wa Vyama vya Kijamii vya ICGLR

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Masahriki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga (Mb.) akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la vyama visivyo vya Kiserikali (Vyama vya Kijamii), kutoka Nchi za Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika mapema leo katika Hoteli ya Ramada Jijini Dar es Salaam. Katika ufunguzi huo Waziri Mahiga aliwashukuru wajumbe kwa kuchagua kuufanyia mkutano wao hapa nchini vilevile kuwa na ushirikiano katika masuala ya kijamii ambayo yatapelekea kuondoa machafuko ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi wanachama
Sehemu ya wajumbe wakimsikiliza kwa makini Balozi Mahiga (hayupo pichani) alipokuwa akifungua Mkutano huo.
Sehemu nyingine ya wajumbe kutoka Sudan Kusini nao wakifuatilia kwa makini ufunguzi huo.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UN eneo la Maziwa Makuu Balozi Said Djinnit naye alipata fursa ya kuzungumza katika ufunguzi wa mkutano huo.
Sehemu ya Watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa nao wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na Mhe. Waziri Mahiga (hayupo pichani), wa kwanza kulia ni Katibu wa Waziri Mahiga, Bw. Adolf Mchemwa, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga (wa kwanza kushoto) na katikati ni Afisa Mambo ya Nje, Bw. Ally Ubwa
Mwenyekiti wa Kikanda wa Jukwaa la Vyama visivyo vya Kiserikalikutoka nchi za Maziwa Makuu, Bw. Joseph Butiku naye akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo 
Mwakilishi wa Umoja wa Afrika eneo la Maziwa Makuu Bi. Altine Traore naye akizungumza
Meza kuu wakimsikilza Bi. Traore (hayupo pichani) alipo kuwa akitoa hotuba yake. 
Waziri Mahiga akizungumza na Waandishi wa Habari.
Picha ya Pamoja.

Picha na Reginald Philip

Waziri Mahiga ashiriki ibada ya kumuaga Marehemu Balozi Rwegasira

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga akitoa pole kwa niaba ya Wizara kwa familia ya aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Marehemu Balozi Joseph Rwegasira wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro Jijini Dar es Salaam.Balozi Mahiga alimwelezea Marehemu Balozi Rwegasira kuwa alikuwa kiongozi hodari wa kupigiwa mfano kutokana na moyo wake wa kufanya kazi kwa bidii na kujituma.
Ndugu na jamaa waliohudhuria ibada hiyo wakimsikiliza kwa makini Waziri Mahiga (hayupo pichani).
Sehemu nyingine ya watu waliohudhuria ibada hiyo
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba naye alipata fursa ya kutoa neno la pole kwa familia ya Marehemu Balozi Rwegasira.
Mmoja wa wanafamilia ya Balozi Rwegasira akisoma utaratibu wa kutoa heshima za mwisho za kuuaga mwili wa Balozi Rwegasira
Sehemu ya Viongozi wa Serikali na Vyama vya Kisiasa wakisikiliza utaratibu wa kutoa heshima za mwisho kwa  mwili wa Balozi Rwegasira.
Waziri Mahiga akimpa mkono wa pole Mama Rwegasira
Waziri Mahiga pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Aziz Mlima wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Bolozi Rwegasira
Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wakitoa mkono wa pole kwa familia ya Balozi Rwegasira 

Monday, March 7, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU WASIFU WA
KATIBU MKUU KIONGOZI MTEULE BALOZI MHANDISI JOHN KIJAZI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amemteua Balozi Mhandisi John William Kijazi (Pichani) kuwa Katibu Mkuu Kiongozi tarehe 6 Machi 2016, akichukua nafasi ya Balozi Ombeni Sefue. 

Kabla ya uteuzi huo, Balozi Mhandisi Kijazi alikuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal mwenye makazi yake jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi. Vilevile, hadi uteuzi wake, Balozi Kijazi amekuwa Mkuu wa Mabalozi wa Afrika nchini India ambaye amekuwa mtetezi mkuu wa wanafunzi wenye asili ya Kiafrika nchini India.

Kabla ya kuwa balozi, Mhandisi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India. 

Kati ya mwaka 1996 hadi 2002, Mhandisi Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya Wizara hiyo hiyo. 

Balozi Mhandisi Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.
Balozi Mhandisi John Kijazi amemuoa Fransiscar Kijazi na pamoja wamejaliwa watoto watatu, David, Emmanuel na Richard Kijazi. 

Balozi Mhandisi John Kijazi ataapishwa leo tarehe 7 Machi 2016 na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu jijini Dar es salaam. 

-MWISHO-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa,
07 Machi 2016


Sunday, March 6, 2016

Rais wa Vietnam kufanya ziara ya kwanza ya kitaifa nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga (Mb.) (kulia), akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ziara ya kitaifa ya siku 4 ya Rais wa Vietnam nchini, Mhe.Truong Tan Seng kuanzia tarehe 08 hadi 11 Machi, 2016. Ziara hiyo itakuwa ni ziara ya kwanza ya kuja Tanzania pia Afrika. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga naye akisikiliza kwa makini mazungumzo ya Waziri na Waandishi wa Habari.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza kwa makini Balozi Mahiga (hayupo pichani).
Bi. Mindi Kasiga naye akitolea ufafanuzi ratiba nzima ya ziara ya Rais huyo wa Vietnam
Sehemu nyingine ya waandishi wa Habari wakinukuu baadhi ya pointi wakati mkutano ukiendelea
Kikao na waandishi wa Habari kikiendelea.

Picha na Reginald Philip

==================================================



Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang atakuwa Rais wa kwanza kufanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Rais Sang atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere siku ya Jumanne tarehe 08 Machi 2016 saa mbili usiku na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambapo mapokezi rasmi yatafanywa siku ya pili na mwenyeji wake, Rais Dkt. Magufuli katika Viwanja vya Ikulu.

Akiongea na Waandishi wa Habari Ofisini kwake leo, Waziri Mahiga alieleza kuwa Rais Sang atafutana na mke wake, Mama Mai Thi, Mawaziri watano na Wafanyabiashara 51 katika ziara hiyo. Dkt. Mahiga alieleza kuwa Serikali inaupa uzito wa pekee ugeni huo kwa sababu ni ziara ya kwanza ya kitaifa katika Awamu ya Tano kufanywa na Mkuu wa Nchi. “Wakuu wa Nchi kadhaa walishakuja hapa nchini lakini kwa ziara za kikazi, sio za kiserikali, hivyo Vietnam imetupa heshima kubwa sana”.  Waziri Mahiga alisema.

Rais Sang ni mara ya kwanza kufanya ziara katika Bara la Afrika na Tanzania ambapo pia atazuru nchi ya Msumbiji baada ya kuondoka hapa nchini tarehe 11 Machi 2016.

Dkt. Mahiga aliwambia Waandishi wa Habari kuwa Tanzania ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Vietnam namna ilivyopiga hatua kubwa ya maendeleo katika kipindi kifupi, licha ya kuendesha vita kubwa ya mapambano ya kupigania uhuru dhidi ya Ufaransa na baadaye dhidi ya Marekani. Alisema nchi hiyo imepiga hatua katika sekta za viwanda, kilimo, mawasiliano na uvuvi.  Kwa upande wa kilimo, nchi hiyo ni ya kwanza kwa kuuza kahawa aina ya robusta na korosho duniani ingawa mbegu za mazao hayo zimechukuliwa Tanzania. 

Aidha, Vietnam ni maarufu duniani kwa kuuza samaki aina ya sato ambao walichukuliwa kutoka Ziwa Victoria.

Waziri wa Mambo ya Nje alieleza kuwa ili Tanzania nayo ifike ilipo Vietnam ni lazima ifuate mambo matatu ambayo Vietnam inayazingatia. Mambo hayo ni kufanya kazi kwa bidii katika mazingira ya aina zote, utekelezaji wa maamuzi wanayofanya na kuwekeza katika mafunzo ya ufundi, miundombinu kama ya umeme, barabara, reli, bandari na mabemki kwa ajili ya mitaji na huduma nyingine za kifedha.

Katika ziara hiyo, Rais wa Vietnam pamoja na mambo mengine atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake; Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein; Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai; Kuongea na wafanyabiashara na kutembelea eneo la uwekezaji la EPZA, Ubungo Jijini Dar es Salaam.

-Mwisho-