Tuesday, June 21, 2016

Dkt. Mlima akutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Aziz Mlima akiwa katika na mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa India, Mhe. Amar Sinha, Mazungumzo hayo yalijikita katika kuboresha na kukuza mahusiano kati ya Tanzania na India hasa kwenye nyanja ya Viwanda ambayo itazalisha ajira kwa vijana na kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili.. 
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (wa kwanza kushoto), na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Ally Kondo na Bi. Mercy Kitonga wakinukuu mambo muhimu ya mazungumzo hayo.
Sehemu ya Ujumbe ulioambatana na Mhe. Sinha ukifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Dkt. Mlima na Mhe. Amar Sinha. Wa kwanza kulia ni Baloizi wa India nchini Tanzania, Mhe. Sandeep Arya
Mkutano ukiendelea.
Dkt. Aziz Mlima na Mgeni wake, Mhe. Amar Sinha wakiwa katika picha ya pamoja.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India akutuna na Waziri Mahiga.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) kulia akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa India, Bw. Amar Sinha alipokuja kumtembelea Ofisini kwake na Kufanya naye Mazungumzo kuhusu umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na India.
Mhe. Waziri akiwa katika mazungumzo na mgeni wake ambapo walijadili namna Tanzania na India zitakavyoweza kushirikiana katika sekta mbalimbali kama vile uwekezaji, elimu, afya, TEHAMA na ufundi.
Bw. Sinha akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo.
Mhe. Waziri akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India zawadi yenye picha za wanyama mbalimbali wanaopatikana katika hifadhi za taifa hapa nchini.




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India akutuna na Waziri Mahiga.

Tanzania imetakiwa kujifunza kutoka India kufuatia maendeleo makubwa yaliyofikiwa na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali za viwanda,  teknolojia, TEHAMA, kilimo, usalama na afya. Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India, Bw. Amar Sinha ofisini kwake

Waziri Mahiga alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa ushirikiano wa Tanzania na India katika sekta ya uchumi unahitajika kwa kiasi kikubwa ili Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli iweze kufikia malengo yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Alisema kuna umuhimu wa Tanzania na India kushirikiana kwa pamoja katika sekta za teknolojia, elimu, afya, elimu ya ufundi na TEHAMA ili kuiongezea uwezo Serikali iweze kufikia malengo yake yaliyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025.

Mhe. Waziri aliishukuru Serikali ya India kwa misaada ya miradi ya maendeleo inayotoa kwa Tanzania. Misaada hiyo ni pamoja na ununuzi wa matrekta kwa ajili ya kuboresha kilimo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 40 unaosimamiwa na SUMA-JKT.

Msaada mwingine ni ujenzi wa miundombinu ya maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam uliogharimu Dola za Marekani milioni 178.125. Aidha, India imekubali kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha maji kutoka Ziwa Victoria hadi katika mikoa ya Shinyanga na Tabora utakaogharimu Dola za Marekani milioni 268.35 pamoja na mradi mwingine wa maji utakaogharimu Dola za Marekani milioni 92 utakaojengwa visiwani Zanzibar.

Awali, Bw. Sinha alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima. Wawili hao walisisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa ajili ya faida ya wananchi wa pande zote mbili. Maeneo waliyoyainisha ni pamoja na kilimo, mafuta na gesi, madawa, afya, madini na uchumi wa bahari (Blue economy).

Kuhusu uchumi wa Bahari, Balozi Mlima alieleza kuwa hilo ni suala ambalo Mhe. Rais Magufuli analisisitiza kila siku katika vikao mbalimbali. Alimuomba Katibu Mkuu huyo kuangalia uwezekano wa kusaidia kutafuta wawekezaji wa uvuvi kwenye Bahari Kuu nchini ambayo kwa kauli ya Rais bado haijafanyiwa kazi ipasavyo.

Kwa upande wake, Bw.Amar Sinha alisema kuwa ziara yake imelenga kuimarisha mahusiano ya kihistoria yaliyopo kati ya Tanzania na India pamoja na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano. Alisema India itaendelea kushirikiana na Tanzania na inafurahishwa na mchango inaotoa ambao unasaidia katika uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia 7 kila mwaka.   


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 21 Juni 2016.

WAZIRI MAHIGA ASHIRIKI HAFLA YA MAADHIMISHO YA MIAKA 3 YA UONGOZI WA BABA MTAKATIFU PAPA FRANCIS


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akihutubia katika hafla ya kuadhimisha miaka mitatu ya uongozi wa Baba Mtakatifu Papa Francis na Kumuaga Balozi wa Vatcan hapa nchini aliye maliza muda wake wa uwakilishi.
Hafla ambayo ilifanyika jana katika viwanja vya kanisa la Mt. Petro  Osterbay Jijini Dar es Salaam

Mwakilishi wa Baba Mtakatifu na Balozi wa Vatican hapa nchini Balozi Francisco Montecillo Padilla, akihutubia katika Hafla hiyo ambapo alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Tanzania na watu wake kwa ukarimu, upendo pia ushirikiano aliokuwa akiupata kwa kipindi chote alichokuwa anawakilisha Taifa lake hapa nchini. 
Kutoka kulia ni Kadinali Pengo, Mke wa Rais wa awamu ya tatu, Mama Anna Mkapa na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Tarcisio Ngalalekumtwa wakifurahia jambo kwa pamoja. 
Sehemu ya Mabalozi waliohudhuria hafla hiyo
Waziri Mahiga akisalimiana na Kadinali Pengo wakati wa hafla hiyo
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin W. Mkapa akizungumza na Dkt. Mahiga
Mkuu wa Mabalozi hapa nchini Mhe. Ambrosio Montecillo akizungumza na mmoja wa Maaskofu waliokuwepo kwenye hafla Hilo
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine (wa kwanza kushoto), akizungumza na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe.Egon Kochanke
Askofu Francisco Montecillo Padilla akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mabalozi waliohudhuria hafla hiyo

=========================================




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

WAZIRI MAHIGA ASHIRIKI HAFLA  YA MAADHIMISHO YA MIAKA 3 YA UONGOZI WA BABA MTAKATIFU PAPA FRANCIS.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika hafla ya kuadhimisha  miaka mitatu ya Uongozi wa Baba Mtakatifu Papa Francis  pamoja na kumuaga Balozi wa Vatican  na muwakilishi wa Papa hapa nchini Askofu Francisco Montecillo Padilla ambaye amemaliza muda wake wa kuhudumu hapa nchini.

Hafla hiyo ilifanyika jana jioni katika viwanja vya Parokia ya Mtakatifu Petro Osterbay Jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo Mhe. Mahiga alimpongeza Papa Francis pamoja na kumuelezea kuwa ni mtu wa Mataifa yote na mfano wa kiongozi bora duniani kwakuwa misingi yake ya uongozi imejikita katika kusimamia utu, kupinga Ubaguzi wa rangi pamoja na matabaka katika jamii. Pia amekuwa mpiganaji mkubwa katika masuala ya amani na mtetezi wa wakimbizi hivyo Tanzania na Dunia nzima inatambua mchango wake kwa ujumla na kuzidi kumwombea mafanikio katika utendaji wake.

Vilevile alimpongeza Askofu Francisco Montecillo Padilla ambaye amekuwa akihudumu  nchini  kwa muda wa miaka minne (4) na kueleza kuwa amekuwa mfano bora katika kazi za kichungaji kwa kuweza  kutembelea  nchi nzima katika Majimbo ya Kanisa Katoliki licha ya kazi yake kuwa na changamoto nyingi. Alikumbusha tukio la mlipuko lililotokea kanisani  mjini Arusha wakati Askofu Padilla akiendesha Ibada, ni mfano dhahiri wa kazi alizokuwa akizifanya nchini na katika hilo amejiwekea historia katika huduma yake ya kichungaji.

Kwa upande wa ushirikiano  baina ya Tanzania na Vatican, Mhe. Mahiga alieleza ni wa muda mrefu tangu 1960. Katika kuhakikisha uhusiano huo unaimalika mataifa hayo mawili yamekuwa yamekuwa yakifanya jitihada za makusudi katika kukuza uhusiano huo na alieleza hilo lilidhihirishwa na ujio wa Papa John Paul wa pili ambaye alifanya ziara nchini Tanzania mwaka 1990.

Pia alieleza Mhe. Rais Magufuli anapenda kutoa shukurani za dhati kwa huduma ambazo zimekuwa zikifanywa na Balozi wa Papa nchini pamoja na Kanisa Katoliki katika kuchangia shughuli za maendeleo hasa katika sekta ya Afya na Elimu ambapo wamefungua Shule za ufundi za Don Bosco katika Mikoa yote ."Ni imani yangu kuanzishwa kwa shule hizo hakutaishia katika ngazi ya mikoa tu, bali utaendelea katika ngazi ya wilaya na hata kata"

Aidha, alizungumzia sera ya viwanda ya  Mhe. Rais John Pombe Magufuli katika kuondoa tatizo la kukosa ajira na kukuza uchumi wa Taifa, alimweleza Balozi huyo ni muda muafaka sasa mataifa hayo mawili yakajikita zaidi katika kuhakikisha yanaibua maeneo mapya ya ushirikiano ili kuhakikisha sera hiyo inafikiwa kwa kuvutia zaidi wawekezaji na kukuza biashara.

Watu wengine mashuhuri waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin W. Mkapa na mke wake Mama Anna Mkapa, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Kadinali Polycarp Pengo na  Maaskofu wa Majimbo ya Kanisa Katoliki nchini, wengine ni Watawa na Walei.
    
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 21 Juni 2016.



MHE. WAZIRI BALOZI DKT. MAHIGA AKUTANA NA RAIS WA SERIKALI YA ZANZIBAR MHE. DKT. SHEIN





Rais wa Serikali ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein akielezea jambo kwa Waziri  Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alipomtembelea Ofisini kwake Ikulu, Zanzibar mwishoni mwa wiki


Rais wa Serikali ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) alipomtembelea Ikulu Zanzibar.
Rais wa Serikali ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein (kulia) akiwa na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) alipotembelea Zanzibar mwishoni mwa wiki.
Rais wa Serikali ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt. Ali Mohamed Shein (kulia) akiwa katika mazungumzo na  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) aliotembelea Ikulu 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar