Monday, June 8, 2020

SERIKALI YAAGIZA CHUO CHA DIPLOMASIA KUONGEZA TAFITI, MACHAPISHO


Serikali imekiagiza Chuo cha Diplomasia kujikita kuongeza tafiti pamoja na machapisho mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha wahitimu wa chuo hicho kutoa mchango wao katika Taifa hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.

Maagizo hayo yametolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipotembelea chuo hicho na kuongea na wahadhiri, wafanyakazi pamoja na wanafunzi.

Dkt. Ndumbaro amesema ili chuo cha diplomasia kiendelee kuheshimika zaidi duniani lazima kihakikishe kuwa kinazalisha tafiti na machapisho ya kutosha.

"Utafiti na machapisho siyo suala la wahadhiri peke yao…..siyo suala la wanafunzi peke yao ni suala la wanachuo…… mawazo yenu lazima yafanyiwe utafiti kwa kushirikiana na wahadiri wenu na ni lazima tuwe na machapisho zaidi," Amesema DKt. Ndumbaro

Naibu Waziri ameongeza kuwa moja kati ya changamoto inayoikumba diplomasia hivi sasa ni mabadiliko ya mifumo mbalimbali duniani ambapo wanadiplomasia wanapaswa kujua kuwa dunia ipo katika mlengo upi, hivyo vyema mkajikita katika tafiti zenu ili kuweza kusaidia kufafanua masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa yanayotokea duniani.

"Lakini pia niliagiza muongeze lugha zaidi kwa sababu pia diplomasia pia ni mawasiliano na unawasiliana na watu wa lugha tofauti tofauti, kwa hiyo tuongeze lugha mbalimbali ili diplomasia iweze kufanya kazi yake," Amesema DKt. Ndumbaro.

Aida, Naibu Waziri ameagiza pia chuo hicho kuanzisha semina za kila mwezi ambapo zitajumuisha Wahadiri na wanafunzi pamoja na mabalozi wastaafu kwa lengo la kujadili mambo yanayohusu diplomasia na kuwapa uzoefu wa masuala ya kidiplomasia.

Wanafunzi kwa upande wao wamepata fursa ya kumuelezea Naibu Waziri changamoto mbalimbali zinazo wakabili zikiwemo za kupata asilimia ndogo za mkopo wa elimu ya juu, ukosefu wa mafunzo kwa vitendo, ukosefu wa mabweni pamoja na mazingira ambayo siyo wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

"Mkopo tunaopewa ni mdogo sana na hautoshi hivyo tunaomba serikali itusaidie kutuongezea fedha za mkopo ili tuweze kukidhi mahitaji yetu wakati tunapokuwa chuoni,"Amesema Isack Sadock  

Pia, Dkt. Ndumbaro baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wanafunzi chuoni hapo, ameuagiza uongozi wa chuo kuandaa na kuratibu mafunzo kwa vitendo badala ya kufuatiliwa na wanafunzi, kutoa huduma stahiki kwa wanafunzi wenye ulemavu/maitaji maalumu ili waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Nae Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera amemhakikishia Naibu Waziri kuwa chuo kitayafanyia kazi na kuyatekeleza maagizo yote aliyoyatoa.

"Mhe. Naibu Waziri naomba nikuhakikishie kuwa maagizo yako tumeyapokea……….mimi kwa kushirikiana na menejimenti, wahadhiri na wafanyakazi tayafanyia kazi kwa wakati," Amesema Dkt. Ponera  
Aidha, Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro amekagua mradi wa ujenzi wa jengo jipya la chuo cha Diplomasia.

Katika hatua nyingine, ametoa msimamo wa Serikali kuhusu changamoto zinazojitokeza mipakani hasa katika mpaka wa Tanzania na Kenya na kusema kuwa Serikali ipo kwenye mazungumzo na Kenya ili kuweza kubaini tatizo ni kitu gani.

"Kwa sasa tupo kwenye majadiliano na wenzetu wa Kenya na kuona tatizo ni kitu gani je ni corona tu au ni zaidi ya corona? Msimamo wa serikali yetu ni kuwa kila nchi ipime watu wake…..na tunaamini huo ndiyo msimamo sahihi wa diplomasia ya uchumi," Amesema Dkt. Ndumbaro.

Chuo cha Diplomasia kilianzishwa rasmi tarehe 13 Januari 1978 kwa kusainiwa Makubaliano yaliyofanywa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wa wakati huo, Mhe. Benjamini William Mkapa wa Tanzania na Mhe. Joaquim Chissano wa Msumbiji.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera (aliyesimama ktk meza kuu) akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipotembelea chuo hicho leo na kuongea na wahadhiri, wafanyakazi pamoja na wanafunzi 

Baadhi ya wanafunzi wakimsikiliza Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (hayupo pichani)

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro akiongea na wanafunzi (hawapo pichani)

Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro akioneshwa mchoro wa jengo jipya la chuo cha Diplomasia na meneja mradi Abdalla Khama 

Meneja mradi wa jengo jipya Abdalla Khama akimuelezea jambo Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro wakati alipotembelea eneo la mradi

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera (aliyesimama) akimkaribisha Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro (aliyekaa wa kwanza kushoto) kwenye kikao cha menejimenti ya chuo  




Saturday, June 6, 2020

UNFORGETTABLE EXPERIENCE


NCHI ZA NORDIC ZAAHIDI KUENDELEZA, KUIMARISHA UHUSIANO WAKE NA TANZANIA


Nchi za NORDIC ambazo ni Norway, Sweden, Finland na Dernmark zimeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuhakikisha kuwa Tanzania inasonga mbele katika maendeleo yake kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Akiongea wakati wa maadhimisho ya wiki ya Nordic jijini Dar es Salaam, Balozi wa Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen amesema kuwa nchi za Nordic zimeadhimisha wiki ya Nordic nchini Tanzania na zimejadili masuala ya malengo ya maendeleo endelevu ambapo pamoja na mambo mengine, wametumia wiki ya Nordic kuendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Nordic na Tanzania.

"Wiki ya Nordic inatoa fursa ya kushirikiana na kujifunza mambo mbalimbali yakiwemo ya kijamii, kisiasa na kichumi pamoja na kupata uzoefu wa maendeleo kutoka kwa kila mmoja wetu," Amesema Balozi Jacobsen.

Ameongeza kuwa, nchi za Nordic zimejidhatiti kufanya kazi kwa karibu na Tanzania ili kuhakikisha kuwa Tanzania inasonga mbele katika maendeleo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiongea mara baada ya kukabidiwa mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu ikiwa ni ishara ya kuhamasisha maendeleo ya Tanzania, amesema kuwa mpira huo ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi za Nordic.

"Ushirikiano wetu (Tanzania) na nchi za Nordic ni wa muda mrefu kabla ya uhuru na hata baada ya uhuru. Tumekuwa tukifurahia ushirikiano wetu na nchi za Nordic na umekuwa ukimarika kila wakati, ni matumaini yetu sisi kama serikali kuwa uhusiano utaendelea kuimarika zaidi," amesema Dkt. Ndumbaro     

Mwezi Novemba 2019, ulifanyika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya nje wa Afrika na Nordic, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo uzikutanisha nchi za Afrika na Nordic na kutoa fursa ya kujadili masuala mbalimbali yakiwemo, elimu, kilimo biashara na uwekezaji.

Balozi wa Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen akimkabidhi mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.  Damas Ndumbaro (Mb) jijini Dar es Salaam 

Kaimu Balozi wa Denmark nchini, Mhe. Mette Pilgaard (wa pili kushoto) akiwaelezea jambo Mabalozi wa Sweden, Mhe. Anders Sjöberg, (wa kwanza kushoto), Norway Mhe. Elisabeth Jacobsen na Finland Mhe. Riitta Swan pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.   Damas Ndumbaro (Mb) akiwaelezea jambo Mabalozi wa nchini za Nordic

Balozi wa Sweden nchini, Mhe. Anders Sjöberg (wa kwanza kushoto) akiongea na mabalozi wenzake wa nchini za Nordic pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.  Damas Ndumbaro (Mb)         

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.   Damas Ndumbaro (Mb) akiwa ameshikilia mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu katika picha ya pamoja na mabalozi wa nchini za Nordic   

Mabalozi wa nchini za Nordic pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakipiga makofi mara baada ya naibu waziri kukabidiwa mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.   Damas Ndumbaro (Mb) pamoja na mabalozi wa nchini za Nordic wakiwa wameshikilia mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu


Monday, June 1, 2020

KATIBU MKUU BALOZI KANALI IBUGE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA TAIFA LA ISRAEL KWA TANZANIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Taifa la Israel  kwa Tanzania Mhe. Oded Joseph ambaye analiwakilisha Taifa hilo kutokea Nairobi, Kenya.

Kanali Balozi Ibuge katika mazungumzo hayo amweleza Balozi Oded, kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kukakabiliana  na kusambaa kwa COVID-19 
na madhara sambamba na madhara cake.
Aidha, pamoja na mambo mengine Wawili hao katika mazungumzo yao wamejadili masuala mbalimbali ikiwemo ya kuendelea kukuza na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na biashara baina ya Tanzania na Israel. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akifafanua jambo kwa Balozi wa Taifa la Israel nchini Mhe.Balozi Oded wakati wa mazungumzo. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge akiagana na Balozi wa Taifa la Israel nchini Mhe.Balozi Oded  mara baada ya kuhitimisha mazungumzo yao.

Sunday, May 31, 2020

Awamu ya Pili ya Watanzania warejea nchini kutoka India kutokana na ugonjwa wa COVID-19

Baadhi ya watanzania waliokuwa wamekwama India kutokana na ugonjwa wa COVID-19 wakiwa ndani ya ndege maalum ya Air Tanzania wakisubiri kuondoka kurejea Tanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji Jijini Mumbai tarehe 30 Mei 2020. Serikali ya India ilisitisha huduma ya kuingia na kutoka kwa ndege za kimataifa ikiwa ni moja ya mkakati wa kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19.
Sehemu nyingine ya watanzania waliokuwa wamekwama nchini India wakiwa ndani ya ndege maalum ya Air Tanzania wakisubiri kuondoka kurejea Tanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji Jijini Mumbai tarehe 30 Mei 2020.

Baadhi ya watanzania waliokuwa wamekwama India wakisubiri kuingia katika ndege maalum ya Air Tanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji Jijini Mumbai tarehe 30 Mei 2020.

Ndege  aina ya Boeng 787-8 ya Dreamliner ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) ikipakia watanzania 119 waliokuwa wamekwama nchini India katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji Jijini Mumbai tarehe 30 Mei 2020.
================================================
Serikali yarejesha kwa awamu ya pili Watanzania 192 waliokuwa wamekwama nchini India kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19
Ubalozi wa Tanzania nchini India kwa kushirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania [ATCL] pamoja na Diaspora wa Tanzania nchini India kwa mara nyingine wamefanikisha safari ya pili ya kuwarejesha nchini Watanzania 192 waliokuwa wamekwama katika miji mbalimbali nchini India. Watanzania hao walikwama kutokana na zuio la kuingia na kutoka kwa ndege za Kimataifa lililowekwa na Serikali ya India kama hatua mojawapo ya kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Ndege maalum ya aina ya Boeng 787-8 ya Dreamliner ya Shirika la Ndege la Tanzania ilitumwa tena na Serikali Jijini Mumbai kuja kuwachukua Watanzania hao waliokwama nchini India tangu tarehe 22 Machi 2020 lilipowekwa zuio hilo na Serikali ya India. Ndege hiyo iliondoka tarehe 30 Mei 2020 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji,  Mumbai ikiwa imebeba jumla ya raia wa Tanzania 192, miongoni mwao ni waliokuwa wamekwenda India kwa ajili ya matibabu; wahitimu kutoka vyuo mbali mbali na wanafunzi ambao wanalazimika kurudi nyumbani kwa kuwa vyuo vimefungwa hadi mwezi Agosti/Septemba 2020.
Tofauti na awamu ya kwanza, safari hii pia ilihusisha kuwarejesha nchini India raia wa nchi hiyo wapatao 202 ambao walikuwa wamekwama nchini Tanzania. Hatua hii ya Serikali ya Tanzania itasaidia sana katika kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya India na Tanzania.
Mpaka sasa jumla ya Watanzania 438 wamerejeshwa Tanzania kutoka India kwa utaratibu huu maalum. 

Friday, May 29, 2020

PROF. KABUDI AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA ITALIA NCHINI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge, ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu mahusiano baina ya Tanzania na Italia.

Aidha, walitumia mazungumzo hayo kujadili hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania pamoja na Serikali ya Italia katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19. Mhe. Waziri alifahamisha kuwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kwenye mapambano ya ugonjwa huo zimezingatia mazingiria na hali halisi ya Tanzania pamoja na nchi jirani zinazozunguka Tanzania.

Kwa upande wake Balozi Mengoni alipongeza juhudi hizo za Serikali ambapo alifahamisha kuwa Serikali yake ya Italia inaziunga mkono na kwamba ipo tayari kutoa ushirikiano pale itakapohitajika kufanya hivyo.

Viongozi hao walikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria baina ya Mataifa hayo mawili ambao umejikita katika sekta za elimu, afya, utalii pamoja na biashara na uwekezaji.


Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akimuelezea jambo Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge




PROF. KABUDI ATAKA NCHI ZA SADC KUIMARISHA USHIRIKIANO




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof Palamagamba kabudi (Mb) (wa kwanza kushoto) akiongea na wajumbe wa mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya (Video Conference) leo Jijini Dar es Salaam 


Baadhi ya Mawaziri pamoja na maafisa waandamizi/ makatibu wakuu wakifuatilia mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya (Video Conference) leo Jijini Dar es Salaam 


Baadhi ya maafisa waandamizi/ makatibu wakuu wakifuatilia mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya (Video Conference) leo Jijini Dar es Salaam 
Baadhi ya mawaziri wakifuatilia mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya (Video Conference) leo Jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika kwa njia ya (Video Conference) leo Jijini Dar es Salaam wakifuatilia mkutano huo


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof Palamagamba Kabudi amezitaka Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuimarisha ushirikiano na umoja wakati huu wa kuenea kwa janga la  Virusi vya Corona huku bidhaa na huduma muhimu zinazovuka mipaka baina ya nchi na zikiendelea kutolewa.

Prof. Kabudi amesema hayo jijini Dar es salaam wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC kwa njia ya Video katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Nawaomba Nchi zote Wanachama wa SADC tuimarishe umoja na mshikamano wetu wakati huu wa kuenea kwa janga la Virusi vya Corona, huku bidhaa na huduma muhimu zinazovuka mipaka baina ya nchi nan chi zikiendelea kutolewa, huu ni wakati wa kuepuka vitendo vya kujitenga na kuongeza mashauriano baina ya nchi,” amesema.

Aidh Mhe Waziri ameziomba Nchi za SADC kuwapa heshima na kuthamini utu wa madereva wanaosafirisha bidhaa na huduma muhimu kuvuka mipaka ya nchi kwa wakati huu ambao ugonjwa wa corona umeenea katika nchi wanachama.

Amesema Nchi wanachama zinapaswa kuchukua hatua za kukabiliana na ueneaji wa virusi vya Corona bila ya kuwanyanyapaa madereva na kuwachukulia kama watu wanaosambaza virusi hivyo na kuongeza kuwa madereva hao wanapaswa kupewa heshima stahiki kama binadamu wengine na kuwashukuru kutokana na hatari wanayochukua ya kusafirisha mizigo na huduma wakati huu wa kuenea kwa janga hilo.

“Madereva wetu wamevunjika moyo kwa sababu wanaonekana kama wao ndio wanaosambaza virusi vya Corona na sio askari wazuri ambao wanatoa huduma ya kusafirisha huduma na biidhaa muhimu wakati huu wa mlipuko, katika nchi za jumuiya,”

Ameziomba nchi za SADC kuwapa heshima na kuthamini utu wa madereva hao huku zikiendelea kuchukua tahadhari za kupambana na janga la virusi vya corona na kuongeza kuwa umoja wetu ni muhimu sana kwa wakati huu.

“Naziomba nchi zetu tuwape heshima na kuthamini utu wa madereva hao na kuwapa heshima wanayostahili huku tukiendelea kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya katika kukabiliana na janga hilo,” alisema.

Prof. Kabudi amesema janga la COVID 19 linaonekana kama halitoisha ndani ya muda mfupi na nchi za ukanda wa SADC lazima ziishi  kwa kufuata mifumo salama katika biashara na usafirishaji wa huduma na bidhaa ili kupata ukuaji wa uchumi na kuondoa umasikini huku tukiwa bado tunakabiliana na janga hili la ueneaji wa virusi vya corona.

Amesema wakati hatua za kukabiliana na janga la Corona zikiendelea kuchukuliwa nchi za SADC lazima zikumbuke dhumuni la utangamano miongoni mwa nchi wanachama ambalo ni kuboresha ufanyaji biashara baina ya nchi na nchi na hivyo kutowaangusha waanzilishi wa Jumuiya ya SADC.

Amesema ufanyaji wa biashara baina ya nchi na nchi ndani ya SADC uko chini ya asilimia 20 hali ambayo inazuia nchi wanachama kuona ukuaji wa uchumi wake na kuongeza kuwa janga la corona lichukuliwe kama chachu ya kuongeza juhudi za kuinua kiwango cha ufanyaji biashara baina ya nchi na nchi kupitia utekelezajia wa Protokali ya SADC katika biashara ya 2005 na uanzishwaji wa eneo huru la biashara la SADC.

Ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la SADC Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwele na Waziri wa Maliasilia na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala. 


Thursday, May 28, 2020

PROF. KABUDI AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA MABALOZI WA UFARANSA, UTURUKI NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Pamalagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier ambapo pamoja na mambo mengine, Balozi Clavier ameipongeza Tanzania kwa hatua ilizochukua kupambana na janga a virusi vya corona nchini.

Balozi Clavier pia amemhakikishia Mhe. Waziri kuwa Ufaransa inaiunga mkono Tanzania kwa asilimia 100 kwa hatua ilizochukua kupambana na janga la virusi vya corona na kusema Ufaransa itaipatia Tanzania Euro milioni 30 ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu na riba ndogo kwa ajili ya kupambana na janga la virusi vya Corona pamoja na kusaidia kuinua uchumi.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Waziri Kabudi amemuelezea Balozi wa Ufaransa jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na Janga la Corona nchini na kumhakikishia utayari wa Tanzania katika kupambana na janga hilo na kuongeza kuwa Serikali ya Tanzania ilichukua hatua hizo kulingana na hali halisi ya maisha ya watanzania.

Prof. Kabudi amesema hatua zilizochukuliwa na Tanzania zililenga kuwafanya watanzania kuendelea na maisha yao bila ya kuathiriwa kiuchumi huku wakijilinda na kuchukua tahadhari ambazo zilikuwa zikitolewa na wataalamu wa afya nchini na duniani.

Balozi Clavier amemuambia Mhe. Waziri Kabudi kuwa Ufaransa pia imetoa msaada wa Dola 500,000 ambazo watapewa wakulima wadogowadogo 6,000 nchini kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha kilimo chao na maghala ya kuhifadhia mazao yao.

Ameongeza kuwa Rais wa Ufaransa ameziandikia nchi za G20 na Paris Club kuzishawishi kuahirisha ulipaji wa madeni na riba zake na pia kufuta kabisa madeni hayo ili kuimarisha uchumi ambao umeathiriwa na janga la corona katika nchi zinazoendelea.

Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi amekutana na kuagana na Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Ali Davutaglu ambaye amemaliza muda wake wa utumishi na amemtakia maisha mema na kumwambia kuwa ni matarajio yake kuwa atakuwa Balozi wa hiari wa Tanzania nchini uturuki na kwingineko duniani.

Naye balozi Davotaglu ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa ikimpatia alipokuwa akitekeleza majukumu yake nchini na kuahidi kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea zawadi ya kitabu cha Mwl. Nyerere kutoka kwa Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Frederic Clavier


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimuelezea jambo Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier wakati alipokutana na balozi huyo leo katika ofisi ndogo za wizara Jijini Dar es Salaam


Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) wakati balozi huyo alipokutana na Mhe. Waziri leo katika ofisi ndogo za wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na Balozi wa Uturuki nchini ambaye amemaliza muda wake wa utumishi, Mhe. Balozi Ali Davutaglu wakati walipokutana kwa mazungumzo katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Balozi Ali Davutaglu akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) wakati walipokutana kwa mazungumzo katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) pamoja na Balozi wa Uturuki nchini, Mhe. Balozi Ali Davutaglu wakiangalia picha ya kazi zilizofanywa na Ubalozi wa Uturuki wakati walipokutana kwa mazungumzo katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimkabidhi zawadi ya picha Balozi wa Uturuki nchini aliyemaliza muda wake wa utumishi, Mhe. Balozi Ali Davutaglu 


Wednesday, May 27, 2020

SADC: NGAZI YA MAKATIBU WAKUU WAPENDEKEZA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA MIPAKANI


Makatibu Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamependekeza kuruhusu Biashara za bidhaa zote kuendelea kusafirishwa katika Nchi zao kama ilivyokuwa kabla ya janga la Virusi vya Corona.

Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC kwa ngazi ya Mkatibu Wakuu uliofanyika kwa njia ya Mtandao (video conference) leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Makatibu Wakuu amesema mkutano huo umejadili na kutoa mapendekezo ya kuondoa vikwazo vyote vya kibiashara ili kuweza kuendeleza uchumi ndani ya Jumuiya.

Balozi Ibuge amesema kuwa uamuzi huo utawawezesha wananchi kuendelea na maisha yao ya kawaida na biashara zao kwa kuwa janga la COVID 19 litaendelea kuwepo kwa muda ambao ukomo wake haujulikani japo juhudi za kuukabili ugonjwa huo zinaendelea.

“Kikao cha makatibu cha makatibu wakuu cha leo, kimependekeza  kuondoa kikwazo cha bidhaa mahususi tu kupita katika mipaka yetu badala yake bidhaa zote zinazowezesha wananchi wetu kuendelea na maisha ni lazima ziruhusiwe kupita katika mipaka ya nchi wanachama wa SADC” Amesema Balozi Ibuge.

Aidha, Katibu Mkuu ameongeza kuwa ni muhimu wa wanaSADC kujumuika katika wakati huu na kuona ni jinsi gani wanaweza kushirikiana na kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi wanachama wa SADC unakua kwa kuongeza juhudi katika sekta ya biashara. 
  
Balozi Ibuge ameongeza kuwa “kwa mfano halisi sisi kama Tanzania hatukufunga mipaka yetu, na katika kutokufunga mipaka yetu bado tunatambua kwamba tunaendelea kuwategemea wenzetu kama wanavyotutegemea sisi............tuna badari inayohudumia nchi nane za SADC na zisizokuwa za SADC na ambazo ndizo hasa tunapozungumzia utengamano na mazingiara ya kufanya biashara na kuzingataia tahadhari mbalimbali za uonjwa wa COVID 19 ambazo nchi hizo zimekuwa zikichukua,"

Aidha, Mkutano huu pia umejadili hali ya kifedha ndani ya Jumuiya, Utekelezaji wa Maazimio yaliyotokana na kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC ambayo ni Menejimenti ya Maafa, utekelezaji wa kaulimbiu ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC isemayo "Mazingira Wezeshi kwa ajili ya Maendeleo Endelevu na Jumuishi ya Viwanda, Kukuza Biashara na Ajira ndani ya SADC" na mapitio ya hali halisi ya biashara baina ya nchi, maendeleo ya viwanda ndani ya Jumuiya na taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa Jumuiya na Mpango kazi wake.

Mkutano huo umahusisha wataalamu kutoka nchi wanachama 12 wa SADC kutoka sekta za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha na Mipango, Uchukuzi na Mawasiliano, Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii pamoja na Afya. Mkutano huo pia utatoka na maazimio ambayo nchi wanachama watatakiwa kuyatekeleza ndani ya muda utakaokubaliwa.

Nchi zilizoshiriki Mkutano huo ni pamoja na Angola, Afrika Kusini, Comoro, Eswatini, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na Mwenyekiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC kwa ngazi ya Mkatibu Wakuu uliofanyika kwa njia ya Mtandao (video conference) leo jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge (wa kwanza meza kuu kushoto) akiongea na wajumbe wa mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC kwa ngazi ya Mkatibu Wakuu uliofanyika kwa njia ya Mtandao (video conference) leo jijini Dar es Salaam