Tuesday, October 19, 2021

TANZANIA, CHINA ZAAHIDI KUIMARISHA MISINGI YA DIPLOMASIA

 Na Mwandishi wetu, Dar

Tanzania na China zimeahidi kuendelea kuimarisha misingi ya uhusiano wa diplomasia baina ya mataifa hayo iliyodumu kwa zaidi ya miaka 50 kwa lengo la kukuza na kuendeleza maendeleo endelevu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Chen Mingjian, wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amesema kuwa pamoja na mambo mengine, wamejadili masuala mbalimbali ikiwemo suala la kukuza na kuendeleza misingi ya uhusiano wa kidiplomasia iliyowekwa wakati wa kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya mataifa haya 1964.

“Uhusiano wa Tanzania na China ni wa muda mrefu na umekuwa imara katika nyakati zote hii ni kutokana na kila taifa kuheshimu misingi ya taifa jingine na kutokuingilia masuala ya ndani ya taifa jingine, naamini kwa kuzingatia misingi hii uhusiano huu utaendelea kukua na kuimarika zaidi,” Amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa wakati wote Tanzania na China zimekuwa na maelewano mazuri ambayo yamechangia kuimarisha diplomasia kwa mataifa hayo.

Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Chen Mingjian, ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa ikimpatia tangu aliwasili na kuongeza kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya mataifa mawili.

“Naamini kuwa mimi ni kiungo cha kuimarisha na kuendeleza uhusiano baina ya China na Tanzania…..tumekuwa tukishirikiana katia sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, biashara na uwekezaji, miradi ya mikopo nafuu na misaada, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Uchukuzi, Utalii na utamaduni naahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” Amesema Balozi Mingjian

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Chen Mingjian wakati walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Balozi wa China hapa nchini Mhe. Chen Mingjian akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati walipokutana kwa mazungumzo leo katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Chen Mingjian yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Chen Mingjian yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Balozi wa China hapa nchini Mhe. Chen Mingjian akimkabidhi zawadi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam


Monday, October 18, 2021

TANZANIA, KENYA KUMALIZA VIKWAZO VYA KIUTAWALA DISEMBA

Na Mwandishi Wetu, Dar

Tanzania na Kenya zimedhamiria kumalizia kuondoa vikwazo vya kiutawala vilivyosalia ifikapo Disemba 2021 baada ya kuondoa vikwazo 46 visivyokuwa vya kikodi.

Hayo yamesemwa wakati wa mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Mhe. Dany Kazungu jijini Dar es Salaam ambapo takwimu zinaonesha urari wa biashara kati ya Nchi hizo umeongezeka mara sita zaidi baada ya kuondolewa kwa vikwazo hivyo.

Kutokana na hatua hiyo, Tanzania imeonekana kunufaika zaidi kwa kuondolewa kwa vikwazo hivyo kwa kuuza zaidi bidhaa zake nchini Kenya.

“Hii ni ishara nzuri kwa Tanzania lakini pia ni fursa kwa Tanzania na Kenya kuondoa umaskini kwa watoto wetu na ndugu zetu kupata ajira kwa wingi katika sekta ya biashara,” Amesema Mhe. Kazungu

Pia Balozi Kazungu amemueleza Waziri Mulamula kuhusu azma ya Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kufanya ziara rasmi hapa nchini na kisha kuhudhuria sherehe za Uhuru tarehe 9 Disemba 2021 ambapo alialikwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipotembelea Kenya mapema mwaka huu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema Tanzania inaheshimu makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa awali wa kuondo vikwazo hivyo na dhamira ni kuwa ifikapo Disemba 2021 vikwazo vya kiutawala navyo viwe vimeondolewa ili kukuza zaidi mahusiano ya Kidiplomasia na Biashara baina ya Tanzania na Kenya.

“Tumekubaliana kuhakikisha ifikapo mwezi Disemba 2021 vikwazo vyote vya kitawala viwe vimetatuliwa……….azma yetu ni kuhakikisha kuwa kila kitu kinakuwa sawa kwa Ustawi wa Diplomasia na biashara baina ya Tanzania na Kenya,” amesema Balozi Mulamula.

Katika tukio jingine, Balozi Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mwakilishi wa Taasisi ya Sister Cities ya Marekani Bi. Ronda Pierce katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Mhe. Dany Kazungu akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara leo Jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimuleleza jambo Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Mhe. Dany Kazungu walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara leo Jijini Dar es Salaam


Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Mhe. Dany Kazungu yakiendelea katika Ofisi ndogo za Wizara leo Jijini Dar es Salaam


Mwakilishi wa Taasisi ya Sister Cities ya Marekani Bi. Ronda Pierce akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi ndogo za Wizara leo Jijini Dar es Salaam


Mazungumzo baina ya wakilishi wa Taasisi ya Sister Cities ya Marekani Bi. Ronda Pierce na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) yakiendelea katika Ofisi ndogo za Wizara leo Jijini Dar es Salaam



  

Friday, October 15, 2021

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI ATETA NA BALOZI WA CHINA HAPA NCHINI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) aakiwa katika mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa Nchini Balozi Chen Mingjian.

Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amekumbushia utekelezwaji wa ahadi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi ya kuipa Tanzania masoko ya bidhaa za asali na mabondo, ahadi aliyoitoa Chato Mkoani Geita mwezi Januari,2021 wakati wa ziara yake hapa nchini


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa Nchini Balozi Chen Mingjian mara baada ya kumaliza mazungumzo.

VACANCY ANNOUNCEMENT AT THE CONSULATE OF THE REPUBLIC OF KENYA IN ARUSHA, TANZANIA.

 


CLICK HERE TO OPEN THE LINK

Thursday, October 14, 2021

BALOZI MBAROUK ATETA NA DKT. MATHUKI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki leo katika Ofisi za Jumuiya hiyo leo Jijini Arusha.  

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk (Mb) akisalimiana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki leo katika Ofisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jijini Arusha


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk (Mb) akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki leo katika Ofisi za Jumuiya hiyo Jijini Arusha

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk (Mb) akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki leo katika Ofisi za Jumuiya hiyo Jijini Arusha

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk (Mb) leo katika Ofisi za Jumuiya hiyo Jijini Arusha


Afrika yajiandaa kuzalisha chakula cha kutosha

Afrika yajiandaa kuzalisha chakula cha kutosha

Na. Mwandishi Maalum, Addis Ababa

Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Afrika umefunguliwa leo jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo pamoja na mambo mengine, Mawaziri watapitia Andiko na mikakati ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Mwaka 2022 ya “Lishe na Usalama wa Chakula barani Afrika”. Kaulimbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa lishe bora kwa ajili ya ukuaji na ustawi wa watoto barani Afrika, bara ambalo kwa miaka mingi limekuwa linakabiliwa na uzalishaji mdogo wa chakula.    Hivyo, nchi za Afrika zinashauriwa kutekeleza mapendekezo ya Progarmu ya Afrika ya Maendeleo ya Kilimo na Azimio la Malabo kuhusu kilimo ili kuondokana na changamoto ya lishe duni.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo na katika mijadala yake, pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha ya kazi katika Umoja wa Afrika.

Mhe. Mulamula atakumbusha na kulisisitiza suala hilo kwa sababu limeainishwa katika kaulimbiu ya mwaka 2021 ambayo pamoja na mambo mengine, imehimiza matumizi ya lugha za kiafrika na Kiswahili ni moja ya lugha hizo ambayo inakuwa kwa kasi na kuzungumzwa na watu wengi barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Aidha, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa kuhusu ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo katika hotuba ya ufunguzi ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo alisistiza umuhimu wa nchi wanachama kuzingatia tahadhari za maambukizi ya UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na kuhamasisha watu wao kupata chanjo ya ugonjwa huo, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha kuwa nchi za Afrika zinapata idadi ya kutosha ya chanjo kwa ajili ya watu wake.

Katika Mkutano huo pia, Mawaziri wa Mambo ya Nje watapitia na kupitisha bajeti ya Mwaka 2022 ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika na kufanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi, zikiwemo za makamishna wawili wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais na Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Pan Africa, wajumbe wanne wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na wajumbe wanne wa Bodi ya Ushauri ya Afrika ya Kupambana na Rushwa.  

Vile vile, Mkutano wa 39 wa Mawaziri utapitia na kupitisha miundo ya taasisi saba za Umoja wa Afrika, ukiwemo muundo wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika ambalo Tanzania imeridhia Mkataba wake hivi karibuni. Kupitishwa kwa miundo hiyo itakuwa ni fursa zikiwemo za ajira kwa nchi wanachama, hivyo, Balozi Mulamula amewataka Watanzania kuzichangamkia, pindi zitakapotangazwa.

  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kushoto)  na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bi. Eliza Rwitunga wakiwa katika kikao cha kujiandaa na ujumbe wa Tanzania kabla ya kuingia kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Afrika.


Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akisoma hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa 39 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 14 na 15 Oktoba 2021

Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz (kulia) na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Balozi Caroline Chipeta wakisikiliza hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa 39 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 14 na 15 Oktoba 2021


Ujumbe wa Tanzania katika kikao cha maandalizi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula 

ujumbe wa Tanzania ukijumuisha maafisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia wakiwa katika kikao cha maandalizi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula. 

Picha ya pmoja ya Mawaziri wa nchi za Umoja wa Afrika wanaoshiriki Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za AU jijini Addis Ababa, Ethiopia.


 

Wednesday, October 13, 2021

Balozi Bana awapokea Wanajeshi watakao shiriki Michezo ya Amani na Mshikamano ya Kijeshi, nchini Nigeria.


Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana amewapokea Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliowasili nchini humo kujumuika na wanamichezo wengine kutoka nchi mbalimbali za Barani Afrika kushiriki michezo ya Amani na Mshikamano ya Kijeshi ya Sahel Barani Afrika iliyoandaliwa na Taasisi ya Michezo ya Kijeshi Afrika (Organization of Military Sports in Africa - OSMA) Sahel Countries Military Games for Peace and Solidarity.

Sambamba na kuwajengea utimamu wa mwili na akili washiriki Wanajeshi wanaoshiriki michezo hii, michezo hiyo pia inalenga kujenga umoja, ushirikiano na udugu miongoni mwao hasa katika kupambana na vitendo vya uhalifu katika eneo la Sahel na kuleta amani katika eneo hilo ambalo limekuwa na matatizo ya uasi na changamoto nyingine za kiusalama. 

Akizungumza wakati wa mapokezi ya Wanajeshi hao Balozi Bana ameongeza kusema ushiriki wa Tanzania katika michezo hiyo kutasaidia kuimarisha na kuongeza ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo kubadilishana taarifa katika eneo la ulinzi na usalama na nchi zingine za Afrika

“Wakati huu dunia inapokabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama ni muhimu pia kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuendelea kuimarisha mahusiano na vyombo vingine vya nje ya nchi ili kwa pamoja kuweza kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hizo.” Balozi Bana. 

Michezo hiyo ilifunguliwa Oktoba 11, 2021 jijini Abuja, na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Mhe. Dkt. Ogbonanya Onu wa Serikali ya Shirikisho la Nigeria. Katika ufunguzi Dkt. Onu alibainisha kuwa michezo hiyo ni muhimu kwa sasa kwa kuzingatia hali ya usalama ya sasa inayokabili taifa hilo.

Michezo hiyo inatarajiwa kuudhuliwa na washiriki takribani 327 kutoka nchi 14 zikiwemo Nigeria, Burkina Faso, Cameroon, Congo Brazzaville, Guinea Conakry, Kenya, Mali, Tanzania na Chad. Michezo mingine itakayofanyika ni mpira wa miguu na gofu.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wanariadha wa JWTZ wanaoshiriki michezo ya Amani na Mshikamano ya Kijeshi ya Sahel Barani Afrika



Chuo Kikuu cha Port Harcourt cha nchini Nigeria chaonesha nia ya kufundisha Lugha ya Kiswahili
Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Mhe. Benson Alfred Bana ameeleza kuwa Chuo Kikuu cha Port Harcourt kimeonesha utayari wa kuanza kufundisha tena somo la lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Slaam kama ilivyokuwa halo awali. 

Balozi Bana amebainisha hayo baada ya kutembelea na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Chuo cha Port Harcourt Prof. Owunari Abraham Georgewill, ambapo pamoja na masuala mengine walijadili kuhusu uwezekano na namna ya kuanza kufundisha somo la Kiswahili katika Chuo hicho.

“Taratibu zimeanza kufanyika ili kukamilisha makubaliano ambayo yatapelekea somo la Kiswahili kufundishwa chuoni hapo, hii itatoa fursa kwa Walimu wa Kiswahili wa Tanzania kufundisha somo hilo katika chuo hicho, pia ni fusa muhimu katika kukuza lugha ya Kiswahili ambayo ni sehemu ya Utamaduni wa Mtanzania” Amesema Balozi Bana.

Miongo minne iliyopita Chuo kikuu cha Port Harcourt kilikuwa kikifundisha somo la Lugha ya Kiswahili. Hata hivyo kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi, Chuo hicho hakikuendelea kufundisha somo hilo. 

Tuesday, October 12, 2021

EALA WAKUTANA MKUTANO WA KWANZA JIJINI ARUSHA

Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala) limeanza leo mkutano wake wa kwanza, kikao cha tano, bunge la nne ambapo pamoja na mambo mengine, Bunge hilo limejadili masuala mbalimbali ya kamati ya sheria na maendeleo yake ndani ya Jumuiya hiyo.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) Mhe. Martin Ngoga akifungua Mkutano wa Kwanza, Kikao cha tano, Bunge la nne ulioanza leo Jijini Arusha


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) pamoja na wabunge wengine wa Bunge hilo wakifuatilia Mkutano kwanza wa (Eala), leo Jijini Arusha


Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Mhe. Wanjiku Muhya kutoka Kenya akichangia hoja kuhusu Kamati ya Sheria katika Mkutano Kwanza leo Jijini Arusha


Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Mhe. Gasinzigwa Oda kutoka Rwanda akichangia hoja kuhusu Kamati ya Sheria katika Mkutano Kwanza leo Jijini Arusha


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akinukuu jambo wakati wa Mkutano Kwanza wa (Eala), ukiendelea leo Jijini Arusha


Mbunge wa Eala kutoka Sudan Kusini Mhe. Mukulia Kennedy Ayason  akichangia hoja kuhusu Kamati ya Sheria katika Mkutano Kwanza leo Jijini Arusha


Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kanda wa Kenya, Adan Mohamed (kulia) akijadili jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) nje ya Ukumbi wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala), mara baada ya kuahirishwa kwa Mkutano wa Kwanza, Kikao cha tano, Bunge la nne, ulioanza leo Jijini Arusha



Monday, October 11, 2021

TANZANIA YAPONGEZWA KUFANIKISHA MAONESHO YA UTALII UKANDA WA AFRIKA MASHARIKI

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongezwa kwa kufanikisha maonsho ya kwanza ya kitaifa ya kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 9 – 11 yaliyolenga kutangaza vivutio na fursa mbalimbali za utalii ndani ya Jumuiya hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na baadhi ya Mawaziri wa Utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa kufunga maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo jijini Arusha.

“Nawapongeza kwa kufanikisha maonesho haya ni imani yangu kuwa kupitia maonesho haya nchi zetu za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepata fursa ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na kujadili njia mbalimbali za kukabiliana changamoto zinazoikabili sekta ya Utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki,” Amesema Dkt. Mwinyi

“Natoa wito kupitia maonesho haya ambayo yatakuwa yanafanyika kila mwaka kwa mzunguko kwa kila nchi mwanachama……..jitihada zaidi zinahitajika katika kutangaza vivutio vya utalii katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuboresha sera zetu za utalii,” ameongeza Dkt. Mwinyi

Dkt. Mwinyi pia ameitaka Kamati Maalumu ya Kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya ziara Zanzibar na kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya utalii pamoja na zile za biashara na uwekezaji.

Awali Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kupitia maonesho haya ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki yamekuwa na mafanikio makubwa ambapo zaidi ya waoneshaji 100 kutoka mataifa mbalimbali duniani wameshiriki, kati yao 41 wakitoka mataifa mbalimbali na nchi 25 zikishiriki ikiwa ni pamoja na sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Nae Waziri wa Uhifadhi wa Wanyamapori na Utalii kutoka Sudan ya Kusini Mhe. Luteni Jenerali Rizik Zakaria Hassan ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha maonesho ambayo yemeweza kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki ambayo pia yametoa fursa ya kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya utalii.

“Maonesho haya yemekuwa na manufaa makubwa sana kwa kutuweka sekta ya utalii ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki ……….binafsi nawapongeza sana Tanzania kwa kulifanikisha jambo hili muhimu kwetu, naamini kupitia maonesho haya tutazidi kuimarika ziadi kama jumuiya kwa maendeleo yetu sote,” Amesema Luteni Jenerali Hassan.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Forodha na Biashara Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bwn. Keneth Bagamuhunda ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki, amesema maonesho yalilenga kutoa fursa kwa kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii ili kuifahamisha Afrika na Dunia kuwa ndani ya Afrika Mashariki kuna vivutio vya utalii.

“Tutaendelea na maonesho haya kwa kila mwaka lengo likiwa ni kutangaza utalii na kuhakikisha soko la utalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linakuwa kila mwaka,” Amesema Bwn. Bagamuhanda.

Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Malikale wa Zanzibar, Mhe. Leila Mohamed Mussa (Mb) amesema Afrika kwa sasa inatakiwa fursa za utalii na biashara ili kuweza kuziongezea Serikali zetu mapato.

“Afrika Mashariki inayo mambo mengi ya kutoa katika bara la Afrika na Duniani kwa ujumla hasa katika sekta ya utalii kwa kuwa tumejaliwa vivutio mbalimbali vya utalii,” amesema Bibi Leila Mohamed Mussa.

Oktoba 09, 2021 maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki yalizinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki jijini Arusha.

Kufanyika kwa maonesho hayo kunatokana na kuzinduliwa hivi karibuni mpango wa pamoja kutangaza utalii katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliozinduliwa rasmi na Mawaziri wa Maliasili na Utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Maonesho hayo yalihudhuriwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania (Mwenyeji), Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia washiriki wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, leo Jijini Arusha


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akipata maelezo wakati alipotembelea banda la Rwanda katika maonesho ya kwanza ya Kikanda ya Utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akikaribishwa na Balozi wa Kenya nchini Tanzania katika banda la Kenya wakati alipokuwa akitembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, leo Jijini Arusha


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Mkewe Mhe. Mama Mariam Mwinyi na viongozi mbalimbali katika banda la Zanzibar leo Jijini Arusha

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro wakifungua na kuweka jiwe la msingi la kwanza la maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki, leo Jijini Arusha


Kikundi cha ngoma kutoka Makumira Arusha kikitumbuiza wakati wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha


Kikundi cha ngoma kutoka Sudan Kusini kikitumbuiza wakati wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali mara baada ya kufunga maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha


Sekta zaidi nchini kunufaika na mikopo nafuu ya Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas A. Nyamanga akiwa katika mazungumzo na Mkuu wa ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya. 
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas A. Nyamanga wakikabidhiana zawadi baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya. 

-------------------------------------------

Sekta zaidi nchini kunufaika na mikopo nafuu ya Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya

Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (European Investment Bank-EIB) imekubali kuongeza kasi na wigo wa maeneo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Benki hiyo. Hayo yameelezwa wakati wa mazungumzo baina ya Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Luxembourg na kwenye Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas A. Nyamanga na Mkuu wa ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa benki hiyo, Bw. Diederick Zambon yaliyofanyika hivi karibuni kwenye Ubalozi wa Tanzania, Brussels. 

Katika mazungumzo hayo, wawili hao walijadili kwa kina juu ya miradi mbalimbali na fursa nyingine zinazoweza kunufaisha Tanzania kupitia mikopo nafuu inayotolewa na Benki hiyo. Miongoni mwa miradi iliyojadiliwa ni pamoja na ujenzi wa awamu ya pili ya mradi wa kuboresha msongo mkubwa wa umeme katika vituo vya Iringa na Shinyanga (Tanzania Electricity Backboneinterconnector project-TBIP II. EIB ilikuwa ni moja ya taasisi za fedha zilizotoa mkopo nafuu kwa ajili ya mradi huu kwa awamu ya kwanza (TBIP I). Katika mazungumzo hayo, Bw. Zambon ameonesha utayari wa kuendeleza mazungumzo zaidi na Serikali ya Tanzania kuhusu mradi huu na miradi mingine ikiwemo miradi ya maji.

Wawili hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi kwenye utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa viwanja vya ndege vya Tabora, Shinyanga na Kigoma pamoja na ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Sumbawanga. Mradi huu pia unafadhiliwa na Benki ya EIB kwa mkopo nafuu wa Euro milioni 50.

Benki hiyo yenye makao yake makuu nchini Luxembourg pia imekubali kuanza majadiliano na Serikali ya Tanzania pamoja na sekta binafsi ili kukubaliana juu ya mazingira yatakayoiwezesha Benki hiyo kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa sekta binafsi ili kuchochea zaidi maendeleo ya Watanzania. Mikopo hiyo italenga zaidi wajasiriamali wadogo na wakati; wakulima na watanzania wenye viwanda vinavyoongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo; taasisi mbalimbali za fedha na wafanyabiashara kwa ujumla.

Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Bw. Zambon unatarajiwa kufanya ziara nchini Tanzania mwezi huu wa Oktoba au mwanzoni mwa Mwezi Novemba mwaka huu kwa ajili ya kuendeleza majadiliano na Serikali pamoja na sekta binafsi kwenye masuala haya muhimu kwa uchumi wa Tanzania.

EIB ni miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo wa Tanzania na imekuwa ikishirikiana na Serikali na sekta binafsi katika utoaji wa mikopo nafuu kwa miradi mbalimbali nchini.