Friday, November 5, 2021

TANZANIA, NORWAY KUONGEZA USHIRIKIANO

 Tanzania na Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za nishati, utunzaji wa mazingira na matumizi bora ya ardhi.

Mkubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili maeneo ambayo NORAD imeonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika kusaidia kuyaendeleza na kuyaboresha kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.   

Maeneo waliyokubaliana ni nishati jadidifu, umeme vijijni, gesi asilia, elimu, matumizi bora ya ardhi, kusaidia kaya masikini, maji safi na salama, utunzaji wa mazingira na kuzuia ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya mkaa na kuni pamoja na uchumi wa buluu.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Sokoine amemhakikishia Mkurugenzi wa NORAD Bw. Solhjell kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea na jitihada za kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa uhakika kwa kuendelea na ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere, gesi asilia, nishati jadidifu na umeme wa jua ili kupunguza uharibifu wa mazingira kutokana na kushamiri kwa matumizi ya kuni na mkaa.

Norway imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta za maendeleo tangu mwaka 1964, baadhi ya maeneo ambayo nchi hizo zimekuwa zikishirikiana ni pamoja na uzalishaji wa nishati ya umeme hususan vijijini, afya, elimu, kilimo na utunzaji wa misitu. 

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akizungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell akimueleza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia kwa Mkurugenzi wa NORAD ni Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elisabeth Jacobsen.


Kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell kikiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto kwa Balozi Sokoine ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akifuatilia mazungumzo hayo.


Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Elisabeth Jacobsen akielezea jambo wakati wa kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la NORAD Bw. Bard Vegar Solhjell kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam


 


Thursday, November 4, 2021

MKUTANO WA MAKATIBU WAKUU WANAOSHUGHULIKIA MASUALA YA AFRIKA MASHARIKI NA MIPANGO KATIKA NCHI ZA EAC UNAFANYIKA JIJINI ARUSHA

Mkutano wa Makatibu Wakuu wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika jijini Arusha, Tanzania tarehe 4 Novemba 2021.

Mkutano huu na mkutano wa ngazi ya wataalamu uliofanyika tarehe 1 na 2 Novemba 2021 ni sehemu ya mikutano ya awali kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa 32 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango utakaofanyika jijini Arusha tarehe 5 Novemba 2021.

Mikutano hii ya awali pamoja na mambo mengine ina jukumu la kupitia na kuwasilisha agenda na mapendekezo ya masuala mengine ya kikanda yatakayojadiliwa katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano wa Makatibu Wakuu unaongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine.

Viongozi wengine walioambatana na Dkt. Ndumbaro katika mkutano huo ni pamoja na; Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa, Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Harshil Adballah, na Afisa Mtendaji Mkuu, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Bw. Nicodemus Mkama.


Mwenyekiti wa Mkutano wa Makatibu Wakuu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Kenya, Mhe. Dkt. Kevit Desai (wa pili kushoto) akiongoza Mkutano wa Makatibu Wakuu unaofanyika jijini Arusha tarehe 4 Novemba 2021 kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa 32 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango utakaofanyika jijini Arusha tarehe 5 Novemba 2021.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro (kulia) akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Makatibu Wakuu wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango katika Nchi za Afrika Mashariki, Kushoto ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa.

Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Harshil Adballah, na Afisa Mtendaji Mkuu, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Bw. Nicodemus Mkama wakifuatilia mkutano.

Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi na Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Sera Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi Agnes Meena wakifuatilia mkutano.

Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Justin Kisoka na Afisa Biashara Mkuu katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Abdul Chacha wakifuatilia mkutano. 

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano.

Ujumbe wa Burundi

Ujumbe wa Kenya

Ujumbe wa Uganda