Wednesday, November 10, 2021

BALOZI SOKOINE AKUTANA NA KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NJE WA SLOVENIA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Slovenia Balozi Jozef  Drofenik walipokutana katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Slovenia Balozi Jozef Drofenik akizungumza alipokutana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Slovenia Balozi  Jozef Drofenik yakiendelea .



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Slovenia Balozi Jozef Drofenik (kushoto) na  Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria na Manunuzi ya Umma Wizara ya Mambo ya Nje ya Slovenia Bw. Gregor Pelicon walipokutana katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Slovenia Balozi Jozef Drofenik walipokutana katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.  

   


 

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine amekutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Slovenia Balozi  JOZEF DROFENIK katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Slovenia ambao umekuwepo kwa miaka mingi kwa maslahi ya nchi zote mbili.

Akizungumza katika kikao hicho Balozi Sokoine ameihakikishia Slovenia kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya nchi hiyo na kuahidi kuongeza ushirikiano kwa ajili ya kukuza na kuimarisha uhusiano wa kirafiki uliopo baina ya nchi hizo. Balozi Sokoine ametumia nafasi hiyo kuwaita na kuwaalika wawekezaji, wafanya biashara na watalii kutoka nchini humo kuja Tanzania ili kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji na utalii zinazopatikana nchini.

Naye Balozi  Jozef Drofenik kutoka Jamhuri ya Slovenia ameihakikishia Serikali ya Tanzania utayari wa nchi yake kuendelea kushirikiana na Tanzania na kufanya kazi kwa pamoja na kuialika kushiriki katika Jukwaa la Slovenia na nchi za Afrika litakalofanyika mwakani  ambalo amesema ni nchi chache za Afrika hualikwa kushiriki . Balozi Jozef Drofenik  amewakaribisha Watanzania kwenda Slovenia na maandiko ya miradi mbalimbali ili kuwekeza nchini humo na kuongeza kuwa watakuwa tayari kuwapokea na kufanya nao kazi kwa pamoja. 

Viongozi hao wamekubaliana kuangalia namna ya kuendelea kuimarisha  ushirikiano wa nchi zao na kuona kama Slovenia itakuwa tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya biashara, uwekezaji na uchumi, utalii, utengenezaji dawa, elimu, kilimo, uhandisii wa misitu ili kuhifadhi misitu , sayansi na teknolojia , uchumi wa buluu ili kuwa na uvuvi endelevu na matumizi bora ya rasilimali za majini na eneo la mafuta na gesi.

Tuesday, November 9, 2021

SERIKALI YAWAHIMIZA DIASPORA WA TANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI ZILIZOPO NCHINI

Mkutano wa kujadili mapendekezo ya miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaoishi nje (Diaspora) umefanyika  kwa njia ya mtandao leo tarehe 09 Novemba 2021 ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu “Umuhimu wa Diplomasia ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa katika Kuwaletea Wananchi Maendeleo uliofanyika tarehe 06 Novemba 2021.

Mkutano huo ambao umeratibiwa na kuongozwa na  Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka umepokea mapendekezo ya miradi 12 iliyowasilishwa na  Watanzania hao ambao ni Bw. Hassan Ng’anzo wa Norway, Dkt. Swabury Alawi wa Ujerumani na Bw. Patrick Dyauli wa Uingereza.

Wakiwasilisha mapendekezo ya miradi hiyo ambayo imejikita kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za Afya, Mazingira, Nishati, Madini, Ujenzi na Uchukuzi, Watanzania hao ambao pia ni wamiliki wa Kampuni za ANICO, ESSB na SE Holdings, wameiomba Serikali kuwapatia ushirikiano wa kutosha ili kuwezesha miradi hiyo ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji wa uhakika, kuja nchini kwani ina manufaa makubwa kiuchumi na itatengeza ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wake, Balozi Rutageruka amewashukuru na kuwapongeza Watanzania hao kwa hatua hiyo ya kizalendo ya kuwa tayari kuja kuwekeza nchini na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano watakaohitaji ili kufanikisha lengo hilo. Kadhalika, amewahimiza Diaspora wengine kujitokeza kwa wingi kuja kuwekeza au kuleta wawekezaji na wafanyabiashara wenye tija nchini.

Mkutano huo pia umewashirikisha wadau muhimu zaidi ya 20 kutoka ndani na nje ya nchi akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. John Simbachawene, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahamoud Thabit Kombo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diapora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago, Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Sweden na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.

Wadau wengine walioshiriki ni kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, TIC, ZIPA na TANTRADE.

Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka akichangia jambo wakati wa Mkutano wa kujadili mapendekezo ya  miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaioshi nje (Diapora) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 09 Novemba 2021. Kulia anayesikiliza ni Bw. Hassan Ng'anzo, Mtanzania anayeishi Norway ambaye aliwasilisha mapendekezo ya miradi ambayo wapo tayari kuja kuwekeza nchini. Miradi hiyo imejikita katika sekta mbalimbali kama vile afya, nishati, madini, mawasiliano na ujenzi na uchukuzi
Balozi Rutageruka akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Dkt. Abdallah Possi wakati akizungumza kwenye mkutano wa kujadili mapendekezo ya  miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaioshi nje (Diapora)
Balozi Rutageruka akimsikiliza Dkt. Swabury Alawi, Mtanzania anayeishi Ujerumani wakati wa mkutano wa kujadili mapendekezo ya  miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaioshi nje (Diapora)
                              
Balozi Rutageruka akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diapora cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago  wakati akichangia hoja kwenye mkutano wa kujadili mapendekezo ya  miradi ya uwekezaji kutoka kwa Watanzania wanaioshi nje (Diapora)

Mkutano ukiendelea huku Maafisa kutoka Idara ya Diplomasia ya Uchumi, Bw. Magabilo Murobi (kulia) na Bw. Herman Berege (kushoto) wakinukuu masuala muhimu yanayojadiliwa.



 













Prof. Mbennah awasilisha Hati za Utambulisho nchini Mauritius

Balozi wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake Harare, Zimbabwe, Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah akingia Ikulu ya Port Louis kwa ajili ya kuwasilisha Hati za Utambulisho
Balozi wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake Harare, Zimbabwe, Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah akisalimiana na Rais wa Mauritius, Mhe. Prithvirajsing Roopun kwenye Ikulu ya Port Louis kabla ya kuwasilisha Hati za Utambulisho.

Balozi wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake Harare, Zimbabwe akisaini kitabu cha wageni kwenye Ikulu ya Port Louis.

Balozi wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake Harare, Zimbabwe, Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Mauritius, Mhe. Prithvirajsing Roopun kwenye Ikulu ya Port Louis.

Balozi wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake Harare, Zimbabwe, Mhe. Prof. Emmanuel Mbennah akiwa katika mazungumzo na Rais wa Mauritius, Mhe. Prithvirajsing Roopun kwenye Ikulu ya Port Louis. Wawili hao walijadili masuala ya ushirikiano baina ya Tanzania na Mauritius hususan katika sekta ya uwekezaji na biashara.

Sunday, November 7, 2021

MAADHIMISHO YA MIAKA 107 YA VITA YA KWANZA NA MIAKA 76 YA VITA VYA PILI VYA DUNIA

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisoma hotuba yake wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 107 tangu kumalizika kwa vita ya kwanza ya dunia na miaka 76 tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia. Maadhimisho hayo yamefanyika katika makaburi ya Mashujaa yaliyoko eneo la Kijitonyama Jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Uingereza Nchini Mhe. David Concar akisoma hotuba yake katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 107 tangu kumalizika kwa vita ya kwanza ya dunia na miaka 76 tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia. Maadhimisho hayo yamefanyika katika makaburi ya Mashujaa yaliyoko eneo la Kijitonyama Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (katikati) pamoja na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar na baadhi ya Mabalozi kutika nchi za Jumuiya ya Madola wakifuatilia kumbukizi ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 107 tangu kumalizika kwa vita ya kwanza ya dunia na miaka 76 tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia 

Viongozi na wananchi wakifuatilia kumbukizi ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 107 tangu kumalizika kwa vita ya kwanza ya dunia na miaka 76 tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb), Balozi wa Uingereza Nchini, Mhe. David Concar pamoja na Balozi wa Ujerumani Nchini, Mhe. Regina Hess wakienda kuweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu wa mashujaa wa vita ya kwanza ya dunia na ya pili ya dunia katika makaburi ya Mashujaa yaliyoko eneo la Kijitonyama Jijini Dar es Salaam 

Balozi wa Canada Nchini, Mhe. Pamela O’Donnel pamoja na Balozi wa Pakistan Nchini, Mhe. Muhammad Saleem wakienda kuweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu wa mashujaa wa vita ya kwanza ya dunia na ya pili ya dunia katika makaburi ya Mashujaa yaliyoko eneo la Kijitonyama Jijini Dar es Salaam 

Balozi wa Marekani Nchini, Mhe. Donald Wright pamoja na baadhi viongozi wakitoa heshima mara baada ya kuweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu wa mashujaa wa vita ya kwanza ya dunia na ya pili ya dunia katika makaburi ya Mashujaa yaliyoko eneo la Kijitonyama Jijini Dar es Salaam 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, Balozi wa Uingereza Nchini, Mhe. David Concar pamoja na Balozi wa Ujerumani Nchini, Mhe. Regina Hess wakiweka shada la maua katika mnara wa askari ulioko Posta Jijini Dar es Salaam ikiwa ni maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 107 tangu kumalizika kwa vita ya kwanza ya dunia na miaka 76 tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 107 tangu kumalizika kwa vita ya kwanza ya dunia na miaka 76 tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia
















Saturday, November 6, 2021

TANZANIA KUENDELEA KUTEKELEZA DIPLOMASIA YA UCHUMI KATIKA KUJILETEA MAENDELEO

Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi ili kuliletea Taifa maendeleo ya kiuchumi kupitia mahusiano na nchi mbalimbali, mashirika ya kikanda na kimataifa.

Balozi Rutagaruka  ametoa wito huo  leo tarehe 06 Novemba 2021 wakati wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu “Umuhimu wa Diplomasia ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa katika Kuwaletea Wananchi Maendeleo” uliofanyika kwa njia ya mtandao na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wabunge, Mabalozi na Wanadiaspora.

Akizungumza kwenye Mdahalo huo akiwa jijini Dodoma, Balozi Rutageruka amesema kuwa, upo umuhimu mkubwa kwa Tanzania kuendelea kuimarisha mahusiano yake na nchi mbalimbali na mashirika ya kikanda na kimataifa ili inufaike kiuchumi kupitia fursa lukuki zilizopo nchini kama vivutio vya Utalii, fursa za Uwekezaji na Biashara pamoja na kuhakikisha wadau wote  zikiwemo Taasisi za Umma na Binafsi, Mabalozi na Wananchi kwa ujumla wanashiriki kikamilifu katika kutekeleza mikakati mbalimbali  iliyopo ili kufikia malengo kusudiwa kupitia Diplomasia ya Uchumi.

Ameongeza kusema kuwa, tayari mafanikio mengi yamepatikana kupitia utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ikiwemo kuimarika kwa Sekta za Uchumi ambapo tayari mikataba kadhaa ya manufaa kwa nchi imesainiwa ukiwemo ule wa Serikali ya Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kampuni ya Mafuta Ghafi ya Afrika Mashariki (EACOP) itakayohusika na Ujenzi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga. Mafanikio mengine ni kuondolewa kwa vikwazo 46 kati ya 64 vya muda mrefu visivyo vya kiforodha kati ya Tanzania na Kenya. Vikwazo hivi vimeondolewa kufuatia ziara ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kenya mwezi Mei 2021.

Kadhalika amesema kuwa, Tanzania imeimarisha ushiriki wake katika masuala ya kikanda na kimataifa na kwamba mwezi Septemba 2021 Tanzania iliridhia Mkataba wa kuanzisha Eneo Huru la Biashara Barani Afrika na kwamba kuridhiwa kwa mkataba huu kumeongeza ushawishi wa Tanzania katika mtangamano wa Afrika na kuwa sehemu ya soko kubwa la Afrika lenye idadi ya watu wapatao bilioni 1.3. Aliainisha maeneo mengine ya mafanikio kuwa ni pamoja na kukua kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili na ufunguzi wa Balozi na Konseli Kuu ambapo hadi sasa Tanazania inazo Balozi 44 na Konseli Kuu 6.

Mbali na mafanikio hayo,  Balozi Rutageruka amesema Serikali itaendelea kutekeleza kikamilifu mikakati iliyopo ya kutekeleza Diplomasia ya Uchumi ikiwa ni pamoja na kuvutia utalii, uwekezaji na biashara kwa kutumia maonesho na makongamano; kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa; kutafuta fursa za masomo na ufadhili; kubadilishana ujuzi katika nyanja mbalimbali kati ya Taasisi za Tanzania na Taasisi nyingine nje ya nchi na kutumia Balozi za Tanzania katika kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini  Korea ya Kusini, Mhe. Togolani Mavura ambaye wakati wa mdahalo huo alizungumzia umuhimu wa Diplomasia amesema ni muhimu kwa Tanzania kuendelea kuwekeza kwenye Diplomasia hususan kuimarisha ushirikiano na nchi zingine ili kuepusha migogoro ambayo husababisha nchi kupoteza mwelekeo na badala ya kuokoa fedha kwa ajili ya huduma muhimu za jamii kama maji, afya na umeme nchi zinajikuta zinawekeza kwenye masuala ya migogoro na vita ambayo hugharimu fedha nyingi.

Naye Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi, Mhe. Hoyce Temu amesema Tanzania chini ya Utawala wa Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kung’aa kimataifa na kwamba mashirika mbalimbali ya kimataifa yameonesha nia ya kuisaidia Tanzania kufikia malengo yake hususan kwenye agenda mbalimbali ikiwemo ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030.

Akichangia hoja wakati wa mdahalo huo, Bi. Loveness Mamuya ambaye ni Mtanzania anayeishi Marekani amesema Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nje (Diaspora) ipo tayari kushirikiana na Serikali katika kuchangia maendeleo ya nchi na kutoa rai kwa Serikali kuwashirikisha kikamilifu Diapora kwenye mipango mbalimbali ikiwemo kutafuta wawekezaji na wafanyabiashara wa uhakika kutoka kwenye maeneo waliyopo.

Mdahalo huo ambao umeandaliwa na Taasisi ya Watch Tanzania na kuwashirikisha wazungumzaji mbalimbali umeongozwa na Dkt. Hezron Makundi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Diplomasia ya Uchumi ni Mkakati wa nchi kushirikiana na mataifa mengine, mashirika au taasisi za kimataifa kujinufaisha kiuchumi kupitia biashara, uwekezaji, utalii na teknolojia.


Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka akizungumza wakati wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu "Umuhimu wa Diplomasia ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa katika kuwaletea Wananchi Maendeleo". Mdahalo huo ambao umeandaliwa na Taasisi ya Watch Tanzania umefanyika kwa njia ya mtandao tarehe 06 Novemba 2021 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Mabalozi, Wanadiaspora, Wahadhiri na Wabunge. 
Balozi Rutageruka akimsikiliza Mbunge wa Mtama, Mhe. Nape Nnauye alipokuwa anachangia hoja wakati wa mdahalo  huo

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi, Mhe. Hoyce Temu naye akizungumza wakati wa mdahalo wa kitaifa kuhusu Diplomasia ya Uchumi

Balozi wa Tanzania nchini Korea ya Kusini, Mhe. Togolani Mavura akizungumza wakati wa mdahalo huo

Mtanzania anayeishi Marekani Bi. Loveness Mamuya naye akichangia jambo wakati wa mdahalo kuhusu Diplomasia ya Uchumi huku Balozi Rutageruka akimsikiliza 



 

Friday, November 5, 2021

MAWAZIRI WANAOSHUGHULIKIA MASUALA YA AFRIKA MASHARIKI NA MIPANGO WA NCHI ZA EAC WAKUTANA JIJINI ARUSHA

Mkutano wa 32 wa Baraza la Mawaziri la kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango umefanyika leo tarehe 05 Novemba, 2021 jijini Arusha, Tanzania.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ambaye ameambatana na; Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohammed Mchengerwa, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda- Zanzibar  Mhe. Omar Said Shaaban, na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe. 

Viongozi wengine walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na; Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum; na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Harshil Abdallah, na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa,.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri pamoja na masuala mengine umejadili na kutoa maamuzi mbalimbali ya kisera katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Baadhi ya agenda zilizojadiliwa ni; Taarifa ya utekelezaji wa maamuzi na maelekezo yaliyopita ya Baraza la Mawaziri la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango; Hali ya ulipaji wa michango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Nchi Wanachama; Mapendekezo ya maeneo ya vipaumbele vya jumla na mahsusi vya Jumuiya kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023; na taarifa ya kadi ya alama (score card) ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2020. 

Agenda nyingine ni pamoja na; Taarifa ya andiko la Mkutano wa Kazi (high level retreat) wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu hali iliyofikiwa katika kuondoa Vikwazo Vya Kibiashara Visivyo Vya Kikodi (NTBs) katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; na Mapitio ya Sheria ya Uondoshaji Vikwazo Vya Kibiashara Visivyo Vya Kikodi (NTBs) ya Kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Ukamilishwaji wa Kanuni za utekelezaji wa Mkataba.

Mkutano wa 32 wa Baraza la Mawaziri la kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango umefanyika ana kwa ana na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kenya, Jamhuri ya Burundi, na Jamhuri ya Uganda. Wajumbe wengine kutoka Jamhuri ya Rwanda na Jamhuri ya Sudan Kusini wameshiriki kwa njia ya mtandao.

======================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akishiriki Mkutano wa 32 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango uliofanyika leo tarehe 05 Novemba 2021 jijini Arusha, Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb)(Kati) akiongoza kikao cha ndani katika ngazi ya Mawaziri.
Kushoto ni Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
 Mhe. Mohammed Mchengerwa, na kutoka kulia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda- Zanzibar  Mhe. Omar Said Shaaban  na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe
. 


Mwenyekiti wa Mkutano wa Mawaziri ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda wa Kenya, Mhe. Adan Mohammed (kati) akifungua rasmi Mkutano wa 32 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango uliofanyika jijini Arusha tarehe tarehe 5 Novemba 2021. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Dkt. Peter Mathuki.

Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda - Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum.

Kutoka kulia ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa na Mkurugenzi Idara ya Ulinzi, Siasa na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi.

Ujumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Sehemu nyingine ya ujumbe kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Pamoja na Mhe. Balozi Mulamula ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndenjembi (kushoto) na Naibu Waziri, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe. 

Ujumbe kutoka Jamhuri ya Burundi

Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kenya

Ujumbe kutoka Jamhuri ya Uganda