Wednesday, March 2, 2022

TANZANIA IRELAND KUENDELEZA USHIRIKIANO

 

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick zilizofanyika nyumbani kwa Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini.


 

Balozi wa Ireland nchini Mhe. Mary O’Neil akizungumza wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick zilizofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.


 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki , Balozi Swahiba Mndeme (kulia) wakimsikiliza Balozi wa Ireland nchini Mhe. Mary O’Neil  akizungumza wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick zilizofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Comoro na  Mkuu wa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini Mhe.Ahmada El Badaoui Mohamed Fakih wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick zilizofanyika nyumbani kwa Balozi wa Ireland jijini Dar es Salaam.


Balozi wa Kenya nchini  Mhe. Dan Kazungu (katikati) akijadili jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) walipokutana nyumbani kwa Balozi wa Ireland nchini Mhe. Mary O’Neil kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick ambayo huadhimishwa nchini humo tarehe 17 Machi ya kila mwaka .


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell  wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick zilizofanyika nyumbani kwa Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini (kulia) akiwaangalia.


Baadhi  ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania walioshiriki sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick zilizofanyika nyumbani kwa Balozi wa Jamhuri ya Ireland jijini Dar es Salaam.



 

Tanzania na Ireland zimeahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo kwa manuufaa ya pande zote mbili

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ametoa ahadi hiyo aliposhiriki katika maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick ambayo huadhimishwa na Jamhuri ya Ireland tarehe 17 ya kila mwaka.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku hiyo Waziri wa Mulamula ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Ireland kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo wa Tanzania hasa katika Nyanja za kusaidia kaya masikini, elimu na kuwajengea uwezo wanawake na watoto wa kike nchini.

Amesema Serikali inathamini mchango wa Ireland kwa Tanzania na kusisitiza kuwa itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo ili kufikia maendeleo ya kweli kwa pamoja.

Naye Balozi wa Ireland nchini Mhe. Mary O’Neil ameahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada za kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Ireland na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa faida ya wananchi wa nchi zote.

Maadhimisho ya siku hiyo yamezinduliwa rasmi leo Tarehe 02 Machi 2022 jijini Dar es Salaam katika makazi ya Balozi wa Ireland nchini na kuhudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa wanaoziwakilisha nchi na Mashirika yao hapa nchini.

Siku ya Mtakatifu Patrick huadhimishwa kila ifikapo tarehe 17 Machi nchini Ireland kuadhimisha kuwasili kwa ukristo nchini humo na kusherehekea urithi wa utamaduni wa watu wa Ireland kwa ujumla.

 

 

 

RAIS WA TCCIA NCHINI AFANYA ZIARA YA KIKAZI OMAN


Rais wa Chama Cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul Faraji Koyi,  amefanya ziara ya kikazi nchini Oman hivi karibuni.  Akiwa nchini Oman amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na wenye Viwanda ya Oman, Mhandisi Redha Jumaa Al Saleh.


Katika mazungumzo yao, ambayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo kukuza biashara na uwekezaji baina ya pande hizo mbili ili kuzitumia kikamilifu fursa nyingi za kiuchumi zinazopatikana katika nchi hizi mbili na hatimaye kukuza kiwango cha biashara kati ya nchi hizi ambacho kwa sasa kinaonekana bado kipo chini.


Wakati wa mazungumzo hayo, Bw. Koyi aliueleza ujumbe wa Oman kuwa, zipo fursa nyingi nchini Tanzania ambazo Oman inaweza kunufaika nazo zikiwemo za uwekezaji wa Viwanda vya kuchakata mazao ya Kilimo, Utalii, Uzalishaji Umeme, Kilimo, Ujenzi wa nyumba na sekta ya usafirishaji wa anga na baharini. Kadhalika aliwajulisha kuwa, Serikali ya Tanzania inachukua hatua mbalimbali za kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, reli na viwanja vya ndege Ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara.

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Oman, Mhandisi Al Saleh aliwaeleza wajumbe kuwa, nchi hiyo imefungua milango ya uwekezaji katika Maeneo Huru ya Uwekezaji (EPZ) ya Salala, Duqm na Sohar. Aidha, Serikali ya Oman imetoa fursa kwa wawekezaji kutoka nje kutolazimika kuwa na ubia na mwekezaji mwenyeji.


Akizungumzia suluhisho la changamoto za ufanyaji biashara kati ya Tanzania na Oman, Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdalah Kilima amesema tayari Ubalozi huo umewasilisha pendekezo hapa nchini la kuanzisha safari za ndege ya mizigo kwenda Oman kupitia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL). Pia Ubalozi umezungumza na mashirika ya meli nchini Oman ili kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya nchi hizi mbili

Wakati huohuo, Ujumbe wa Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima ya Tanzania walikutana na Viongozi wa Baraza la Biashara kati ya Oman na Tanzania wa upande wa Oman ambapo walikubaliana kufufua mikakati ya ushirikiano kupitia Kampuni ya Uwekezaji ya Oman na Tanzania (OTIC) iliyoanzishwa mwaka 2016.

Mbali na kushiriki mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Oman, Ujumbe wa TCCIA ulifanya ziara katika Kiwanda cha Taifa cha Chai cha Oman, wazalishaji wa chai ya MUMTAZ jijini Muscat na kupata maelezo ya utendaji wa kiwanda hicho ambapo pamoja na mambo mengine, Kampuni hiyo imeahidi kufuatilia fursa zilizopo nchini, ikiwemo upatikanaji wa chai.

Kwenye ziara hiyo, Rais wa TCCIA nchini alifuatana na Bw. Abdul Mwilima, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoa wa Kigoma; Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Nerbat Mwapele na Afisa Masoko Mwandamizi, Bi. Fatma Khamis.

 Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul Faraji Koyi (mwenye barakoa nyeupe) akiwa kwenye mazungumzo na  Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na wenye Viwanda ya Oman, Mhandisi Redha Jumaa Al Saleh (wa kwanza kulia).  Bw. Koyi alikuwa nchini Oman kwa ziara ya kikazi ya kuimarisha ushirikiano kati ya TCCIA na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Oman. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima (mwenye suti nyeusi).

Viongozi wa Jumuiya za Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima ( wa nne kushoto) mara baada ya mazunungumzo  ya kuimarisha ushirikiano wa Taasisi zao.

Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA) akiwa kwenye mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni ya Uwekezaji ya Oman na Tanzania (OTIC). Bw. Koyi alikuwa nchini Oman kwa ziara ya kikazi ya kuimarisha ushirikiano kati ya TCCIA na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Oman.

Mhe. Balozi Kilima (wa pili kushoto) akiwa na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul Faraji Koyi (kushoto) walipotembelea kiwanda cha Chai cha Taifa cha Oman kinachozalisha chai ya MUMTAZ jijini Musact hivi karibuni. Bw. Koyi alikuwa nchini Oman kwa ziara ya kikazi.