Thursday, October 20, 2022

TANZANIA YAHAMASISHA WAWEKEZAJI SEKTA YA TEHAMA ILI KUKUZA UCHUMI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kunufaika kiuchumi kupitia sekta hiyo. 

Waziri Dkt. Tax amesema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya ASSECO  ya Poland Bw. Adam Goral, inayojishughulisha na masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yenye nia ya kuwekeza nchini.

Akizungumza na Rais huyo, Mhe. Dkt. Tax amemweleza nia ya Serikali ya Tanzania ya kutaka kujiimarisha kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari  na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupitia teknolojia hiyo nchi iweze kunufaika kiuchumi.

Mhe. Waziri amesema kuwa,  katika ulimwengu wa sasa mifumo mingi ya utendaji imebadilika ambapo kazi nyingi  hukamilishwa kwa kutumia vifaa vya kisasa kama simu, kompyuta na mtandao. Hivyo unahitajika uwekezaji wenye tija hususan kwenye eneo la usalama wa taarifa  za watumiaji.

Ameongeza kuwa matumizi ya tehama nchini yameendelea kukua  siku hadi siku ambapo taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali, za Fedha, Shule, Hospitali na nyingine hutegemea teknolojia ya uhakika na salama ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija. 

Amesema mbali na mchango mkubwa wa tehama katika ukuaji wa uchumi nchini pia imeendelea kuchangia uzalishaji wa ajira kwa watanzania hususan vijana.

"Tanzania inayo nia ya dhati ya  kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza na kunufaika kiuchumi kupitia matumizi  ya tehama. Hata hivyo jambo muhimu katika teknolojia hii ni usalama wa taarifa katika matumizi ya teknolojia hiyo. Hivyo, tungependa wawekezaji kulipa kipaumbele suala hili pale wanapokuja kuwekeza”, alisema Dkt. Tax.

Aidha, Mhe. Dkt. Tax ameahidi kuiunganisha taasisi hiyo na mamlaka husika nchini, ikiwemo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhusu nia yao ya kutaka kuwekeza nchini ili mazungumzo yaanze.

Kwa upande wake Rais wa Kampuni hiyo, Bw. Goral amemshukuru Mhe. Waziri kwa kutembelea Kampuni hiyo na kusema kampuni yake inatengeneza software zake yenyewe na kuongoza kwa teknolojia kwa upande wa Ulaya mashariki ina nia ya dhati ya kuwekeza  nchini na ipo tayari kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo mbalimbali ya tehama.

“Kampuni yetu ina nia ya dhati ya kuwekeza Tanzania na usalama wa matumizi ya mtandao ni kipaumbele chetu. Tayari tunayoo Program maalum ilianza mwaka 2020 inayoshughulikia usalama wa mitandao. Tupo tayari kubadilishana uzoefu na ujuzi na Tanzania” alisema Bw. Goral

Awali akitoa mada kwenye mkutano huo kuhusu hali ya matumizi ya teknolojia ya habari nchini,  Mtaalam wa Tehama kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy amesema  Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya tehama ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hadi sasa watanzania wanaomiliki simu ni milioni 28 na muamala ya simu imeingiza mapato ya zaidi Shilingi Trilion 20 kwa mwaka 2021 pekee.

Kampuni ya Asseco  iliyoanzishwa mwaka 1991 hutoa mafunzo na ushauri kuhusu masuala ya tehama na kutengeneza software zake yenyewe. Tayari imewekeza katika Mabara sita na nchi 60 ulimwenguni zikiwemo Ethiopia, Nigeria, Togo na Botswana kwa upande wa Bara la Afrika.

Mhe. Dkt. Tax alikuwa nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine alitumia ziara hiyo kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amakizungumza wakati wa mkutano kati yake na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya ASSECO ya Poland inayojishughulisha na masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Dkt. Adam Goral. Wakati wa Mkutano huo Kampuni ya ASSECO ilieleza nia yake  ya kuja nchini kuwekeza 

Rais wa Kampuni ya ASSECO, Dkt. Goral akizungumza wakati wa mkutano na Mhe. Dkt. Tax

Mkutano ukiendelea


Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akishiriki Mkutano huo. Kulia ni Afisa kutoka Ubalozi wa Tanzania Poland, Bw. Raphael Macha

Wajumbe kutoka Tanzania wakati wa mkutano huo

Wajumbe wengine wa Tanzania

Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy akiwasilisha mada kuhusu matumizi na changamoto za mtandao

Ujumbe wa Serikali ya Poland akiwemo Balozi wa Poland nchini Tanzania (kushoto)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiagana na Rais wa Kampuni ya ASSECO, Dkt. Goral


BALOZI CHIPETA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA MFALME WA UHOLANZI

 

 

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Caroline Kitana Chipeta akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mtukufu Mfalme Willem-Alexander wa Uholanzi

Balozi wa Tanzania katika Falme ya Uholanzi, Mhe. Caroline Kitana Chipeta akizungumza na Mtukufu Mfalme Willem-Alexander wa Uholanzi baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho

 
Balozi wa Tanzania katika Falme ya Uholanzi, Mhe. Caroline Kitana Chipeta katika picha na Mtukufu Mfalme Willem-Alexander wa Uholanzi baada ya kuwasilisha  Hati za Utambulisho kwa Mfalme huyo

Balozi wa Tanzania  katika Falme ya Uholanzi, Mhe. Caroline Kitana Chipeta katika picha ya pamoja na maafisa Ubalozi wa Tanzania nchini humo baada ya kuwasilisha  Hati za Utambulisho kwa Mfalme wa Uholanzi

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Caroline Kitana Chipeta alipowasili katika kasri  lililoko Noordeinde, The Hague,  Uholanzi kuwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mtukufu Mfalme Willem-Alexander wa Uholanzi 


 

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Falme ya Uholanzi , Mhe. Caroline Kitana Chipeta, awasilisha Hati za Utambulisho kwa Mtukufu Mfalme Willem-Alexander wa Uholanzi.

 

Hafla hiyo imefanyika katika moja ya Kasri za Kifalme iliyoko Noordeinde, The Hague,  Uholanzi tarehe 19 Oktoba, 2022.

 

Julai 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alimteua Balozi Caroline Kitana Chipeta kuwa Balozi wa Tanzania katika Falme ya Uholanzi.


Wednesday, October 19, 2022

DKT. STERGOMENA TAX AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA POLAND KUJA NCHINI

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Poland waje nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uchumi wa bluu na madini.

 

Waziri Tax ameyasema hayo, wakati akihutubia mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland. Mkutano huo ambao uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Poland na Ubalozi wa Tanzania nchini humo umefanyika katika Ofisi za Taasisi ya Uwekezaji na Biashara ya Poland zilizopo jijini Warsaw.

 

Mhe. Dkt. Tax amesema Serikali chini ya uongozi imara wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji wengi wenye tija na mitaji waje kuwekeza nchini.

 

Ameyataja maeneo ambayo yanahitaji wawekezaji kutoka Poland na sehemu nyingine duniani kuwa ni pamoja  uchimbaji madini, uchumi wa bluu, teknolojia ya habari na mawasiliano, viwanda vya sukari na nguo na miundombinu.

 

Amesema ili kuhakikisha wawekezaji wanaofika nchini wanafikia malengo yao, Serikali inaendelea kuboresha mifumo mbalimbali ikiwemo,  kuboresha upatikanaji wa viza na vibali mbalimbali lakini pia Serikali inaboresha mikataba mbalimbali ili kuondokana na urasimu wote kwenye sekta hiyo muhimu ya uwekezaji. Pia Serikali imeendelea kuboresha miundombinu yake ikiwemo Bandari ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wawekezaji. Huduma zingine zinazoboreshwa ni kuwa na umeme wa uhakika ambapo hadi sasa ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115  na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaendelea nchini.

 

Amesema ziara yake nchini Poland pamoja na mambo mengine inalenga kukuza baiashara na uwekezaji kati ya nchini hizi mbili.

 

“Ninawakaribisha wafanyabaiasha na wawekezaji kutoka Poland kuja Tanzania. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia imejipanga kikamilifu kuwahudumia. Tunaendelea siku hadi siku kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini” alisema Dkt. Tax.

 

Amesema mbali na maboresho hayo, Tanzania ni nchi sahihi kwa wawekezaji kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo amani, miundombinu ya kisasa ya barabara, reli, bandari na soko la uhakika kupitia uanachama wa Tanzania kwenye Jumuiya za kikanda za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko Huru la Biashara Barani Afrika (CFTA)

 

“Serikali imeendelea kuondoa  vikwazo vya  kuanzisha na kuendesha  biashara  kwa kupitia upya   sheria, kanuni na taratibu za biashara  na kuzifuta zile  ambazo zimethibitika  kuwa zinayafanya mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kuwa magumu.”

 

Mhe. Waziri  amesema kwa kuwa nchi ya Poland imepiga hatua kubwa katika masuala mengi ikiwemo teknolojia ya usimamizi wa maji, Tanzania ingefurahi kuona wawekezaji kutoka nchi hiyo wanawekeza kwenye sekta hiyo kwa wingi.

 

Amesema kuwa uchimbaji wa madini kama vile Tanzanite na mengine mengi, ni fursa nyingine ya kibiashara ambayo wafanyabiashara wa Poland wanakaribishwa kuichangamkia hapa nchini.

 

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Taasisi hiyo,  Bw. Zbigniew Sokal alitumia fursa hiyo kumweleza utayari wa Taasisi yake kushirikiana na Taasisi za Uwekezaji nchini ikiwemo TIC na ZIPA ili kujiimarisha zaidi. Alisema tayari makampuni kadhaa ya Poland yapo tayari kuwekeza nchini Tanzania.

 

Wakati wa Mkutano huo Wawakilishi kutoka Kampuni 10 za Poland zinazojishughulisha na masuala mbalimbali  ikiwemo utengenezaji wa mitambo ya kilimo, uchimbaji visima virefu, usimamizi wa maji na utunzaji wa mazingira, teknolojia mpya ya uchomeleaji vyuma na  umeme wa jua waliwasilisha mada kuhusu Kampuni zao.

                                                       

Wakati huhuo, Mhe. Waziri Dkt. Tax alipata fursa ya kutembelea Mradi mkubwa wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfera uliopo  katika mji wa Jozefow. Mradi huo wa aina yake pamoja na mambo mengine hususanya majitaka kutoka majumbani na kuyatibu kwa matumizi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji miti na maua katika mji huo. Kadhalika takangumu zingine hutayarishwa kitaalam na kuwa mbolea ya samadi kwa ajili ya mazao hayo ya miti na maua.

 

Akizungumza kuhusu mradi huo, Rais wa Kampuni hiyo, Bw. Stanslaw Zdanowicz amesema mradi huo ambao unaendeshwa kisasa, pamoja na mambo mengine umesaidia kuwapunguzia wananchi gharama za uondoshaji majitaka majumbani kwao.

 

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Tax alishukuru kupata fursa ya kutembelea Kampuni hiyo na kujionea teknolojia ya hali ya juu ya usimamizi wa kisasa wa majitaka na alitumia fursa hiyo kuwakaribisha nchini kuja kuwekeza pamoja na kutembelea vivutio vya utalii vya nchini ikiwemo Zanzibar, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.

 

Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

 

Katika ziara hiyo Mhe. Waziri Tax amefuatana na Wajumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),  Mamlaka ya Ukuzaji  Biashara na Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Wakala wa Taifa wa Hifadi ya Chakula (NFRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Makamu wa Rais wa Taasisi ya Biashara na Uwekezaji ya Poland Bw. Zbigniew Sokal alipowasili kwenye  Ofisi za Taasisi hiyo jijini Warsaw, Poland kwa ajili ya kushiriki Mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland wenye nia ya kuwekeza nchini. Wakati wa Mkutano huo Kampuni 10 ziliwasilisha mada. Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Poland. 

Mhe. Dkt. Tax akizungumza wakati wa Mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland wenye nia ya kuwekeza nchini. Pamoja na mambo mengine aliwaeleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini ikiwemo uchimbaji madini, uchumi wa bluu kilimo na  miundombinu,
 
Wajumbe kutoka Tanzania na Poland walifuatilia mkutano. Walioketi upande wa kushoto ni Balozi wa Poland nchini Tanzania, (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (katikati) na Brigedia Jenerali, Mkeremy
Mhe. Dkt. Tax akimsikiliza Bw. Sokal akizungumza. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Poland, Mhe. Abdallah Possi
Sehemu ya wajumbe kutoka Poland na Tanzania wakifuatilia mkutano
Sehemu nyingine ya wajumbe
Sehemu nyingine ya wajumbe
Sehemu nyingine ya wajumbe
Mkutano ukiendelea
Mkutano ukiendelea
 
   


 
  

.......Ziara ya Mhe. Dkt. Tax kwenye Mradi  wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfera

Mhe. Dkt. Tax na ujumbe wake wakifuatilia mada kuhusu Mradi wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfora kutoka kwa Rais wa Kampuni hiyo Bw. Stanisław Zdanowicz
Mhe. Dkt. Tax na ujumbe wake wakifuatilia mada

Mkutano ukiendelea
Mhe. Dkt Tax akipata maelezo ya namna wanavyobadilisha taka ngumu kuwa mboleaM
Mhe. Dkt. Tax akiwa kwenye moja ya maabara kwenye kampuni hiyo




Mhe. Dkt. Tax akipokea zawadi ya mchoro wa jengo hilo

Mhe. Dkt Tax akimpatia zawadi Rais wa Kampuni hiyo