Monday, August 7, 2017

Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameitaja tarehe ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania kuwa ni siku ya maendeleo ya kweli kwa Tanzania na Uganda na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.

Uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo litakalokuwa na urefu wa kilomita 1445 litakalogharimu takribani Shilingi trilioni 8 za Tanzania ulifanywa na Rais Magufuli na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga siku ya Jumamosi tarehe 05 Agosti 2017 na kushuhudiwa na umati mkubwa wa watu wakiwemo viongozi wakuu wa Serikali na vyama vya siasa kutoka pande zote mbili.

Rais Magufuli alieleza kuwa hadi kufikia hatua ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa bomba hilo, vikwazo vingi vilijitokeza, hivyo anamshukuru Rais Museveni kwa kuipa kipaumbele Tanzania kwa kuwa bomba hilo lingeweza kupita mahali pengine ambako umbali ungekuwa mfupi kwa zaidi ya kilomita 500.

Aliendelea kueleza kuwa licha ya Tanzania kutoa vivutio vingi kwa Uganda ikwemo kusamehe baadhi ya kodi kama za ongezeko la thamani lakini ujenzi wa bomba hilo utakuwa na manufaa makubwa kwaTanzania katika kipindi cha ujenzi unaotarajiwa kuanza mwezi Januari 2018 na kukamilika mwaka 2020 na baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.

"Tutapata mamilioni ya Dola yatakayotokana na ada ya usafirishaji ambayo ni Dola 12.5 kwa pipa moja na inakadiriwa kwa siku yatasafirishwa mapipa 216,000". Rais Magufuli alisema.

Manufaa mengine ni pamoja na ajira ambapo inakadiriwa watu kati ya elf 10 hadi 15 watapata ajira za kudumu bomba litakapokamilika na ajira za muda mfupi za watu zaidi ya elf 30 katika kipindi cha ujenzi.

Aidha, bomba litakuza biashara ya bidhaa mbalimbali ikiwemo saruji na vifaa vingine vitakavyotumika katika ujenzi wa bomba,  ujenzi wa nyumba za kupangisha na kuchochea ujenzi wa viwanda ambavyo malighafi zake zinatokana na mabaki yanayotokana na usafishaji wa mafuta kama vile viwanda vya mbolea. 

Vile vile, bomba linatarajiwa kupunguza gharama za uendeshaji katika sekta ya anga kutokana na unafuu wa mafuta na linakuja wakati mwafaka kwa kuwa Tanzania imeshaanza kulifufua shirika lake la ndege na Uganda ipo mbioni pia kulifufua shirika lake. Imeelezwa kuwa moja ya sababu ya Mashirika ya ndege ya nchi za Mashariki ya Kati kufanya vizuri kibiashara inatokana na unafuu wa mafuta ya ndege.

Mhe. Rais alitoa wito kwa wakandarasi watakaojenga bomba hilo kuharakisha  ujenzi ili uweze kukamilika kabla ya muda uliopangwa wa miaka mitatu.

"Kuna sababu gani ya kutumia muda wote huo wakati fedha zipo na wakandarasi wote mnatoka nchi kubwa zilizopiga hatua ya maendeleo, Tuoeni zabuni kwa wakandarasi wengini (sub contractors) ili ujenzi ukamilike kwa muda mfupi". Rais Magufuli alishauri. 

Wakandarasi watatu, wawili kutoka Ufaransa, Total na Cnooc na mwingine kutoka Uingereza, Tullow Oil kwa pamoja watajenga bomba hilo.

Mhe. Magufuli alibainisha kuwa Tanzania na Uganda zipo katika mazungumzo ili wataalamu wa Kiganda waliogundua mafuta hayo mwaka 2006 waje Tanzania kufanya utafiti kwenye maziwa ya Tanganyika na Eyasi ambayo yana viashiria vya kuwepo kwa mafuta.

Rais Magufuli alihitimisha hotuba yake kwa kumuhakikishia Mhe. Museveni kuwa Tanzania ni nchi iliyokamilika kiulinzi, hivyo Waganda wasiwe na wasi wasi kuhusu usalama wa bomba hilo ambalo litapita katika mikoa 8 ya Tanzania , wilaya 24 na vijiji 124.

Kwa upande wake, Rais Museveni aliishukuru Tanzania kwa kutoa vivutio vingi ili ujenzi wa bomba hilo uendelee kwani bila ya hivyo mafuta hayo hayatakuwa na faida ukizingatia bei ya mafuta katika soko la dunia imeshuka.

Alisema sababu kubwa ya bara la Afrika kuwa masikini hadi leo ni kutumia bidhaa isiyozalisha na kuzalisha bidhaa isiyotumia. 

Kwa mujibu ya takwimu alizotoa, nchi za Afrika Mashariki zinaagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 33 na inauza bidhaa zenye thamani ya Dola milioni 13.8 tu kwa mwaka. Fedha hizo zinafaidisha nchi zilioendelea kuimarisha uchumi wao na kuziacha nchi za Afrika kubaki masikini.

Kutokana na hali hiyo, Rais Museveni alizisihi nchi za Afrika zibadilishe mfumo wa uchumi kwa kujenga viwanda na kuuziana bidhaa. Hivyo, ana matumaini makubwa  kuwa ujenzi wa bomba hilo litaongeza kipato kitakachotumika kuchochea mabadiliko ya kiuchumi ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Martine Shigella aliwahakikishia Marais wawili kuwa mkoa umejipanga kutoa huduma stahiki kwa wageni wote watakaoingia mkoani humo kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo.

"Tumejipanga kuzalisha chakula cha kutosha na tumetenga maeneo ya kujenga nyumba za makazi, hivyo wawekezaji jitokezeni kuchukua maeneo hayo". Mkuu wa Mkoa alihimiza. Aliwasihi watu wa Tanga wasomeshe watoto wao ili waweze kuwa na vigezo vya kupata ajira zitakazotokana na ujenzi wa bomba hilo.

Alihitimisha kwa kumuomba Rais Magufuli asaidie kuimarisha bandari ya Tanga angalau iwe na kina cha mita 12 ili iweze kuhudumia meli zote zitakazotumika kubeba shehena za vifaa vya kujengea bomba la mafuta.


 -Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Tanga, 05 Agosti, 2017.

Viongozi Wakuu wa Serikali wakiwa katika mstari kwa ajili ya kuwapokea Waheshimiwa Marais wa Tanzania na Uganda kwenye viwanja vilivyofanyika hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania. Mwenye ushungi ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Madam Balozi Grace Martin, Mkuu wa Itifaki

Rais wa Jamhuri ya Muungno wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) akiwa kwenye Meza Kuu na Mgeni wake, Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni (katikati) na Makamu wa Rais, Mama Samia Hassan Suluhu.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Martine Shigella akitoa neno la ukaribisho kwa Marais wa Uganda na Tanzania na wageni waalikwa waliohudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta iliyofanyika katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga tarehe 05 Agosti 2015.

Bw. Guy Mourice, Rais wa Kampuni ya Total na Msimamizi  wa ujenzi wa bomba hilo akitoa maelezo mafupi kuhusu ujenzi wa bomba hilo utaskavyotekelezwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Mhe. Abdulrahman Kinana akiwasalimia viongozi na wananchi waliofurika viwanjani hapo kushuhudia hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta.

AWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi.

Makamu wa Rais, Mhe. Samia Hassan Suluhu akiwasalimia wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Uganda akisoma hotuba yake kwenye hafla ya uwekasji wa jiwe las msingi la ujenzi wa bomba ls mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisoma hotuba katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa bomba lamfuta kutoka Uganda hadi Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mhe. Paul Makonda akipeana Mkono na Bw. Ruge Mutahaba wa Cloud FM. Wawili hao walitakiwa  na Mhe. Rais Magufuli kumaliza tofauti zao.

Viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wabunge walioshiriki hafla hiyo.

Sehemu ya umati wa wananchi waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi.

Burdani ndani ya viwanja vya Chongoleani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakiweka jiwe la Msingi kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Waheshimiwa Marasi wakishikana mikono baada ya kuweka jiwe la msingi.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.