Wednesday, September 23, 2015

Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati azungumza na Balozi wa UAE nchini

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Abdallah Kilima (kulia) akimsikiliza Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mhe. Abdulla Ibrahim Ghanim Alsuwaidi (kushoto) alipokuja kujitambulisha na kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi  na Balozi mpya katika Idara hiyo ya Mashariki ya Kati. Katika mazungumzo yao waligusia masuala ya kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu.  
Afisa Mambo ya Nje, Bw. Hangi Mgaka akisikiliza mazungumzo kati ya Balozi Kilima na Balozi Abdulla Ibrahim Ghanim Alsuwaidi (hawapo pichani).
Balozi Kilima (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Alsuwaidi

Tuesday, September 22, 2015

Katibu Mkuu akutana kwa mazungumzo na Naibu Mwangalizi Mkuu wa Uchaguzi kutoka EU

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza  Naibu Mwangalizi Mkuu wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU), Bi.Tania Marques alipokuja Wizarani kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mipango ya Timu ya Waangalizi kutoka Jumuiya ya Ulaya wakati wa uchaguzi mkuu.
Maafisa Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo hayo kwa makini. Kushoto ni Bw.Gerald Ngwafu na Bi. Mona Mahecha
Balozi Mulamula (kulia) akizungumza na Bi.Marques
Balozi wa Umoja nchini, Mhe. Filiberto Sebregondi (wa kwanza kushoto) naye akichangia jambo wakati wa mazungumzo hayo.
Mazungumzo yakiendelea

BALOZI DORA MSECHU AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA RAIS ICELAND ATEMBELEA CHUO KIKUU CHA UMOJA WA MATAIFA, TAWI LA ICELAND

Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Nordic na Baltiki, Mhe. Dora Msechu akiwa na na Rais wa Iceland (HOM Iceland) baada ya kuwasilisha hati za utambulisho.
Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Nordic na Baltiki, Mhe. Dora Msechu akiwa katika mazungumzo  na Rais wa Iceland (HOM Iceland)  baada ya kuwasilisha hati za utambulisho.
Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Nordic na Baltiki, Mhe. Dora Msechu akiwa na na Rais wa Iceland (HOM Iceland) pamoja na Bw. Yusuph Mndolwa, Afisa Ubalozi, baada ya kuwasilisha hati za utambulisho leo
====================

Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Nordic na Baltiki, Mhe. Dora Msechu amewasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Rais wa Iceland, Mhe. Ólaf Ragnar Grimsson 

 Mhe. Balozi Dora Msechu sasa amekamilisha kazi ya kuwasilisha Hati za Utambulisho kwenye nchi zote nane za Eneo lake la Uwakilishi; Sweden, Denmark, Estonia, Finland, Iceland, Latvia, Lithuania na Norway. 

 Mhe. Balozi Dora Msechu amepata pia fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa, tawi la Iceland na kukutana na Mkuu wa Chuo Bw. Ludvik Georgsson kwa madhumuni ya kuwatafutia Watanzania fursa za masomo chuoni hapo kwenye fani ya joto ardhi (Geothermal).
Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Nordic na Baltiki, Mhe. Dora Msechu akilakiwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa, tawi la Iceland Bw. Ludvik Georgsson. Katikati  ni Bw. Ngereja Mgejwa, Mwanafunzi wa Kitanzania anayesoma Chuoni hapo.


Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Nordic na Baltiki, Mhe. Dora Msechu katika mazungumzo ya kuombea watanzania nafasi za masomo na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa, tawi la Iceland Bw. Ludvik Georgsson. Katikati  ni Bw. Ngereja Mgejwa, Mwanafunzi wa Kitanzania anayesoma Chuoni hapo.

Monday, September 21, 2015

Balozi Mulamula aongoza maadhimisho Siku ya Kimataifa ya Amani

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati akifungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Alliance Francaise, Jijini Dar es Salaam tarehe 21 Septemba, 2015. Balozi Mulamula alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo


Sehemu ya wageni waalikwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani akiwemo Balozi wa Afrika Kusini hapa nchini, Mhe. Thami Mseleku (mwenye suti ya kahawia) wakimsikiliza Balozi Mulamula (hayupo pichani) akihutubia wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez nae akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani. Bw. Rodriguez pia alisoma ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu maadhimisho hayo
Sehemu ya wageni waalikwa akiwemo Mama Shamim Khan ( wa kwanza kushoto) wakimsiliza Bw. Rodriguez (hayupo pichani)
Aliyekuwa Kamanda wa Kwanza wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na Vikundi vya Uasi nchini DRC, Meja Jenerali James Mwakibolwa akiwasilisha mada kuhusu "Wajibu wa Raia katika Kutunza Amani" wakati wa maadhimisho hayo
Sehemu ya wageni waalikwa na waandaaji wa maadhimisho hayo  akiwemo Bi. Stela Vuzo (kushoto), Afisa  kutoka Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) wakimsikiliza Meja Jenerali Mwakibolwa (hayupo pichani)  
Bw. Baraka Chelego akiwasilisha mada kuhusu Vijana na Uchaguzi: Fursa na Changamoto wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani
Sehemu ya Maafisa wa Jeshi wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa.
Kikundi cha Burudani kikitumbuiza wakati wa maadhimisho hayo huku mgeni rasmi Balozi Mulamula na wajumbe wengine kwenye meza kuu wakifurahia
Wageni waalikwa wakikishangilia kikundi cha burudani ( hakipo pichani). Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Maulidah Hassan.
Mmoja wa Wanafunzi walioshiriki maadhimisho hayo akitoa ujumbe wake kuhusu umuhimu wa wazazi na wananchi kwa ujumla wenye sifa ya kupiga kura kutumia fursa hiyo kuchagua viongozi bora na kuzingatia amani. 
Balozi Mulamula akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya maadhimisho kumalizika
Balozi Mulamula akiagana na Bw. Alvaro
Balozi Mulamula akiagana na Kiongozi wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini ambaye pia ni Balozi wa DRC, Mhe. Juma Halfan Mpango.
Balozi Mulamula akiagana na Balozi Mseleku
Picha ya pamoja

Picha na Reginald Philip
==================================================

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa Watanzania hususan vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuhakikisha amani iliyopo nchini inadumu.

Balozi Mulamula ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Alliance Française, Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamuala ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema kuwa kila Mtanzania anao wajibu wa kuchangia katika amani ya nchi huku akiwataka vijana ambao ni wengi kuhakikisha wanailinda amani iliyopo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na vizazi vijavyo.

Aliongeza kuwa fursa mbalimbali zikiwemo za uongozi na maisha bora hazipatikani  kwa kutumia nguvu wala vurugu na kuwataka vijana kujikita katika elimu, kufanya kazi kwa bidii  na uadilifu ili kutimiza ndoto zao ikiwemo kuwa viongozi wanaofaa hapo baadaye.

“Nahamasika kwamba vijana ambao ni asilimia 60 ya wananchi wa Tanzania wanao wajibu mkubwa katika kulinda amani ya nchi yetu na ninaamini kuwa kijana anaweza kuwa kiongozi popote pale alipo na katika lolote analolifanya hivyo nawaomba mjijenge kwenye elimu, bidii katika kazi na kuwa waadilifu ili muwe viongozi bora baadaye”, alisema Balozi Mulamula.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2015, Balozi Mulamula aliwahakikishia wananchi kuwa utakuwa wa amani na utulivu na kwamba wananchi wote wanao mchango mkubwa wa kuhakikisha amani inakuwepo wakati wote wa uchaguzi hadi hapo utakapokamilika. Vile vile alitoa rai kwa wananchi kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaowataka badala ya kuingia mitaani na kusababisha uvunjifu wa amani.

“Tumieni fursa iliyopo kuchagua viongozi bora. Kura yako ndio amani yako. Hivyo nawaomba wote wenye sifa mjitokeze kupiga kura wakati ukifika” alisisitiza Balozi Mulamula.

Awali akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa maadhimisho hayo ya 33 yanayobeba kauli mbiu isemayo Ushirikiano kwa ajili ya Amani; Utu kwa Wote yamefanyika wakati muafaka huku Tanzania ikijiandaa na uchaguzi mkuu na kuwataka vijana kuzingatia utawala wa sheria kwani kupanga ni kuchagua na kwamba  amani ndio kitu cha kwanza.

Aidha, katika ujumbe wake kwenye maadhimisho hayo uliosomwa na Bw. Rodriguez, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Kimoon ametoa wito kwa nchi zote duniani zinazokabiliwa na migogoro na uvunjifu wa amani kuweka silaha chini na kurejea katika meza za mazungumzo. Aidha amezitaka nchi zote duniani kuwekeza kwa vijana ambao ndio wajenzi wa amani.

Akiwasilisha mada wakati wa maadhimisho hayo kuhusu  Wajibu wa Raia katika Kutunza Amani” Kamanda wa Kwanza wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa iliyoanzishwa kupambana na Waasi huko DRC, Meja Jenerali, James Mwakibolwa alisema kuwa Tanzania imekuwa kisiwa cha amani kutokana na juhudi za viongozi katika kuhakikisha amani inadumishwa na vilevile ushirikiano mkubwa wa wananchi kwa serikali yao.

Aidha, aliongeza kuwa ili amani iliyopo idumu ni muhimu kuwa na viongozi thabiti wanaotenda haki na pia elimu ya uraia itolewe kwa wananchi kwani amani ikitoweka kila mtu ataathirika kwa namna moja au nyingine.

“Nimekuwa kwenye maeneo ya vita na ukosefu wa amani na nimejifunza kuwa amani ikitoweka si rahisi kuirejesha. Hivyo nawasihi Watanzania wenzangu kudumisha amani kwa kutii sheria bila shuruti na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama pale inapohitajika ili nchi iendelee kuwa na amani na kukuza uchumi kwa maendeleo ya nchi” alisema Meja Jenerali Mwakibolwa.

Siku ya Kimataifa ya Amani huadhimishwa duniani kote  tarehe 21 Septemba kila mwaka ambapo maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Ushirikiano kwa ajili ya Amani; Utu kwa Wote”.  

-Mwisho-


Friday, September 18, 2015

Balozi wa Uswisi nchini amtembelea Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, akimkaribisha Balozi wa Uswisi hapa nchini Mhe. Florence Tinguely Mattli ofisini kwake kwa mazungumzo ya kuboresha na kuendeleza ushirikiano mwema kati ya nchi hizo mbili. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani tarehe 18 Septemba, 2015 Jijini Dar es Salaam.
Balozi Liberata Mulamula akisisitiza jambo kwa Balozi wa Uswisi, Mhe. Florence Tinguely wakati wa mazungumzo yao.
 Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Florence Tinguely akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula.
Kikao kikiendelea....
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga, akizungumza na Balozi wa Switzerland Mhe. Florence Tinguely muda mfupi kabla ya mkutano huo kuanza.
 Picha ya pamoja kati ya Balozi  Mulamula Balozi  na Balozi  Mattli.
Picha ya pamoja 
========
PICHA NA REUBEN MCHOME.

Thursday, September 17, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Safari za Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete Nje ya Nchi

Wizara imesikitishwa na taarifa za uongo zilitolewa katika vyombo vya habari kuwa Mhe. Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uongozi wake wa miaka 10 ametumia Shilingi trilioni 4 kwa ajili ya safari za kikazi nje ya nchi, ambazo ni wastani wa bajeti nzima ya wizara kwa miaka ishirini na tano (25).

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kutoa ufafanuzi kuwa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, kiasi kikubwa kabisa cha bajeti kuwahi kutengwa kwa ajili ya safari za Viongozi Wakuu yaani Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ni shilingi bilioni 50 ambazo zilitengwa kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015 kwa ajili ya Idara ya Itifaki. Kwa miaka mingine yote wastani umekuwa ni kati ya shilingi bilioni tano hadi 25 kulingana na mahitaji ya idara hiyo.

Ifahamike kuwa kiasi hicho cha shilingi bilioni 50 ni bajeti nzima ya Idara ya Itifaki, ambapo kuna fungu maalum kwa ajili ya ziara za viongozi. Fungu hilo linagharamia makundi makuu matano kama ifuatavyo:
1.    Kundi la Rais wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
2.    Kundi la Makamu wa Rais wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
3.    Kundi la Waziri Mkuu wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
4.    Kundi la Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nje ya nchi wanapotembelea Tanzania; na
5.    Kundi la Wajumbe Maalum wanaokuja nchini kuleta taarifa muhimu kwa Rais.
Makundi yote haya hugaramiwa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ndani ya bajeti ya Idara ya Itifaki kifungu cha Ziara za Viongozi.  

Aidha uandaaji wa bajeti ya Wizara chini ya Idara ya Sera na Mipango unahusisha wadau wengine nje ya Wizara kama vile Kamati ya Bunge ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hupitishwa kila mwaka na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tunapenda kuwaatahadharisha wananchi juu ya watu wanaotoa taarifa za uongo kwa madhumuni ya  kujenga chuki dhidi ya Serikali.  Ikumbukwe kuwa ziara za viongozi zinazoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje zina mafanikio makubwa kwa nchi na Watanzania kwa ujumla.

Wizara inaandaa taarifa ya ndefu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara, changamoto na mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambayo itatolewa kwa umma kwa lengo la kutoa elimu zaidi. 

MWISHO.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
17 Septemba 2015


Tanzania na Norway kuimarisha ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akihutubia katika ufunguzi rasmi wa Semina ya Ushirikiano wa Kibiashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency ya Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Monica Maeland, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, Balozi wa Norway nchini, Mhe. Hanna-Marie Kaarstad na wadau wengine katika sekta ya biashara na uwekezaji kutoka Norway na hapa nchini.
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Maeland (kulia) akimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo. Kushoto ni  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula na katikati ni  Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Kaarstad. 
Waziri Membe akiendelea kuzungumza
Waziri wa Biasha na Viwanda nchini Norway Mhe. Monica Maeland naye alipata fursa ya kuzungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya Ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Norway, Mhe. Maeland yupo nchini kwa lengo la kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania nchini Norway. Pia wakati wa ziara hiyo Mhe. Maeland amezindua mtambo wa mbolea wa Yara ulioko kwenye Bandari ya Dar es Salaam na pia atatembelea Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga (kulia) na mmoja wa wadau katika semina hiyo Bw. John Ulanga (kushoto) wakifuatilia Hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa na Mhe. Membe na Mhe. Maeland (hawapo pichani). 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Tunsume Mwangolombe (katikati) naye akifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo.

Sehemu ya wadau wakifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo 
Semina ikiendelea
Waziri Membe (katikati) na Waziri Maeland kwa pamoja na wajumbe waliofuatana nao wakiwa kwenye mazungumzo mara baada ya kumaliza ufunguzi wa semina.
Waziri Membe (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya  faida ya semina hiyo ya wafanyabiashara wa Tanzania na Norway
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea


Picha na Reginald Philip
======================================================

TANZANIA NA NORWAY KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI

Waziri wa Mmabo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe ameisifu Serikali ya Norway kwa kuwa mshirika wa karibu wa maendeleo wa Tanzania hususan katika sekta za biashara na uwekezaji.

Waziri Membe alitoa kauli hiyo kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Abdallah Kigoda wakati akifungua rasmi semina kuhusu kuimarisha ushirikiano wa Kibiashara  na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam leo.

Katika ufunguzi huo ambao ulihudhuriwa pia na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Norway, Mhe. Monica Maeland ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi, Mhe. Membe alisema kuwa Tanzania na Norway zimekuwa na ushirikiano wa kidiplomasia kwa miaka mingi lakini sasa nchi hizi zimeamua kushirikiana zaidi katika masuala ya uwekezaji na biashara ili kukuza uchumi kwa maendeleo ya nchi zote mbili.

Aliongeza kuwa, kwa miaka mingi Tanzania imefaidika na  ushirikiano na Norway katika sekta mbalimbali ambapo nchi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuisaidia Tanzania kupambana na umaskini na kukuza uchumi. Hata hivyo alisema umefika wakati sasa nchi hizi mbili zinufaike kupitia biashara na uwekezaji ambapo nchi zote zina fursa nyingi katika maeneo hayo ikiwemo gesi na mafuta, kilimo na madini.

Mhe. Membe alisema kuwa kufanyika kwa semina hii itakayowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji itaongeza thamani katika uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili ambapo Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Norway ambayo ni miongoni mwa nchi zinazosafirisha zaidi gesi asilia na mafuta duniani. Hivyo aliwaasa Watanznaia kutumia semina hiyo kujifunza ili kuimarisha sekta ya nishati ya hapa nchini. 

“Semina hii ni fursa kwa Kampuni za Tanzania na Norway kujifunza na kubadilisha uzoefu na mawazo ya namna bora ya kuboresha sekta za biashara na uwekezaji kwa manufaa ya nchi zote mbili” alisema Waziri Membe.

Akizungumzia biashara inayofanyika kati ya Tanzania na Norway, Mhe. Membe alisema kuwa Tanzania inatakiwa kuongeza biashara yake nje ya nchi ili kuimarisha uchumi wake. Alieleza kuwa kwa sasa biashara kati ya Tanzania na Norway imeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi bilioni 6.9 mwaka 2014 kwa bidhaa zilizozwa Norway kutokea Tanzania ikiwemo kahawa, chai, viungo, maua, mbogamboga, mbao na madini.

Kwa upande wa bidhaa kutoka Norway, Tanzania imenunua kwa ongezeko la kutoka bilioni 22.3 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi bilioni 73 mwaka 2014. Bidhaa hizo ni pamoja na dawa za binadamu na bidhaa za viwandani.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara wa Norway, Mhe. Monica aliipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika maendeleo na ukuaji wa uchumi ambao umefikia asilimia 7. Alieleza kuwa Tanzania itafikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa vile inayo dhamira ya dhati na imejipanga kupitia uvumbuzi wa gesi na mafuta, nguvukazi ya vijana na mageuzi yaliyopo katika sekta ya uchumi.

Alieleza kuwa Norway ipo tayari kuendelea kuisadia Tanzania katika sekta ya gesi na mafuta kwa vile nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika eneo hilo hususan katika masuala ya teknolojia. Aidha, aliongeza kuwa Tanzania ni mshirika wa kweli wa Norway katika maendeleo hivyo nchi yake itashirikiana kikamilifu na Tanzania.
“Kuna msemo maarufu unasema kama unataka kwenda mbio nenda peke yako, lakini kama utanaka kufika mbali nenda pamoja na mwenzako. Hivyo Norway inataka kwenda pamoja na Tanzania ili kuziwezesha nchi hizi kufika mbali kimaendeleo” alisisitiza Mhe. Monica.

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Hanne-Marie Kaarstad alisema kuwa upo umuhimu mkubwa kwa nchi hizi mbili kukuza biashara kwa kuishirikisha sekta binafsi kikamilifu kwani ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu.

Semina hiyo ambayo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Norway, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) ilihudhuriwa na Makampuni 34 kutoka Norway na Tanzania na pia wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji.

-Mwisho-

Balozi Mulamula akutana na Balozi wa Uturuki nchini

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Uturuki hapa nchini, Mhe. Yasemin Eralp, baada ya Balozi huyo kumtembelea Katibu Mkuu kwa mazungumzo ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani tarehe 17 Septemba, 2015.
Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakifuatilia mazungumzo hayo. Kulia ni Bw. Kondo Ally na Bw. Anthony Mtafya (kushoto).
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Uturuki hapa nchini Mhe. Yasemin Eralp mara baada ya mazungumzo.
======================================
PICHA NA REUBEN MCHOME.