Sehemu ya Wajumbe wakifuatilia ufunguzi wakati Katibu Mkuu, Balozi Mulamula akizungumza (hayupo pichani) |
Sehemu nyingine ya wajumbe wakifuatilia ufunguzi |
Wajumbe wengine wa mkutano |
Mwenyekiti wa Asasi za Kiraia eneo la Maziwa Makuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku akizungumza wakati wa mkutano huo. |
Wajumbe wakifuatilia wakati Mzee Butiku akizungumza |
Balozi Mulamula akiagana na Mzee Butiku mara baada y akufungua mkutano |
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Samwel Shelukindo (kushoto) akizungumza na mmoja wa washiriki wa mkutano mara baada ya ufunguzi |
Balozi Mulamula akizungumza na Wandishi wa Habari kuhusu umuhimu wa Asasi za Kiraia katika eneo la Maziwa Makuu. |
Picha ya Pamoja kati ya mgeni rasmi Balozi Mulamula na Wajumbe wa Mkutano |
=================================
BALOZI MULAMULA: ASASI ZA KIRAIA ZINA MCHANGO MKUBWA KATIKA AMANI UKANDA WA MAZIWA MAKUU
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa Asasi za Kiraia zina nafasi kubwa katika utatuzi wa migogoro na kuleta amani hususan katika eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika kwa ujumla.
Balozi Mulamula aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa Wenyeviti wa Asasi za Kiraia kutoka Nchi za Maziwa Makuu unaofanyika kwa siku mbili katika Hoteli ya Golden Tulip, Jijini Dar es Salaam.
Balozi Mulamula ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Kwanza wa Sekretarieti ya Maziwa Makuu alisema kuwa kwa uzoefu wake utatuzi wa migogoro, kulinda amani na katika kuhakikisha demokrasia na utawala wa sheria vinafuatwa kila chombo kina nafasi na umuhimu wake na kwamba Asasi za Kiraia zina nafasi kubwa zaidi kwani zinawakilisha maoni ya wananchi.
“Asasi za Kiraia ni chombo muhimu sana katika kuhakikisha amani inakuwepo hususan katika Ukanda wa Maziwa Makuu kwani zinawawakilisha wananchi moja kwa moja hivyo ni vizuri kutambua nafasi yenu”, alisema Balozi Mulamula.
Aidha, aliipongeza Asasi hiyo ya ambayo kwa kiasi kikubwa imefanikiwa tangu ilipoanzishwa mwaka 2011 na kusisitiza ijikite zaidi katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha misingi ya demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria katika nchi za Ukanda wa Maziwa makuu vinafuatwa na kutekelezwa kikamilifu.
“Najua mnazijua hadidu za rejea na wajibu wenu kama Asasi za Kiraia, ni kuhakikisha nchi wanachama zinafuata misingi ya sheria, utawala bora na ule wa sheria ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara katika eneo letu la Maziwa Makuu”, alisisitiza Balozi Mulamula.
Awali akimkaribisha Balozi Mulamula kuzungumza, Mwneyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku alisema kwamba mkutano huo wa Wenyeviti wa Asasi kutoka nchi wanachama wa Maziwa Makuu ni muhimu sana hususan katika kipindi hiki ambapo pamoja na mambo mengine utaandaa na kupitisha agenda za Asasi hiyo zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari, 2016.
Aidha, aliongeza kuwa wakati umefika kwa Nchi Wanachama wa Maziwa Makuu kutambua mchango wa asasi za kiraia na kuzishirikisha ipasavyo katika msuala muhimu hususan yale ya utatuzi wa migogoro ili kuleta tija kwenye eneo hili la Maziwa Makuu ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa na migogoro ya kisiasa na kikabila.
Mkutano huo wa siku mbili uliwashirikisha Wenyeviti wa Asasi kutoka nchi zote 12 wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Jamhuri ya Congo, Angola, Sudan na Zambia.
(Mwisho)