Wednesday, December 30, 2015

Waziri Mahiga akutana na Mabalozi wa Qatar na Kuwait waliopo nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akifanya mazungumzo na Balozi wa Qatar Mhe. Abdullah Jassim Almaadadi alipofika Wizarani kwa ajili ya kumpongeza kwa kuteuliwa katika wadhifa wake mpya na pia kumhakikishia ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar. Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 30 Desemba, 2015.
Balozi Al maadadi naye akizungumza huku Mhe. Mahiga akimsikiliza.
Mazungumzo yakiendelea
Waziri Mahiga akiagana na Balozi Al Maadadi mara baada ya kumaliza mazungumzo.


.......Mkutano na Balozi wa Kuwait nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Augustine Mahiga (kulia) akizungumza na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Nassem Ibrahim Al Najib, alipokuja kumtembelea Wizarani na kufanya mazungumzo naye kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Kuwait na pia kumpongeza.
Balozi Mahiga akiagana na Balozi wa Kuwait mara baada ya kumaliza mazungumzo naye.

Picha na Reginald Philip

Waziri Mahiga apokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Palestina nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na  Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Palestina hapa nchini, Mhe. Hazem Shabat. Tukio hilo lilifanyika Wizarani tarehe 30 Desemba, 2015.
Waziri Mahiga akizungumza na Mhe. Balozi Mteule wa Palestina nchini, Mhe. Shabat mara baada ya kupokea nakala za hati  za utambulisho wake. Katika mazungumzo yao Balozi Shabat alimpongeza Waziri Mahiga kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo na kumuahidi ushirikiano. Pia Waziri Mahiga alimkaribisha nchini Balozi Shabat na kumuomba aendeleze mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Palestina.
Balozi Mteule wa Palestina nchini, Mhe. Shabat naye akizungumza huku Mhe. Dkt. Mahiga akimsikiliza.
Balozi Mteule Mhe. Shabat akimkabidhi Mhe. Mahiga zawadi ya picha inayoonesha Kanisa  lililopo katika mji wa  Jerusalem
Waziri Mahiga akiagana na Mhe. Shabat
Picha ya pamoja






Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nje akutana kwa mazungumzo na Balozi Mdogo wa China nchini.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Simba Yahaya akizungumza na Balozi Mdogo wa China, Mhe. Zhang Biao. Mazungumzo yao yalijikita katika kukuza mahusiano kati ya Tanzania na China katika sekta mbalimbali zikiwemo za biashara, uchumi na kijamii.
Mhe. Zhang Biao naye akizungumza
Maafisa kutoka Wizarani na Ubalozi wa China nao wakifuatilia mazungumzo
Balozi Simba akiagana na Mhe. Biao



Picha na Reginald Philip

Friday, December 25, 2015

Waziri Mahiga awasilisha ujumbe maalum wa Mhe. Rais Magufuli kwa Rais Nkurunziza

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Rajabu Gamaha mara baada ya kuwasili nchini humo kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum wa Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Rais wa Burundi, Mhe. Pierre Nkurunziza kuhusu hali ya kisiasa na usalama nchini humo.
Rais wa Burundi, Mhe. Pierre Nkurunziza akimkaribisha Waziri Mahiga alipowasili kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum kwake. Pembeni ni Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Gamaha.
Waziri Mahiga akimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Spika, Mhe. Aghaton Rwasa alipokutana kwa mazungumzo na Spika wa Bunge la Burundi, Mhe.Paschal Nyabenda (aliyekaa kushoto kwa Waziri Mahiga)

==================================== 



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mhe. Dkt. Augustine Mahiga leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi kwenye Ikulu yake jijini Bujumbura, Burundi kufuatia maagizo ya Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki ikiwa ni hatua ya Tanzania kutafuta suluhu ya kisiasa ya migogoro iliyojitokeza baina ya Serikali na vikundi vinavyo hatarisha amani nchini humo.
Kwenye mazungumzo yao yaliyodumu takriban saa mbili, Mhe. Mahiga alimueleza Rais Nkurunziza azma ya Rais Magufuli kuamsha mazungumzo ya kisiasa ya kuleta amani na kwamba tayari msuluhishi aliyeteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Kaguta  Museveni ameanza maandalizi ya uzinduzi wa mazungumzo hayo yatakayofanyika Entebe, Uganda tarehe 28 Desemba 2015. Waziri Mahiga pia alieleza maoni yake kuhusu hali ya utulivu aliyoiona kwa kipindi cha takriban saa 24 alizokuwa Jjijini Bujumbura na kwamba hakusikia sauti za milipuko wala silaha zozote.
Mhe. Nkurunziza alimshukuru mjumbe huyo wa Rais Magufuli na kumhakikishia ushiriki wa Burundi akieleza kuwa mazungumzo ya Entebe yatasaidia kuleta amani na mshikamano baina ya wananchi wa Burundi. Hata hivyo Mhe. Nkurunziza alisisitiza kuwa ili mazungumzo hayo yawe na tija ni lazima yawe muendelezo wa mazungumzo ya ndani ambayo yeye na Serikali yake wamekwisha yaanza. Aliongeza kuwa ni matumaini yake kuwa makundi yote nchini humo wataungana kwenye mazungumzo hayo yatakayojumuisha asasi za kiraia, kidini, vyama vya siasa na makundi mengine ili kujadili mustakabali wa taifa lao kwa pamoja.
Pamoja na kuridhia ushiriki wa Burundi kwenye mchakato huo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Nkurunziza alieleza kuwa yeye na Serikali yake wako tayari kushirikiana na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kutathmini hali ya usalama nchini mwake.  Hivi karibuni Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilitangaza kupeleka vikosi vya askari elfu tano nchini Burundi kufuatia kile kilichodaiwa kuwa viashiria vya mauaji ya kimbari kama yale yaliyofanyika nchini Rwanda miaka ya tisini.
Rais Nkurunziza alisema uamuzi huo wa Umoja wa Afrika umewashtua wao Serikalini na hata Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wanaohoji sababu za umoja huo kupeleka jeshi kubwa nchini humo. Burundi imekuwa ikishirikiana na Umoja wa Afrika kwenye ulinzi wa amani ambapo ina vikosi vya askari zaidi ya elfu sita nchini Somalia na Afrika ya Kati.
Naye Spika wa Bunge la Burundi Mhe. Paschal Nyabenda alieleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo wa Umoja wa Afrika. Mhe. Nyabenda ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD nchini humo alimweleza Mhe. Mahiga kuwa misingi ya kukataa ukabila imeainishwa kwenye katiba ya nchi hiyo na makubaliano ya Arusha ambapo inalazimisha taasisi zote ziwe na uwakilishi na pengine uwiano sawa kati ya Wahutu na Watusi. Akielezea muundo wa Bunge lake ambalo lina asilimia 60 kwa 40 ya uwakilishi wa Wahutu na Watusi Mhe. Nyabenda alisema kuwa Makamu wa Kwanza wa Spika Mhe. Agathon Rwasa anatoka kwenye kabila la Wahutu na Makamu wa Pili wa Spika, Mhe. Edouard Nduwimana anatokea kwenye kabila la Watusi.
Naibu Spika wa Kwanza wa Bunge hilo Mhe. Agathon Rwasa ambaye pia alishiriki kwenye mazungumzo hayo alisema kuwa wakati umefika sasa kwa Burundi kuangalia mbele na kwa manufaa na maendeleo ya vizazi vijavyo. Alisifu maendeleo aliyoyashuhudia nchini Tanzania ambapo alisisitiza yamekuwepo kutokana na amani nchini humo.
Akiwa nchini Burundi, Mhe. Mahiga na ujumbe wake walikutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Usalama wa Raia na Mambo ya Ndani ambapo alipokea taarifa ya Waziri Mhe. Alain Guillaume Bunyoni kuhusu hali ya usalama nchini humo tangu Rais Nkurunziza alipochaguliwa na chama chake kugombea tena nafasi ya Urais mwezi Aprili mwaka huu.
Kwa upande wake Waziri Mahiga alisifia jitihada zilizowekwa na Wizara hiyo hususan kwenye upande wa ulinzi wa raia na mali zao na kusisitiza umuhimu wa Wizara hiyo na Serikali nzima kuwaelezea wananchi na jumuiya za Kimataifa kwa ujumla jitihada za Serikali kuleta amani nchini humo.
Ziara ya siku mbili ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania ilianzia Entebe, nchini Uganda ambapo Mhe. Dkt. Mahiga alifanya mazungumzo na Mhe. Dkt Crispus Kiyonga, Waziri wa Ulinzi wa Uganda ambaye ameanza maandalizi ya mazungumzo ya amani chini ya uenyekiti wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
25 Desemba, 2015
                                                                                     




 

Wednesday, December 23, 2015

Taarifa kwa Vyombo vya Habari




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

ZIARA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA, MHE. DKT.AUGUSTINE MAHIGA NCHINI BURUNDI NA UGANDA
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augistine Mahiga (Mb), atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika nchi za Uganda na Burundi kuanzia tarehe 23 Desemba, 2015.

Ziara hiyo ya Mhe. Mahiga inafanyika kufuatia maelekezo ya Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kumtaka kwenda kufuatilia hali nchini humo ili kuiwezesha Jumuiya kushughulikia mgogoro wa kisiasa unaondelea nchini Burundi.

Akiwa Uganda, 2015, Mhe. Mahiga atakutana kwa mazungumzo na Mhe. Crispus Kiyonga, Waziri wa Ulinzi wa Uganda ambaye anaendelea na jukumu  la usuluhishi wa mgogoro wa kisiasa wa Burundi kwa niaba ya Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda.

Aidha, Mhe. Waziri atakutana na Mshauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Burundi, Ndg. Jamal Benomar.

Mhe. Waziri atasafiri siku hiyo hiyo kuelekea Bujumbura, Burundi ambapo atakutana na wadau mbalimbali wa mgogoro huo kabla ya kukutana na Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi. Mhe. Waziri atarejea Dar es Salaam tarehe 24 Desemba, 2015 baada ya kukamilika kwa ziara hiyo.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam
23 Desemba, 2015