Monday, March 7, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU WASIFU WA
KATIBU MKUU KIONGOZI MTEULE BALOZI MHANDISI JOHN KIJAZI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amemteua Balozi Mhandisi John William Kijazi (Pichani) kuwa Katibu Mkuu Kiongozi tarehe 6 Machi 2016, akichukua nafasi ya Balozi Ombeni Sefue. 

Kabla ya uteuzi huo, Balozi Mhandisi Kijazi alikuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal mwenye makazi yake jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi. Vilevile, hadi uteuzi wake, Balozi Kijazi amekuwa Mkuu wa Mabalozi wa Afrika nchini India ambaye amekuwa mtetezi mkuu wa wanafunzi wenye asili ya Kiafrika nchini India.

Kabla ya kuwa balozi, Mhandisi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India. 

Kati ya mwaka 1996 hadi 2002, Mhandisi Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya Wizara hiyo hiyo. 

Balozi Mhandisi Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.
Balozi Mhandisi John Kijazi amemuoa Fransiscar Kijazi na pamoja wamejaliwa watoto watatu, David, Emmanuel na Richard Kijazi. 

Balozi Mhandisi John Kijazi ataapishwa leo tarehe 7 Machi 2016 na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu jijini Dar es salaam. 

-MWISHO-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Kikanda na Kimataifa,
07 Machi 2016


Sunday, March 6, 2016

Rais wa Vietnam kufanya ziara ya kwanza ya kitaifa nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga (Mb.) (kulia), akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ziara ya kitaifa ya siku 4 ya Rais wa Vietnam nchini, Mhe.Truong Tan Seng kuanzia tarehe 08 hadi 11 Machi, 2016. Ziara hiyo itakuwa ni ziara ya kwanza ya kuja Tanzania pia Afrika. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga naye akisikiliza kwa makini mazungumzo ya Waziri na Waandishi wa Habari.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza kwa makini Balozi Mahiga (hayupo pichani).
Bi. Mindi Kasiga naye akitolea ufafanuzi ratiba nzima ya ziara ya Rais huyo wa Vietnam
Sehemu nyingine ya waandishi wa Habari wakinukuu baadhi ya pointi wakati mkutano ukiendelea
Kikao na waandishi wa Habari kikiendelea.

Picha na Reginald Philip

==================================================



Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang atakuwa Rais wa kwanza kufanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Rais Sang atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere siku ya Jumanne tarehe 08 Machi 2016 saa mbili usiku na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambapo mapokezi rasmi yatafanywa siku ya pili na mwenyeji wake, Rais Dkt. Magufuli katika Viwanja vya Ikulu.

Akiongea na Waandishi wa Habari Ofisini kwake leo, Waziri Mahiga alieleza kuwa Rais Sang atafutana na mke wake, Mama Mai Thi, Mawaziri watano na Wafanyabiashara 51 katika ziara hiyo. Dkt. Mahiga alieleza kuwa Serikali inaupa uzito wa pekee ugeni huo kwa sababu ni ziara ya kwanza ya kitaifa katika Awamu ya Tano kufanywa na Mkuu wa Nchi. “Wakuu wa Nchi kadhaa walishakuja hapa nchini lakini kwa ziara za kikazi, sio za kiserikali, hivyo Vietnam imetupa heshima kubwa sana”.  Waziri Mahiga alisema.

Rais Sang ni mara ya kwanza kufanya ziara katika Bara la Afrika na Tanzania ambapo pia atazuru nchi ya Msumbiji baada ya kuondoka hapa nchini tarehe 11 Machi 2016.

Dkt. Mahiga aliwambia Waandishi wa Habari kuwa Tanzania ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Vietnam namna ilivyopiga hatua kubwa ya maendeleo katika kipindi kifupi, licha ya kuendesha vita kubwa ya mapambano ya kupigania uhuru dhidi ya Ufaransa na baadaye dhidi ya Marekani. Alisema nchi hiyo imepiga hatua katika sekta za viwanda, kilimo, mawasiliano na uvuvi.  Kwa upande wa kilimo, nchi hiyo ni ya kwanza kwa kuuza kahawa aina ya robusta na korosho duniani ingawa mbegu za mazao hayo zimechukuliwa Tanzania. 

Aidha, Vietnam ni maarufu duniani kwa kuuza samaki aina ya sato ambao walichukuliwa kutoka Ziwa Victoria.

Waziri wa Mambo ya Nje alieleza kuwa ili Tanzania nayo ifike ilipo Vietnam ni lazima ifuate mambo matatu ambayo Vietnam inayazingatia. Mambo hayo ni kufanya kazi kwa bidii katika mazingira ya aina zote, utekelezaji wa maamuzi wanayofanya na kuwekeza katika mafunzo ya ufundi, miundombinu kama ya umeme, barabara, reli, bandari na mabemki kwa ajili ya mitaji na huduma nyingine za kifedha.

Katika ziara hiyo, Rais wa Vietnam pamoja na mambo mengine atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake; Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein; Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai; Kuongea na wafanyabiashara na kutembelea eneo la uwekezaji la EPZA, Ubungo Jijini Dar es Salaam.

-Mwisho-


Friday, March 4, 2016

TANZIA

Marehemu Balozi Joseph Rwegasira
TANZIA
  
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa inasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 1993 hadi 1995, Balozi Joseph Rwegasira (Pichani) kilichotokea tarehe 04 Machi, 2016 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Jijini Dar es Salaam.

Msiba upo nyumbani kwa Marehemu Msasani Jijini Dar es Salaam ambapo tarehe 06 Machi, 2016 mwili wa Marehemu Balozi Rwegasira utaagwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Peter Mbuyuni saa 8.00 mchana.

Aidha, tarehe 07 Machi, 2016 mwili wa Marehemu utasafirishwa kulekea Bukoba, Kagera kwa mazishi.

Wizara inatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu.

Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amina.

Imetolewa na: Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dar es Salaam
04 Machi, 2016




EU Head of Delegation to Tanzania pays a visit at the Ministry of Foreign Affairs

Head of Delegation of the European Union to Tanzania, H.E Roeland Van De Geer (L)  in discussion with the Director of Europe and the Americas in the Ministry of Foreign Affairs, East Africa, Regional and International Cooperation, Amb. Joseph Sokoine when the two met at the Ministry's office yesterday. In their discussion, EU Head of Delegation commended the President of the United Republic of Tanzania who is also the chair of the East African Community (EAC), H.E Dr. John Pombe Magufuli the way he chaired the EAC summit held in Arusha on the 2nd  of March 2016. He also commended the appointment of the former President of the United Republic of Tanzania, H.E Benjamin Mkapa as a facilitator for Burundi peace talks. 
Amb. Sokoine (R) listening attentively to the EU Head of Delegation while officials from Ministry of Foreign Affairs and EU take important points.
Amb. Sokoine and EU Head of Delegation to Tanzania shake hands after their discussion.

WAKUU WA NCHI WA EAC WAFANYA UZINDUZI UJENZI WA BARABARA.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwasalimia wakazi wa Arusha, viongozi na wawakilishi wa mataifa mbalimbali hawapo pichani ambao walihudhuria hafla fupi ya uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa barabara ya Arusha -Holili/Taveta -Voi km 234.3 uliofanyika Tengeru nje kidogo ya jiji la Arusha, tarehe 3 March,2016.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Masharika, Kikanda na Kimataifa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akiwasilisha taarifa ya Tanzania katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa barabara ya Arusha-Holili/Taveta-Voi Km234.3.
Mhe. Rais Dkt. Magufuli na Mhe.  Rais Uhuru Kenyatta wakiongoza zoezi maalum la kukata utepe kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa Mradi wa barabara Arusha-Holili/Taveta-Voi, wakiwa pamoja na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na viongozi mbalimbali walioshiriki hafla fupi ya Uzinduzi huo.
Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni akiagana na Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe tayari kwa kuanza safari ya kurudi nchini Uganda mara baada ya kukamilisha shughuli zilizoambatana na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta akitoa neno la shukrani kwa waziri wa Nishati na Madini Mhe. Sospeter Muhungo kuishukuru Serikali ya Tanzania tayari kwa safari ya kurudi nchini Kenya mara baada ya kukamilisha ushiriki wa Mkutano na kuzindua mradi wa ujenzi wa barabara unayoiunganisha nchi ya Kenya na Tanzania.

Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ally Mohamed Shein akiondoka katika uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwa safari ya kuelekea visiwani Zanzibar mara baada ya kukamilisha zoezi la uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha -Holili/Taveta-Voi uliofanyika Tengeru nje kidogo ya Jiji la Arusha, tarehe 3 Machi,2016.