===========================================
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini hati mbili za
makubaliano na Serikali ya Japan itakayoiwezesha Tanzania kupata kiasi Yen
Bilioni 6 ambazo ni sawa na Sh. Bilioni 116.4 za Kitanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusaini hati hizo,
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile alisema mkataba
wa kwanza utasaidia katika kukamilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17.
Dkt. Likwelile alisema kuwa msaada huo unalenga kuweka mazingira rafiki
ya kwa wafanyabiashara, kuboresha masoko na kuwezesha mazingira ya ushindani
katika utengenezaji wa ajira nchini.
Mkataba wa pili unahusu masuala ya kiufundi yatakayotumika
katika kufanya marekebisho ya mkataba uliosainiwa Octoba 20, 1966, kwa
kuzingatia sheria nyingi zimebadilika, kusainiwa kwa hati hiyo ya
makubaliano itasaidia kutabadilisha baadhi ya vifungu vyenye jina Tanzania na
kuweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujumuisha pande zote mbili za
Muungano katika kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
Aidha, makubaliano hayo yatasaidia kubadilisha baadhi ya vipengele vya
mkataba uliopita ikiwemo kipengele cha usambazaji wa madawa ili kuweza kukidhi
mahitaji ya sasa ya wataalamu kutoka nchini Japan kuweza kuja kufanya kazi za
kujitolea hapa nchini Tanzania.
Katibu Mkuu Dkt. Likwelile ameishukuru Serikali ya Japan na kusisitiza
kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyopangwa ili kuweza kuwa na tija na
kuwaletea maendeleo Watanzania.
Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida amesema kuwa
Serikali ya Japan ina imani kuwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili
utasaidia kukuza maendeleo ya uchumi na kijamii.
Balozi Yoshida amesema kuwa Serikali ya Japani inaunga mkono juhudi za
Serikali inayo ongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika masuala ya viwanda na
mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji kuwekeza nchini Tanzania.
Adha amesema kuwa Japan itaendelea kuwaleta vijana wanaojitolea katika
sekta ya uchumii na ya kijamii jambo limekuwa likitekelezwa tangu mwaka 1969
ambapo hadi sasa idadi ya vijana hao wa kujitolea imefikia zaidi ya 1500.