Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu majukumu na taarifa mbalimbali za utekelezaji za Wizara pamoja na kufafanua taratibu za kiutumishi katika Balozi za Tanzania, sambamba na kuelezea mafanikio yaliyopatikana kutokana na ziara ya wafanyabishara kutoka nchini Oman kwenye mkutano uliofanyika leo katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
Afisa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bw. Tahir Khamis ambaye alikuwa miongoni mwa waratibu wa ziara ya wafanyabiashara kutoka nchini Oman akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea.
Wakati mkutano ukiendelea
===============================================
===============================================
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Kikanda na Kimataifa imejipanga kuwapeleka kwenye Balozi zake nje Watumishi
wapatao 105 na kuwarejesha nchini wengine 79 ambao miongoni mwao muda wao wa
utumishi balozini (Tour of Duty) umemalizika na wengine kustaafu kwa mujibu wa
sheria za Utumishi wa Umma. Kwa kawaida tour
of duty kwa Watumishi nje ni ya muda wa miaka minne (4).
Tanzania ina Balozi 35 nje ya nchi ambazo kwa
ujumla wake zina Watumishi 234. Miongoni mwa Watumishi watakaorejea nchini wamo
Mabalozi, Maafisa, Wahasibu na Makatibu Muhtasi.
Hadi sasa Mabalozi waliorejea nchini ni watatu (3)
ambao ni Balozi Peter Kalaghe
aliyekuwa Uingereza, Balozi James
Msekela aliyekuwa Italia na Balozi
Batilda Burian aliyekuwa Japan.
Itakumbukwa kuwa, Januari 25, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliiagiza
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa
kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi hao ambao mikataba yao iliisha na
wengine kwa ajili ya kupangiwa majukumu mengine.
Aidha, jumla ya Watumishi tisa wa kada mbalimbali waliokuwa Balozini
wamerejea nchini hadi sasa na wengine wanaendelea kurejea kulingana na
upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha jukumu hilo.
Utaratibu wa kuwapeleka na kuwarejesha Watumishi
Balozini ni wa kawaida na upo duniani kote kwa mujibu wa sheria za kimataifa
ukiwemo Mkataba wa Vienna unaotoa mwongozo kwenye masuala ya kidiplomasia.
Wizara itaendelea kupeleka Watumishi wenye sifa na
tija kwa taifa ili kuiwakilisha nchi kikamilifu.
WAKATI HUOHUO, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Oman Mhe. Dkt. Ali Bin
Masoud Al Sunaidy alifanya ziara ya
kikazi nchini Tanzania kuanzia tarehe 12 April hadi 14 April, 2016.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kushiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji
baina ya Tanzania na Oman, kongamano hili lilikuwa na kauli mbiu ya ‘’ Oman
Tanzania Road show : Exploring Opportunities in Investment and Business
between Tanzania and Oman’’.
Ziara na kongamano hili imelenga zaidi katika sekta za Madini, Kilimo
na uboreshaji wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Miundombinu na Mawasilisno, Uvuvi,
Usafirishaji, Utalii, Petroli na Gesi. Mgeni Rasmi katika kongamano hili
alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan
Katika ziara hii, Mhe. Waziri Al
Sunaidy aliongozana na ujumbe wa watu 108 ambapo 12 walikuwa ni Maafisa kutoka Taasisi
mbalimbali za Serikali ya Oman na wengine waliobaki kutoka Sekta Binafsi kutoka
nchi hiyo kwa lengo la kukutana na Taasisi kama hizo hapa nchini.
Kwa upande wa Tanzania wafanyabiashara
190 walishiriki na wenzao kutoka Oman katika kongamano na baadae katika
mikutano ya ana kwa ana (Business to Business meetings).
MAFANIKIO YA ZIARA
1.
Wakati
wa ziara hiyo, Tanzania na Oman zilisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano
baina ya Tanzania Chambers of Commerce na Oman
Chambers of Commerce wa kuanzisha Kampuni ya Oman Tanzania Investment
Company (OTIC). Kampuni imeanzishwa kwa lengo la kutafuta fursa za
uwekezaji Tanzania na Oman na imeazimia kuanza na mtaji wa Dola za Marekani
milioni 25 ambazo zitatumika kutoa mikopo kwa wawekezaji ;
2.
Serikali
ya Oman imeonesha nia ya kuwekeza katika kiwanda cha Sukari cha Kagera (Kagera
Sugar) na kukipa uwezo wa kuzalisha tani 400,000 ambazo zitauzwa katika soko la
Tanzania. Uzalishaji huu pia utahusisha uzalishaji wa Umeme, spiriti na hamira itokanayo na mabaki katika kuchakata sukari. Umeme
utaingizwa katika gridi ya Taifa wakati spiriti ambayo ni muhimu katika
matumizi ya tiba itauzwa katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania. Aidha, Oman
inahitaji hamira ambayo inahitajika kwa kiasi kikubwa nchini humo na nchi
zingine za mashariki ya kati ;
3.
Mbali
na uzalishaji wa sukari, Serikali ya Oman pia inakusudia kuingia ubia na Kagera
Sugar katika kilimo cha umwagiliaji cha uzalishaji wa mazao ya chakula kwa
ajili ya matumizi ya Oman na Tanzania. Utekelezaji wa miradi hii utaleta faida
kwa Tanzania ikiwa ni kuongeza uzalishaji wa sukari na hivyo kupunguza pengo
kati ya uzalishaji na mahitaji halisi ya sukari, lakini pia unategemea
kuzalisha nafasi zaidi ya 5,000 za ajira na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu
wa ajira ;
4.
Serikali
ya Oman pia ilionyesha nia yake ya kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika mradi
wa uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Tanga lakini pia kuziwezesha bandari za
Tanzania kuwa na ushirikiano na zile za Oman ;
5.
Wawekezaji
kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za kisasa
mkoani Mtwara ili kuondoa tatizo la makazi stahili kwa watendaji wakuu wa makampuni
ya mafuta na shughuli zinazoendana na sekta hii ambao hulazimika kila siku
kusafiri kwa ndege kutoka Dar Es Salaam kwenda Mtwara na kurudi jambo ambalo
lina gharama kubwa pamoja na ombi la hekta 1,000 kwa ajili ya kilimo cha mboga
mboga na maua;
6.
Wawekezaji
kutoka Oman pia wameonyesha nia ya kuwekeza katika maeneo kadhaa ikiwemo
uzalishaji wa mitamba na chakula cha mifugo huko Mivumoni, Tanga, ranchi na
machinjio ya Ruvu, miundombinu na viwanja vya ndege, ujenzi wa nyumba za
kisasa Kigamboni na Zanzibar pamoja na
miradi mingine katika sekta ya utalii
pamoja na kuwekeza katika sekta ya viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo
na mifugo ;
7.
Wafanyabiashara
wa Tanzania wamepata nafasi ya kutambua fursa zilizopo Oman ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa soko kwa bidhaa za chakula kama vile matunda, nyama, unga,
sukari, hamira nk; na
8.
Tanzania
kwa ujumla ilinufaika kwa kutangaza fursa za uwekezaji ambazo zipo katika sekta
zinazolengwa na wawekezaji wa Oman lakini pia kubaini fursa zilizopo Oman
ambazo wafanya biashara wa Tanzania wanaweza kunufaika nazo pamoja na
kuwaunganisha wafanya biashara wa Tanzania na wenzao wa Oman katika kukuza
biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu.
Hivyo, utekelezaji wa matarajio
haya unategemea kuongeza ajira, kuongeza ubora na thamani ya mazao ya kilimo na
kutanua wigo wa masoko kwa bidhaa za Tanzania na pia kukuza sekta ya viwanda
nchini.