Mkutano wa 34 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam umefikia tamati. Mkutano huu uliofanyika katika Hoteli ya Serena umehudhuriwa na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka nchi wanachama, watendaji mbalimbali wa Wizara, mashirika ya umma, Watendaji wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na taasisi mbalimbali za Serikali ndani ya Jumuiya.
Pamoja na mambo mengine Mkutano huu ulikuwa ni maalum kwa ajili ya kuandaa agenda zinazohitaji maamuzi ya Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Agenda hizo zinatokana na taarifa ya utekelezaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali ya Mkutano uliopita wa Wakuu wa nchi wa Jumuiya wa mwaka 2015/2016, iliyo andaliwa na Mkutano wa ngazi ya wataalamu.
Baadhi ya mambo yaliyopo kwenye taarifa hiyo ya utekelezaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali ya Mkutano uliopita wa Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2015/2016 ambayo imekabidhiwa kwa Baraza la Mawaziri yanajumuisha mambo yafuatayo;
· Taarifa ya namna ya kuwezesha uundaji wa magari katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupunguza uagizaji wa magari yaliyotumika kutoka nje ya Jumuiya
· Taarifa ya mapitio kuhusu sekta ya nguo na ngozi juu ya kuzuia/kuondoa uagizaji wa nguo na viatu vilivyotumika kutoka nje na;
· Taarifa ya namna endelevu ya Uchangiaji wa bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na wanahabari punde baada ya mkutano amesema Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri umekuwa na mafanikio makubwa kwanza, kutokana na idadi kubwa na yakuridhisha ya wajumbe walioshiriki Mkutano kutoka nchi wanachama ,na pili ni kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka miwili ambayo Tanzania ilikuwa mwenyekiti wa Jumuiya hadi sasa inapokabidhi kwa nchi ya Jamhuri ya Uganda.
Mfanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uwenyekiti;
Waziri Mahiga ameyataja mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka miwili Tanzania ikiwa mwenyekiti wa Jumuiya kuwa ni; kuongezeka kwa nchi ya Sudan Kusini katika Jumuiya, kuboreka kwa mfumo wa elimu kwa ngazi ya elimu ya juu katika Jumuiya na kupungua kwa vikwazo vya biashara vinavyotokana na vikwazo visivyokuwa vya kiforodha ndani ya Jumuiya vilivyopelekea kurahisisha na kuhamasisha biashara katika Jumuiya.
Mkutano huu wa Baraza la Mawaziri utafuatiwa na Mkutano wa 18 wa Kaiwada wa Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uanaotarajiwa kufanyika tarehe 20 Mei, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine Mkutano wa Wakuu wa nchi unatarajiwa kupokea ripoti ya usuluhishi ya kamati inayoongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamini William Mkapa.
Tanzania ilikabidhiwa uwenyekiti wa Jumuiya mwishoni mwa mwaka 2014 katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi uliofanyika Nairobi, Kenya; na ikapewa tena nafasi ya kuendelea kushikilia kiti hicho mwaka 2015, ambapo mpaka sasa Tanzania wakati inaelekea kukabidhi nafasi hii ya uwenyekiti kwa nchi ya Uganda, Tanzania imekuwa mwenyekiti wa Jumuiya kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo.