TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara ya Mambo ya Nje yatoa elimu ya Mtangamano Pemba
Serikali ya Zanzibar imeahidi kuwa itaendelea na jitihada za kuimarisha huduma za kiuchumi kwa madhumuni ya kuweka mazingira mazuri ya kibiashara ili wananchi waweze kunufaika na fursa zinazopatikana kwenye Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Issa Gavu alipokuwa anafunga semina ya siku nne kuhusu mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake iliyofanyika Pemba kuanzia tarehe 15 hadi 18 Mei 2017.
Mhe. Gavu alitoa wito kwa wanasemina hao ambao wengi wao walikuwa ni wajasiriamali kutengeneza bidhaa zenye ubora kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia ya ulimwengu wa sasa ili ziwe na uwezo wa kushindana na bidhaa nyingine katika soko la EAC.
Aidha, Mhe. Gavu aliahidi kuwa Serikali itasaidia wajasiriamali washiriki makongamano, semina, maonesho na warsha mbalimbaili zinazofanyika nchini na nje ya nchi ili iwe fursa kwao kujifunza mambo mapya yanayoendana na ulimwengu wa sasa kwa lengo la kuboresha biashara zao.
Mhe. Gavu aliwasihi wote waliopata na watakaopata fursa za mafunzo kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ili kwa pamoja watumie mbinu, ujuzi na uzoefu wanaoupata kukabili changamoto za ushindani wa soko kulingana na mahitaji ya sasa.
Alisisitiza umuhimu wa nchi zote wanachama wa EAC kuwahudumia raia wa nchi zote kwa usawa bila ubaguzi. Alisema endapo nchi moja ikiwa na tabia ya kunyanyasa raia wa nchi nyingine inaweza kusababisha dhana ya kulipiza kisasi hatimaye vurugu na kuleta mkanganyiko katika Jumuiya.
Vile vile, Waziri wa Nchi alitoa wito kwa nchi zote wanachama kushirikiana kwa pamoja kudhibiti biashara ya magendo. "Sio sahihi kwa nchi moja kufumbia macho biashara ya magendo kwa kutochukua hatua dhidi ya wanaoingiza na kununua bidhaa za magendo". Mhe Gavu alisema. Zanzibar inakabiliwa na biashara ya magendo ya zao la karafuu ambayo inasafirishwa kwa njia za panya kwenda nchi za jirani.
Kwa upande wao wajasiriamali wameahidi kuwa watatumia mafunzo waliyopata kulikabili Soko la EAC bila khofu yeyote kama ilivyokuwa hapo awali.
Semina hiyo ya siku nne ilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga na ilitolewa na wataalamu wa Wizara kwa kushirikiana na Prof. Ammon Mbelle kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 18 Mei, 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.