Saturday, May 20, 2017

Mkutano wa 18 wa Kawaida wa Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wafikia tamati


Mkutano wa 18 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefikia tamati leo Ikulu Jijini Dar es Salaa. Mkatano huu ulikuwa na ujumbe na uwakilishi kutoka nchi zote sita zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki. .

Rais Mhe. Dkt. Magufuli akizungumza katika Mkutano huu wakati wa kukabidhi kiti cha Uwenyekiti amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Uwenyekiti wa Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki imepata mafanikio makubwa na kuifanya istawi zaidi katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara kutokana na kupunguzwa kwa vikwazo vya biashara visivyokuwa vya kiforodha, kuboreka kwa mfumo wa elimu ya Juu ndani ya Jumuiya na kuongezeka kwa Sudan Kusini katika Jumuiya.

Aidha mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Mhe. Museveni akiongea mara baada ya kukabidhiwa nafasi hiyo amesema kunakila sababu ya kulinda na kudumisha Mtangamano kwa kuwa unaharakisha kasi ya maendeleo ya nchi wanachama na watu wake, unaimarisha ulinzi na usalama wa nchi wanachama, na kudumisha undugu wa kihistoria uliodumu kwa muda mrefu miongoni mwa nchi wanachama.

Pia Mkutano huu wa 18 wa Wakuu wa nchi umeshuhudia viapo vya viongozi wapya wawili katika ngazi ya Jumuiya ambao ni Jaji wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Sudan Kusini, Jaji Charles Oyo Nyawezo na Naibu Katibu Mkuu wa Sekretariat ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Eng. Steven Mrote kutoka Tanzania.


Katika Kutano huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekabidhi rasmi uwenyekiti kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni.

Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia hadhira iliyohudhuria Mkutano wa 18 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisaini moja ya nyaraka ya makabidhiano ya uwenyekiti wakati wa Mkutano wa 18 wa Kaiwa wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mshariki.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (wakwanza kulia) akifuatilia Mkutano. Wengine ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt. Philip Mpango (katika) na Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (kushoto).



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Aziz P. Mlima (kulia) akifuatilia Mkutano

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Jaji Charles Oyo Nyawezo kutoka Sudan Kusini kwa kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  mara baada ya kula kiapo.

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Eng.Steven Mrote kutoka Tanzania kwa kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Sekretariat ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  mara baada ya kula kiapo.

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza mwanafunzi wa kitado cha nne aliyejishindia nafasi ya nne katika mashindano ya uandishi wa insha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Shule ya Sekondari Kibaha, Tanzania Bw.Joseph Mbogo

Waziri Mhe. Mahiga akifuatilia Mkutano 

Picha ya pamoja

Friday, May 19, 2017

TANZANIA NA CHINA ZATILIANA SAINI MKATABA WA KUUZA BIDHAA ZA MUHOGO


Balozi wa Tanzania nchini China Mhe.Balozi Mbelwa Kairuki kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Li Yuanping Naibu mkurugenzi mkuu wa taasisi ya udhibiti na ukaguzi wa mazao kwa niaba ya
Serikali ya jamhuri ya China wakitia saini mkataba wa kuuza China bidhaa za muhogo kutoka Tanzania.
Balozi wa Tanzania nchini China Mhe.Balozi Mbelwa Kairuki kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipeana mkono na Naibu Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya udhibiti na ukaguzi wa mazao, Li Yuanping kwa niaba ya Serikali ya jamhuri ya China mara baada ya kutiasaini mkataba wa kuuza China bidhaa za muhogo kutoka Tanzania.

Wizara ya Mambo ya Nje yatoa elimu ya Mtangamano Pemba

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Issa Gavu akisoma hotuba ya kufunga semina kuhusu elimu ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake. Semina hiyo iliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilifanyika Pemba kuanzia tarehe 15 - 18 Mei 2017. Wengine katika picha, kushoto ni katibu wa Wizara hiyo, Bw. Salum Salum na Mkurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Eliabi Chodota.

Kulia ni Mbunge wa Wete, Mhe. Ali Mbarouk akifuatilia kwa makini semina ya mtangamano.

Washiriki wa semina hiyo ambao wengi wao walikuwa wajasiriamali wakisikiliza hotuba ya kufunga semina.
Washiriki wengine wakifuatilia hotuba ya Mhe. waziri wa Nchi.
Mhe. Waziri wa Nchi akiendelea kuwahutubia wana semina na watu wengine waliohudhuria sherehe za ufungaji.
Picha ya pamoja kati ya Mhe. Gavu na washiriki wa semina.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Mindi Kasiga akiwasilisha mada kuhusu Diplomasia ya Umma kwa wana semina hiyo.
Wajumbe wa semina wakisikiliza mada kuhusu Diplomasia ya Umma.
Bi. Mindi akiendelea kuwasilisha mada.
Prof. Ammon Mbelle kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam akiwasilisha mada kuhusu Sera ya Mambo ya Nje kwenye semina hiyo.
Mchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Elly Chuma akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika Diplomasia yaUchumi.
Wajumbe wa Semina wakifuatilia mada.
Mjumbe wa Semina akichangia mada.
Watoa mada wakipongezwa na wajumbe wa semina.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Mambo ya Nje yatoa elimu ya Mtangamano Pemba

 Serikali ya Zanzibar imeahidi kuwa itaendelea na jitihada za kuimarisha huduma za kiuchumi kwa madhumuni ya kuweka mazingira mazuri ya kibiashara ili wananchi waweze kunufaika na fursa zinazopatikana kwenye Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Issa Gavu alipokuwa anafunga semina ya siku nne kuhusu mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake iliyofanyika Pemba kuanzia tarehe 15 hadi 18 Mei 2017.


Mhe. Gavu alitoa wito kwa wanasemina hao ambao wengi wao walikuwa ni wajasiriamali kutengeneza bidhaa zenye ubora kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia ya ulimwengu wa sasa ili ziwe na uwezo wa kushindana na bidhaa nyingine katika soko la EAC.


Aidha, Mhe. Gavu aliahidi kuwa Serikali itasaidia wajasiriamali washiriki makongamano, semina, maonesho na warsha mbalimbaili zinazofanyika nchini na nje ya nchi ili iwe fursa kwao kujifunza mambo mapya yanayoendana na ulimwengu wa sasa kwa lengo la kuboresha biashara zao.


Mhe. Gavu aliwasihi wote waliopata na watakaopata fursa za mafunzo kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ili kwa pamoja watumie mbinu, ujuzi na uzoefu wanaoupata kukabili changamoto za ushindani wa soko kulingana na mahitaji ya sasa.


Alisisitiza umuhimu wa nchi zote wanachama wa EAC kuwahudumia raia wa nchi zote kwa usawa bila ubaguzi. Alisema endapo nchi moja ikiwa na tabia ya kunyanyasa raia wa nchi nyingine inaweza kusababisha dhana ya kulipiza kisasi hatimaye vurugu na kuleta mkanganyiko katika Jumuiya. 


Vile vile, Waziri wa Nchi alitoa wito kwa nchi zote wanachama kushirikiana kwa pamoja kudhibiti biashara ya magendo. "Sio sahihi kwa nchi moja kufumbia macho biashara ya magendo kwa kutochukua hatua dhidi ya wanaoingiza na kununua bidhaa za magendo".  Mhe Gavu alisema. Zanzibar inakabiliwa na biashara ya magendo ya zao la karafuu ambayo inasafirishwa kwa njia za panya kwenda nchi za jirani.


Kwa upande wao wajasiriamali wameahidi kuwa watatumia mafunzo waliyopata kulikabili Soko la EAC bila khofu yeyote kama ilivyokuwa hapo awali.



Semina hiyo ya siku nne ilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga na ilitolewa na wataalamu wa Wizara kwa kushirikiana na Prof. Ammon Mbelle kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.

  

   -Mwisho-     
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 18 Mei, 2017

Thursday, May 18, 2017

Mkutano wa 34 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki wamalizika

Mkutano wa 34 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam umefikia tamati. Mkutano huu uliofanyika katika Hoteli ya Serena umehudhuriwa na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka nchi wanachama, watendaji mbalimbali wa Wizara, mashirika ya umma, Watendaji wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na taasisi mbalimbali za Serikali ndani ya Jumuiya. 

Pamoja na mambo mengine Mkutano huu ulikuwa ni maalum kwa ajili ya kuandaa agenda zinazohitaji maamuzi ya Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Agenda hizo zinatokana na taarifa ya utekelezaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali ya Mkutano uliopita wa Wakuu wa nchi wa Jumuiya wa mwaka 2015/2016, iliyo andaliwa na Mkutano wa ngazi ya wataalamu. 

Baadhi ya mambo yaliyopo kwenye taarifa hiyo ya utekelezaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali ya Mkutano uliopita wa Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2015/2016 ambayo imekabidhiwa kwa Baraza la Mawaziri yanajumuisha mambo yafuatayo;

·     Taarifa ya namna ya kuwezesha uundaji wa magari katika   Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupunguza uagizaji wa         magari yaliyotumika kutoka nje ya Jumuiya



· Taarifa ya mapitio kuhusu sekta ya nguo na ngozi juu ya       kuzuia/kuondoa uagizaji wa nguo na viatu vilivyotumika       kutoka nje     na;

· Taarifa ya namna endelevu ya Uchangiaji wa bajeti ya         Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na wanahabari punde baada ya mkutano amesema  Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri umekuwa  na mafanikio makubwa kwanza, kutokana na idadi kubwa na yakuridhisha ya wajumbe walioshiriki Mkutano kutoka nchi wanachama ,na pili  ni kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka miwili ambayo Tanzania ilikuwa mwenyekiti wa Jumuiya hadi sasa inapokabidhi kwa nchi ya Jamhuri ya Uganda.  

Mfanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uwenyekiti;
Waziri Mahiga ameyataja mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka miwili Tanzania ikiwa mwenyekiti wa Jumuiya kuwa ni; kuongezeka kwa nchi ya Sudan Kusini katika Jumuiya, kuboreka kwa mfumo wa elimu kwa ngazi ya elimu ya juu katika Jumuiya na kupungua kwa vikwazo vya biashara vinavyotokana na vikwazo visivyokuwa vya kiforodha ndani ya Jumuiya vilivyopelekea kurahisisha na kuhamasisha biashara katika Jumuiya.

Mkutano huu wa Baraza la Mawaziri utafuatiwa na Mkutano wa 18 wa Kaiwada  wa Wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uanaotarajiwa kufanyika tarehe 20 Mei, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam. 

Pamoja na mambo mengine Mkutano wa Wakuu wa nchi unatarajiwa kupokea ripoti ya usuluhishi ya kamati inayoongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamini William Mkapa.

Tanzania ilikabidhiwa uwenyekiti wa Jumuiya mwishoni mwa mwaka 2014 katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi uliofanyika Nairobi, Kenya; na ikapewa tena nafasi ya kuendelea kushikilia kiti hicho mwaka 2015, ambapo mpaka sasa Tanzania wakati inaelekea kukabidhi nafasi hii ya uwenyekiti kwa nchi ya Uganda, Tanzania imekuwa mwenyekiti wa Jumuiya kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo.


Waheshimiwa Mawaziri wa Tanzania waliohudhuria Mkutano wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Afrika Mashariki unapigwa kabla ya kuanza kwa Mkutano
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wamasuala ya Afrika Mashariki wa Uganda Mhe.Dkt.A.M Kirunda Kivejinja kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Aziz P. Mlima (wakwanza kushoto) akifuatilia Mkutano.


Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Pindi Chana (wakwanza kushoto) akifuatilia Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mkutano ukiwa ukiendelea, Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam






Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Komoro awasilisha Hati za Utambulisho.



Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Komoro Mhe. Sylvester M. Mabumba (kulia) akiwasili katika Ikulu ya Komoro kwaajili ya hafla ya kuwasilisha Hati za Utambulisho, kushoto ni Mnikulu  wa Ikulu ya Komoro Bw.Hashim Mohamed. Hafla ya kukabidhi Hati hizo ilifanyika mapema wiki hii katika Ikulu hiyo.



Mhe. Balozi Mabumba akijitambulisha sambamba na kutoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kabla ya kukabidhi Hati za Utambulisho.
Mhe. Balozi Mabumba akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika  Ukumbi wa Ikulu ya Komoro. Pembeni yake ni Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo Mambo ya Nje ya Komoro.


==================================================
TANZANIA NA KOMORO ZAAHIDI KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO.
Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Komoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba mapema wiki hii alikabidhi hati za utambulisho  kwa Rais wa Muungano wa Visiwa vya Komoro Mhe. Azali Assoumani. Hafla ya kukabidhi hati hizo ilifanyika kwenye Ukumbi wa Ikulu ya Komoro ijulikanayo kama  Beit.

Wakati akihutubia, Mhe. Mabumba alijitambulisha kwa Mhe. Rais na kueleza furaha yake ya kuteuliwa kuwa Balozi wa pili kutoka Tanzania kuja kutumikia nchini Komoro. Aidha, alieleza furaha yake kwa mapokezi mazuri aliyoyapata tangu kuwasili kwake Visiwani  humo na kwamba yamemfanya ajisikie yupo nyumbani.

Alieleza kuwa anatambua kazi kubwa iliyopo mbele yake na kuahidi kuwa katika kipindi chake wakati akiwa Balozi nchini humo atajitahidi kukuza mahusiano yaliyopo baina ya Tanzania na Komoro. Sambamba na hilo, Mhe. Balozi alieleza dhamira yake ya kutaka kuona mahusiano baina ya nchi hizi mbili yanakuwa na manufaa kwa pande zote halikadhalika kukua kwa uhusiano wa kindugu kwani mahusiano baina ya Tanzania na Komoro ni ya kihistoria.

Pia Mhe. Rais Assoumani katika hotuba yake naye alianza kwa kuonyesha furaha yake ya kuwasili kwa Balozi pamoja na kukiri kupokea barua ya kurejea Balozi aliyepita na ya kuwasili kwa Balozi wa sasa. Vilevile alieleza kuwa kila Mkomoro hujisikia nyumbani pindi anapo tembelea Tanzania kutokana na ukarimu wanao onyeshwa wanapokuwa huko. Aidha Mhe. Rais alimuhakikishia Mhe. Balozi kuwa atarajie kupata ushirikiano wake pamoja na wa Serikali yake katika kipindi chote atakapo kuwa nchini humo.

Mhe. Balozi Mabumba alitumia fursa hiyo pia  kumuomba Mhe. Rais Assoumani kufanye ziara ya kikazi nchini Tanzania ili kuweza kudumisha mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo mbili.

Zanzibar haibaguliwi katika EAC,

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akimkaribisha Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota kutoa mada kwenye semina ya mtangamano inayoendelea Kisiwani Pemba. Ushiriki na mwitikio katika semina hiyo umekuwa mkubwa kwa washiriki ambapo wameonekana kuvutiwa sana na semina hii pia wamekuwa wadadisi wazuri wa kutaka kujua zaidi fursa zinazo patikana kwenye mtangamano huo.
Bw. Chodota akitoa mada kwenye semina ya mtangamano inayoendelea Pemba.
Sehemu ya washiriki wakisikiliza kwa makini mada iliyokuwa ikitolewa na Bw. Chodota (hayupo pichani).
Bw. Chodota akiendelea kutoa mada yake.
Mmoja wa washiriki Bi. Kauthari akiuliza swali mara baada ya mada kumalizika kutolewa na Bw. Chodota hayupo pichani.
Sehemu nyingine ya washiriki wakimsikiliza kwa makini.
Bw. Chodota akijibu swali lililokuwa limeulizwa na Bi Kauthari (hayupo pichani).
Bw. Suleimani Haji kutoka ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar naye akitoa mada kuhusu nafasi ya Zanzibar kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sehemu ya washiriki wakimsikiliza kwa makini Bw. Suleimani (hayupo pichani).
Washiriki wakisikiliza kwa makini mada na maswali yaliyo kuwa yakiulizwa na washiriki wengine.
Mhe. Mbarouk Salim Ali Mbunge wa Jimbo la Wete akiuliza swali kwenye semina. Pembeni yake ni Mbunge wa Jimbo la Konga, Mhe. Mbarouk Ali akisikiliza kwa makini.
Meneja wa TRA kwa upande wa Kisiwani Pemba Bw. Habibu Saleh naye akiuliza swali kwa mtoa mada, Bw. Suleimani (hayupo pichani).
Bw. Salehe akijibu maswali hayo na kutolea ufafanuzi kwa baadhi ya mambo.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Zanzibar haibaguliwi katika EAC,

Serikali ya Zanzibar inashiriki moja kwa moja bila ukomo katika masuala yote ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hivyo Wazanzibari wamehimizwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Jumuiya hiyo na kuondokana na dhana kuwa eti, Serikali yao inabaguliwa.



Akiwasilisha mada leo kuhusu ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye semina ya masuala ya  mtangamano wa EAC inayofanyika Pemba, Afisa wa Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Bw. Suleima Haji alitoa ufafanuzi wa kina kuonesha namna Zanzibar inavyoshiriki katika EAC.



Bw. Haji alieleza kuwa  licha ya Zanzibar kuwa  sehemu ya muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ushiriki wake umedhihirika katika mgawanyo wa miradi ya maendeleo ya EAC, hususan miradi ya Miundombinu.  Alisema Zanzibar iliwasilisha mapendekezo ya miradi 10 kwenye Sekretarieti ya EAC na kutokana na vipaumbe vilivyowekwa miradi 3 imekubaliwa na mchakato wa kuitekeleza unaendelea. Miradi hiyo ni ujenzi wa Bandari ya  Marhubi kisiwani Pemba, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na ununuzi wa meli kubwa zitakazosafirisha abiria na mizigo kwenye nchi wanachama wa EAC.



 Aidha, kwenye miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Zanzibar haijasahaulika. Zanzibar inanufaika na miradi inayofadhiliwa na taasisi inayojihusisha na masuala ya kukuza biashara na kupunguza umasikini katika nchi za EAC inayoitwa "East Africa Trademark" (TMEA).  TMEA ambayo ni mdau mkubwa wa EAC inafadhili mradi ambao unawawezesha Wazanzibari kufanya maombi kwa njia ya mtandao ili kupata cheti cha uasili wa bidhaa. Cheti hicho ni muhimu kwa wafanyabiashara kwani kinatambulisha bidhaa yako ilipotengenezwa na kupata msamaha wa kodi ya forodha inapoingia nchi nyingine za EAC.



Mradi mwingine unaofadhiliwa na TMEA huko Zanzibar ni ule wa kuwasilisha malamiko kwa njia ya mtandao au ujumbe mfupi wa simu pale inapotokea mfanyabiashara amekumbana na vikwazo visivyo vya forodha katika kusafirisha bidhaa zake ndani ya Jumuiya. Ujumbe huo utakapopokelewa, kikwazo kilicholalamikiwa kitafanyiwa kazi na taasisi husika mara moja.


Benki ya dunia pia inaendesha mradi wa kutathmini utekelezaji wa Soko la Pamoja kwa upande wa Zanzibar. Kama inavyotambulika soko la pamoja lina vipengele vingi vikiwemo; usafirishaji huru wa bidhaa, huduma, mtaji na watu. Hivyo kuna umuhimu wa kupima namna nchi wanachama zinavyotekeleza vipengele hivyo.



Ushiriki wa Zanzibar unapatikana pia kwenye uenyeji wa taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Zanzibar imebahatika kuwa mwenyeji wa Kamisheni ya  Kiswahili ya EAC. Kuwa mwenyeji wa taasisi kuna faida kubwa zikiwemo kujitangaza na ajira. Kwa upande wa ajira, Bw. Haji alisema sio tu Wazanzibari wanafaidikia na ajira za  Kamisheni ya Kiswahili, bali wanapata ajira hata katika Sekretarieti ya EAC na kutolea mfano kuwa Mhasibu Mkuu wa kwanza wa Sekretarieti hiyo alikuwa Mzanzibari.


Vile vile, Zanzibar imekuwa mwenyeji wa vikao mbalimbali vya taasisi za Jumuiya. Mwaka 2010 Mahakama ya Afrika Mashariki ilifanya kikao chake Zanzibar, Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) lilifanya kikao chake Zanzibar mwaka 2016 na mwezi Agosti mwaka huu utafanyika mkutano mkubwa wa masuala ya Kiswahili mjini Zanzibar. Aliendelea kusema kuwa katika Bunge la EALA la kipindi hiki,  Zanzibar ina wabunge watatu, wawili wakitokea CCM na mmoja CUF.



Alihitimisha mada yake kwa kuwasihi Wazanzibari waache fikra potofu za kujihisi kubaguliwa badala yake waunganishe nguvu kuchangamkia fursa lukuki za kibiashara zilizopo kwenye mtangamano wa EAC. Alisema Serikali ya Zanzibar inashiriki katika kila jambo ikiwemo kushiriki mikutano ya Marais. Mawaziri na Wataalamu ili kutetea maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.



 -Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 18 Mei, 2017