Mawaziri wa Tanzania
na Rwanda wanaoshughulikia masuala ya miundombinu wameagizwa kukutana mara moja
kujadili ujenzi wa Reli ya kiwango cha Kimataifa kutoka Isaka hadi Rwanda.
Kauli hiyo imetolewa leo
Ikulu jijini Dar Es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mbele ya waandishi wa habari akiwa na mgeni
wake, Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame ambaye amefanya ziara ya kikazi ya siku
moja hapa nchini.
“Kipande cha kutoka
Isaka hadi Rwanda ni kilomita 400 tu, hatuwezi kushindwa kukijenga, tumewaagiza
Mawaziri wa miundombinu wakutane ili wajadili namna ya kupata fedha na kabla
mwaka huu haujaisha tunataka kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo”, Rais
Magufuli alisema.
Rais Magufuli alieleza
kuwa ujenzi wa reli hiyo utasaidia kukuza biashara kati ya Tanzania na Rwanda
ambayo kwa sasa, licha ya kuongezeka kidogo lakini kiwango cha biashara kati ya
nchi hizo bado kipo chini, akitolea mfano wa kuongezeka kwa mizigo ya Rwanda
inayopitia Bandari ya Dar Es Salaam ambayo kwa mwaka jana imefikia idadi ya
tani laki tisa na nusu.
Rais Magufuli ambaye
alimtaja Rais Kagame kuwa ni mwanamapinduzi wa Afrika, licha ya kumpongeza kwa
kushinda kiti cha Rais kwa ushindi wa kishindo mwaka 2017 alimsifu pia kutokana
na mipango yake ya kuibadilisha Rwanda na dhamira ya dhati ya kuwaletea
maendeleo wananchi wa nchi hiyo. “Watanzania na watu wengine wanajua Rwanda
ilipotoka na hatua ulioifikisha hivi sasa”, Rais Magufuli alisema.
Katika ziara hiyo,
Rais Magufuli alimuhakikishia Rais Kagame anayewania nafasi ya Mwenyekiti wa
Umoja wa Afrika (AU) kwa kipindi cha Mwaka 2018 kuwa Tanzania pamoja na marafiki
zake itamuunga mkono kwenye nafasi hiyo. Mhe. Rais alielezea matumaini yake
kuwa Rais Kagame atatumia nafasi yake hiyo kwa kushirikiana na viongozi wenzake
kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazolikabili Bara la Afrika ikwemo
ukosefu wa ajira unaosabisha vijana wengi kukimbia nchi zao.
Kwa upande wake, Rais
Kagame alielezea matumaini yake kuwa Tanznaia itaendelea kushirikiana na Rwanda
katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi kwa faida ya pande zote mbili.
Akijibu swali kuhusu hatua
gani atazichukuwa atakapokuwa Mwenyekiti wa AU kukabiliana na wimbi la vijana
wengi wa Afrika kukimbilia ughaibuni kutafuta maisha.
Rais Kagame alijibu kuwa
nchi moja moja na kwa ujumla wao barani Afrika ziongeze biashara na uwekezaji baina
yao ili kuongeza ajira kwa vijana. Aidha, aliwaasa vijana kuwa jukumu la
Serikali zote duniani ni kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara,
hivyo vijana hawanabudi kutumia fursa zinazopatikana katika nchi zao badala ya
kukimbilia ughaibuni na kutangatanga.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
14 Janauri 2018
|