Friday, April 12, 2019

Wasomi watoa maoni kuhusu EPA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wasomi watoa maoni kuhusu EPA

Dodoma, 12 Aprili, 2019.

Tanzania imeshauriwa kufanya tathmini ya kina kuhusu faida na hasara za kusaini Mkataba wa Ubia wa kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU) unaojulikana kwa kifupi EPA.

Ushauri huo umetolewa na mbobezi wa masuala ya uchumi na mtangamano wa kikanda kutoka Ujerumani, Prof. Helmut Asche, alipokuwa anatoa muhadhara kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kuhusu changamoto za kutekeleza Mkataba wa EPA. Muhadhara huo umeratibiwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na UDOM ulifanyika tarehe 12 Aprili, 2019.

Prof. Asche alieleza kuwa, kutokana na kiwango cha uchumi wa Tanzania, Serikali itakuwa katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi ukizingatia kuwa nchi haiwezi kujitenga na biashara za kimataifa kutokana na umuhimu wake, ingawa kwa upande mwingine, zina gharama zake.

Prof. Asche alihitimisha muhadhara wake kwa kuitaka Serikali ya Tanzania kulishughulikia suala hili kwa umakini mkubwa huku ikizingatia hoja zifuatazo ambazo ni faida au madhara yatakayotokea endapo Tanzania itasaini au kutosaini Mkataba wa EPA; na hatua za kuchukua ili nchi zote za EAC zishawishike kusaini mkataba huo.

Akichangia mjadala huo, mtaalam wa uchumi na kilimo, Prof. Adam Mwakalobo, alieleza kuwa, kabla ya nchi haijachukua uamuzi wa kusaini Mkataba huo, kuna umuhimu wa kufanya utafiti wa kina ili kujua faida na hasara nchi inazoweza kupata. Alisema nchi inaweza kuingia katika mkataba huo hatua kwa hatua na pasipo kuwa na hofu kwa kuwa nchi nyingine za Asia ambazo leo zimepiga hatua kubwa ya maendeleo, zilisaini mikataba kama hiyo kwa awamu.

Mchangiaji mwingine katika mada hiyo, Dkt. Cyril Chami, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, katika Serikali ya Awamu ya Nne, alibainisha masuala kadhaa ambayo yachukuliwe kama tahadhari kwa timu ya wataalamu inayofanya majadiliano ya mkataba huo.

Masuala hayo yamejikita katika utofauti mkubwa wa uchumi wa nchi za EAC na EU katika maneno ya pato la wastani kwa mtu mmoja (per capita income), wastani wa ukubwa wa uchumi wa jumuiya hizo mbili katika uchumi wa dunia kwa jumla, wastani wa bidhaa nchi za EAC inazouza EU na zile inazonunua, kiwango cha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchi za EAC na EU, maendeleo ya viwanda na pato linalotokana na ushuru wa forodha.
Kwa upande wake, Dkt. Godfrey Sansa, alisisitiza umuhimu wa kufanya majadiliano kwenye vipengele vya mkataba ambavyo nchi za EAC zina mashaka navyo kwa lengo la kupata  muafaka pasipo kuwekeana ukomo wa muda. Aidha, alisema kwenye mkataba kuwepo na kipengele cha kuruhusu kupitia upya mkataba huo kila baada ya muda fulani, kwa vile vipengele ambavyo utekelezaji wake vimeonekana vina madhara kwa nchi.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo  ya  Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, akisalimiana na Profesa Helmut Asche ambaye ni mtaalam wa masuala ya uchumi, sayansi ya jamii na mtangamano wa kikanda mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Cive, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).  Profesa Asche ambaye ni raia wa Ujerumani amefanya mudhara wa umma kuhusu  manufaa na chagamoto za Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi (Economic Partnership Agreement -EPA) baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EAC).

Mwenyekiti wa muhadhara huo, Profesa Flora Fabian akimkaribisha Profesa  Helmut Asche kuwasilisha mada kuhusu manufaa na changamoto za Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya nchi wanachama wa EAC na EU.
Profesa Helmut Asche akiwasilisha mada hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt Faraji Kasidi Mnyepe (wa kwanza kushoto) akifuatilia mada hiyo. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Edwin Mhede.
Mtaalam wa Uchumi na Takwimu, Dkt. Cyril Chami, akichangia mada hiyo.
Mtaalam wa Sayansi ya Siasa, Dkt. Godfrey Sansa akichangia mada hiyo.
Mmoja kati ya washiriki wa mkutano huo akiuliza swali.
Maswali yanaendelea.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Kasidi Faraji Mnyepe, akiteta jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Jestas Nyamanga, mara baada ya muhadhara huo kumalizika.
Profesa Helmut Asche (wa kwanza kushoto), Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Edwin Mhede (wa pili kushoto);Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Jestas Nyamanga (wa tatu kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Kasidi Faraji Mnyepe wakibadilishana mawazo mara baada ya muhadhara huo wa umma kumalizika.



Prof. Kabudi afungua rasmi Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma. Ufunguzi wa ofisi hizo umefanyika tarehe 12 Aprili 2019 na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Joseph Kakunda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri anayeshughulikia uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki, Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Mussa Azan Zungu, Mzee Job Lusinde na Meya wa Jiji la Dodoma, Mhe. Prof. Davis Mwamfupe. Katika hotuba yake, Mhe. Prof. Kabudi ameupongeza Ubalozi wa China hapa nchini kwa uamuzi wa kufungua ofisi hizo na kuwataka wakazi wa Dodoma na wananchi kwa ujumla kuzitumia ofisi hizo kwa ajili ya kujiimarisha kibiashara na uwekezaji.
Sehemu ya viongozi waliohudhuria ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (hayupo pichani) alipohutubia hafla hiyo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akitoa hotuba yake

Sehemu ya wageni waalikwa nao wakifuatilia hotuba ya Prof. Kabudi (hayupo pichani wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Caesar Waitara na kushoto ni Bw. Charles Mbando, Katibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Sehemu ya ujumbe wa China wakifuatilia hotuba ya Mhe. Prof. Kabudi (hayupo pichani)
Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke akizungumza wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi huo jijini Dodoma. Mhe. Wang Ke alisema kuwa ufunguzi wa Ofisi hizo ni kuunga mkono kwa dhati mpango wa Serikali ya Tanzania wa kuhamia makao makuu ya nchi uliotangazwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania
Wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Balozi wa China nchini (hayupo pichani)
Sehemu nyingine ya wageni waalikwa wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma
Hafla ikiendelea
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hotuba ya Balozi Wang Ke (hayupo pichani)
Aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini China kuanzia mwaka 1975 hadi 1984  Balozi Mstaafu, Mzee Job Lusinde akizungumza machache kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na China wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma
Mhe. Mussa Azan Zungu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambaye alimwakilisha Spika wa Bunge kwenye hafla hiyo naye akipongeza uamuzi wa China wa kufungua ofisi za Ubalozi jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi kwa pamoja na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke wakifunua kitambaa kuashiria ufunguzi rasmi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma
 Mhe. Prof. Kabudi na Mhe. Balozi Wang Ke pamoja na viongozi wengine wakifurahia baada ya ufunguzi rasmi wa Ofisi za Ubalozi wa China jijini Dodoma.





Profesa Kabudi amekutana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hiyo. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wa kwanza kulia akimwelezea jambo Prof. Palamagamba John Kabudi, wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi. 

Waziri wa Mabo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi wa Pili kutoka Kushoto akielezea msimamo wa Wizara yake katika kuzitangaza fursa za Uwekezaji zilizopo Zanzibar. Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mwinyi.

Profesa Palamagamba John Kabudi wa Pili kutoka Kushoto akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
=====================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi  (Mb.) amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuwa Taifa moja linaloendelea kudumu muda wote kutokana na misingi imara iliyowekwa na Waasisi wa Taifa hilo.
Amesema yapo Makabila mengi katika Mikoa na Wilaya mbali mbali Nchini lakini muungano wa lugha moja inayozungumzwa na Wananchi wake Bara na Zanzibar imekuwa mfano kwa Mataifa mengine Duniani.
Profesa Palamagamba John Kabudi ameeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Ameongeza kuwa yapo Mataifa mengi Duniani yaliyowahi kuunganisha Nchi zao akitolea Mfano iliyokuwa Yugoslavia na sasa imesambaratika pia Senegal na Gambia kwa upande Afrika lakini zimeshindwa kuendeleza Muungano wao.
Waziri Palamagamba John Kabudi alisema wakati Serikali zote mbili zikiendelea kuheshimu kwa kuweka Kumbukumbu za Waasisi hao ambao ni Hayati Mzee Abeid Amani Karume na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Vizazi vya sasa vinapaswa kujifunza tabia ya Viongozi hao walioacha misingi imara ya kitaifa. 

Akigusia suala la Diplomasia ya Uchumi ambayo kwa sasa Tanzania imeelekeza nguvu zake kupitia Balozi zake zilizoko nje ya mipaka ya Tanzania Profesa Palamagamba John Kabudi amesema Serikali inaendeleza mfumo wa kushawishi Wawekezaji ili kuunga mkono jitihada za Taifa za kuwa na Tanzania ya Viwanda ifikapo Mwaka 2025.
Amesema mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa Kuimarisha Uchumi wake unapaswa kuungwa mkono na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika muelekeo wa kuelekea kwenye Maendeleo ya haraka.
Akigusia Sekta ya Utalii kufanya vyema Zanzibar, Waziri Palamagamba amesema Sekta hiyo ni muhimu hivi sasa kwa mapato ya Taifa na nilazima iwekewe utaratibu wa pamoja utakaosaidia kuuza haiba ya pande zote mbili za Muungano.
Alisema vipo vivutio vinavyopaswa kutangazwa kwa pamoja Bara na Zanzibar ambavyo vinaweza kutoa nguvu ya ushawishi wa Watalii kufanya ziara ya kutembelea sehemu zote mbili kwa wakati mmoja.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alielezea faraja yake kutokana na Zanzibar kupiga hatua kubwa katika kuimarisha Sekta ya Utalii inayotoa ajira kubwa hasa kwa Vijana.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ushawishi wa Uwekezaji ndani ya Visiwa vya Zanzibar unapaswa kuungwa mkono na Ofisi zote za Kibalozi za Tanzania zilizopo Mataifa mbali mbali Duniani.
Alisema Zanzibar ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ushawishi wake kwa Wawekezaji na Mataifa ya kigeni unawajibika kusimamiwa na Mabalozi wa Tanzania kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi Seif alimueleza Profesa Palamagamba John Kabudi kwamba Zanzibar kupitia Viongozi wake wote waliopita na waliopo hivi sasa bado wanaendeleza sera na Mikakati iliyoachwa na Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani Karume.
Alisema uimarishaji wa Miundombinu ya Mawasiliano, Ujenzi wa Nyumba za Kisasa za Maendeleo, Afya, Elimu pamoja na huduma za Maji safi na salama ni miongoni mwa Sekta zinazoendelea kuimarishwa na Viongozi wote.
Balozi Seif Ali Iddi alimweleza Profesa Palamagamba John Kabudi, kuwa Miradi iliyobuniwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo ujenzi wa Miji Mipya kama ule wa Ng’ambo tuitakayo katika eneo la Kwahani na Mtaa wa Chumbuni imelenga kustawisha maisha ya Wananchi wake ili kuachana na matumizi mabaya ya Ardhi ndogo iliyopo visiwani humo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
12 Aprili, 2019.