TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi (Mb.) amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuwa Taifa moja linaloendelea kudumu muda wote kutokana na misingi imara iliyowekwa na Waasisi
wa Taifa hilo.
Amesema
yapo Makabila mengi katika Mikoa na Wilaya mbali mbali Nchini lakini
muungano wa lugha moja inayozungumzwa na Wananchi wake Bara na Zanzibar
imekuwa mfano kwa Mataifa mengine Duniani.
Profesa
Palamagamba John Kabudi ameeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha
baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe
Magufuli kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Ameongeza kuwa yapo Mataifa mengi Duniani yaliyowahi kuunganisha Nchi zao akitolea Mfano
iliyokuwa Yugoslavia na sasa imesambaratika pia Senegal na Gambia kwa upande Afrika lakini
zimeshindwa kuendeleza Muungano wao.
Waziri Palamagamba John Kabudi alisema wakati Serikali zote mbili zikiendelea
kuheshimu kwa kuweka Kumbukumbu za Waasisi hao ambao ni Hayati Mzee Abeid Amani Karume
na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Vizazi vya sasa vinapaswa kujifunza
tabia ya Viongozi hao walioacha misingi imara ya kitaifa.
Akigusia
suala la Diplomasia ya Uchumi ambayo kwa sasa Tanzania imeelekeza nguvu zake
kupitia Balozi zake zilizoko nje ya mipaka ya Tanzania Profesa Palamagamba John Kabudi amesema
Serikali inaendeleza mfumo wa kushawishi Wawekezaji ili kuunga mkono jitihada
za Taifa za kuwa na Tanzania ya Viwanda ifikapo Mwaka 2025.
Amesema mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa Kuimarisha Uchumi
wake unapaswa kuungwa mkono na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania katika muelekeo wa kuelekea kwenye Maendeleo ya haraka.
Akigusia
Sekta ya Utalii kufanya vyema Zanzibar, Waziri Palamagamba amesema
Sekta hiyo ni muhimu hivi sasa kwa mapato ya Taifa na nilazima iwekewe utaratibu wa
pamoja utakaosaidia kuuza haiba ya pande zote mbili za Muungano.
Alisema
vipo vivutio vinavyopaswa kutangazwa kwa pamoja Bara na Zanzibar ambavyo
vinaweza kutoa nguvu ya ushawishi wa Watalii kufanya ziara ya
kutembelea sehemu zote mbili kwa wakati mmoja.
Waziri
huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alielezea faraja yake
kutokana na Zanzibar kupiga hatua kubwa katika kuimarisha Sekta ya Utalii inayotoa ajira kubwa hasa kwa Vijana.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema
ushawishi wa Uwekezaji ndani ya Visiwa vya Zanzibar unapaswa kuungwa mkono na
Ofisi zote za Kibalozi za Tanzania zilizopo Mataifa mbali mbali Duniani.
Alisema
Zanzibar ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ushawishi wake
kwa Wawekezaji na Mataifa ya kigeni unawajibika kusimamiwa na Mabalozi wa
Tanzania kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Balozi
Seif alimueleza Profesa Palamagamba John Kabudi kwamba Zanzibar kupitia Viongozi wake wote
waliopita na waliopo hivi sasa bado wanaendeleza sera na Mikakati iliyoachwa na
Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani Karume.
Alisema
uimarishaji wa Miundombinu ya Mawasiliano, Ujenzi wa Nyumba za Kisasa za
Maendeleo, Afya, Elimu pamoja na huduma za Maji safi na salama ni miongoni mwa
Sekta zinazoendelea kuimarishwa na Viongozi wote.
Balozi
Seif Ali Iddi alimweleza Profesa Palamagamba John Kabudi, kuwa Miradi iliyobuniwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo ujenzi wa Miji Mipya
kama ule wa Ng’ambo tuitakayo katika eneo la Kwahani na Mtaa wa Chumbuni
imelenga kustawisha maisha ya Wananchi wake ili kuachana na matumizi mabaya ya
Ardhi ndogo iliyopo visiwani humo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
12 Aprili, 2019.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.