Wednesday, April 3, 2019

Ujumbe wa Libya wakutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje Prof. Palamagamba Kabudi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi akiwa katika mazungumzo na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Libya Mhe. Jamal El Barak


=======================================

Tanzania na Serikali ya Umoja ya Libya, zimekubaliana kuingia katika mazungumzo ya kina yenye lengo la kupitia miradi yote na uwekezaji,  iliyokuwa ikifanywa na Serikali ya Libya hapa nchini kabla ya machafuko nchini humo na pia kuangalia maeneo mapya ya uwekezaji ambayo Libya imeonesha nia ya kutaka kuwekeza chini ya Kamati ya pamoja baina ya nchi hizo mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa mazungumzo na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Libya na kuongeza kuwa baada ya hali ya Libya kutengemaa na Amani kuongezeka wamekubaliana kuingia katika uwekezaji.

“Nimemueleza mgeni wangu kuwa mwaka huu wa 2019 Tanzania tumeutangaza kuwa ni mwaka wa uwekezaji na yeye ameonesha nia ya nchi yake na makampuni ya Libya kutaka kuja kuwekeza hapa nchini,tumejadili pia jinsi ya kufufua kamati ya pamoja kati ya Libya na Tanzania kwakuwa mkutano wa mwisho ulifanyika mwaka 2000 baada ya Kamati hiyo kukutana sasa tutajadili miradi mbalimbali ambayo Libya imewekeza,mitaji iliyoiwekeza lakini pia tutaangalia maeneo mapya wanayopendekeza kuwekeza”

Aidha Profesa Palamagamba John Kabudi amefafanua kuwa lengo jipya katika sheria za uwekezaji Tazania ni kuhakikishia Nchi inakuwa na mfumo wa sheria na uwekezaji ambao kila upande unapata tofauti na mfumo wa zamani ambao wawekezaji walikuwa wakinufaika na nchi inanyonywa.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe kutoka Libya Mhe. Jamal El Barak amesema wamekuja dhumuni la ujumbe wao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ni kumjulisha kuwa Serikali ya Umoja wa Libya iko tayari kufufua na kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizo baada ya hali ya Amani kutengemaa nchini Libya kutokana na mahusiano ya Tanzania na Libya kuwa ya kihistoria.

Mbali na hayo Mhe Jamal El Barak ameongeza kuwa Libya iko tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali za uwekezaji kwa kuwa wanatambaua mazingira ya uwekezaji Tanzania ni mazuri hasa baada ya kuhakikishiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki kuwa mazingira ya uwekezaji yameboreshwa.

Si mara yetu ya kwanza kuwekeza hapa nchini,kabala ya machafuko nchini mwetu tulikuwa tumewekeza katika sekta mbalimbali na sasa tutaangalia maeneo mapya ya uwekezaji”

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.