TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wasomi watoa maoni kuhusu EPA
Dodoma, 12 Aprili, 2019.
Tanzania imeshauriwa kufanya tathmini ya kina
kuhusu faida na hasara za kusaini Mkataba wa Ubia wa kiuchumi kati ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU) unaojulikana kwa kifupi EPA.
Ushauri huo umetolewa na mbobezi wa masuala ya
uchumi na mtangamano wa kikanda kutoka Ujerumani, Prof. Helmut Asche, alipokuwa
anatoa muhadhara kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kuhusu
changamoto za kutekeleza Mkataba wa EPA. Muhadhara huo umeratibiwa kwa
ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
na UDOM ulifanyika tarehe 12 Aprili, 2019.
Prof. Asche alieleza kuwa, kutokana na kiwango cha
uchumi wa Tanzania, Serikali itakuwa katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi
ukizingatia kuwa nchi haiwezi kujitenga na biashara za kimataifa kutokana na
umuhimu wake, ingawa kwa upande mwingine, zina gharama zake.
Prof. Asche alihitimisha muhadhara wake kwa kuitaka
Serikali ya Tanzania kulishughulikia suala hili kwa umakini mkubwa huku ikizingatia
hoja zifuatazo ambazo ni faida au madhara yatakayotokea endapo Tanzania
itasaini au kutosaini Mkataba wa EPA; na hatua za kuchukua ili nchi zote za EAC
zishawishike kusaini mkataba huo.
Akichangia mjadala huo, mtaalam wa uchumi na
kilimo, Prof. Adam Mwakalobo, alieleza kuwa, kabla ya nchi haijachukua uamuzi
wa kusaini Mkataba huo, kuna umuhimu wa kufanya utafiti wa kina ili kujua faida
na hasara nchi inazoweza kupata. Alisema nchi inaweza kuingia katika mkataba
huo hatua kwa hatua na pasipo kuwa na hofu kwa kuwa nchi nyingine za Asia
ambazo leo zimepiga hatua kubwa ya maendeleo, zilisaini mikataba kama hiyo kwa
awamu.
Mchangiaji mwingine katika mada hiyo, Dkt. Cyril
Chami, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, katika Serikali ya
Awamu ya Nne, alibainisha masuala kadhaa ambayo yachukuliwe kama tahadhari kwa
timu ya wataalamu inayofanya majadiliano ya mkataba huo.
Masuala hayo yamejikita katika utofauti mkubwa wa
uchumi wa nchi za EAC na EU katika maneno ya pato la wastani kwa mtu mmoja (per
capita income), wastani wa ukubwa wa uchumi wa jumuiya hizo mbili katika uchumi
wa dunia kwa jumla, wastani wa bidhaa nchi za EAC inazouza EU na zile
inazonunua, kiwango cha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchi za EAC na EU,
maendeleo ya viwanda na pato linalotokana na ushuru wa forodha.
Kwa upande wake, Dkt. Godfrey Sansa, alisisitiza
umuhimu wa kufanya majadiliano kwenye vipengele vya mkataba ambavyo nchi za EAC
zina mashaka navyo kwa lengo la kupata
muafaka pasipo kuwekeana ukomo wa muda. Aidha, alisema kwenye mkataba
kuwepo na kipengele cha kuruhusu kupitia upya mkataba huo kila baada ya muda
fulani, kwa vile vipengele ambavyo utekelezaji wake vimeonekana vina madhara
kwa nchi.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki,
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, akisalimiana na Profesa Helmut Asche ambaye ni mtaalam wa masuala ya uchumi, sayansi ya jamii na mtangamano wa kikanda mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Cive, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Profesa Asche ambaye ni raia wa Ujerumani amefanya mudhara wa umma kuhusu manufaa na chagamoto za Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi (Economic Partnership Agreement -EPA) baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EAC).
Mwenyekiti wa muhadhara huo, Profesa Flora Fabian akimkaribisha Profesa Helmut Asche kuwasilisha mada kuhusu manufaa na changamoto za Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya nchi wanachama wa EAC na EU. |
Profesa Helmut Asche akiwasilisha mada hiyo.
Mtaalam wa Uchumi na Takwimu, Dkt. Cyril Chami, akichangia mada hiyo. |
Mtaalam wa Sayansi ya Siasa, Dkt. Godfrey Sansa akichangia mada hiyo. |
Mmoja kati ya washiriki wa mkutano huo akiuliza swali. |
Maswali yanaendelea. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.