Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akizungumza jambo mara baada ya kuzindua maabara hiyo ya upimaji wa udongo. |
Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akizungumza jambo mara baada ya kuzindua maabara hiyo ya upimaji wa udongo. |
Na Mwandsihi Wetu, Arusha
TEKNOLOJIA ya maabara ya kupima afya ya udongo kwa kutumia gari maalumu lenye uwezo kupima zaidi ya sampuli 100 za udongo kwa siku moja limezinduliwa hapa nchini ili kupima udongo na kumhakikishia mkulima uzalishaji wa mazao kwa wingi na yenye tija sokoni.
Uzinduzi wa Teknolojia hiyo kutoka nchini Uholanzi ulifanyika jijini Arusha kati ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania Bw.Abdallah Ulega kwa niaba ya Tanzania na Makamu Waziri wa Kilimo na Ubora wa Chakula wa Uholanzi, Bi.Marjolijn Sonnema kwa niaba ya nchi yake ili kufanikisha mageuzi katika sekta ya kilimo.
Akizungumza mara baada ya kufanya uzinduzi wa teknolojia hiyo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Bw Ulega aliishukuru Serikali ya Uholanzi kwa kutoa teknolojia yake kwa Tanzania na kusema kuwa itasaidia kuleta mapinduzi katika uzalishaji mazao.
“Kupima afya ya udongo inatoa majibu juu ya ubora wa ardhi husika, mazao yanayofaa kulimwa katika eneo hilo, kiwango cha mbolea kinachotakiwa na kutoa makadirio ya kiwango cha mavuno katika eneo husika,” alisema Naibu Waziri Ulega.
Aliongezea kuwa gharama ya kupima shamba iliyowekwa ya shilingi 25,000 mpaka 30,000 wakulima wanaweza kumudu na kuwataka wapema mashamba yao kabla ya kufanya kilimo ili kujua matatizo yaliyopo kwenye ardhi yake na nini afanye ili tija ya uzalishaji iongezeke.
“Teknolojia hii imeletwa kwetu hivyo tunakila sababu ya kuhamasisha wakulima nchini kupima mashamba yao ili wajipatie uhakika wa zao lilalofaa katika ardhi yake na nini afanye katika kuboresha ili aweze kuongeza tija ya uzalishaji,” alisema.
Naibu Waziri Ulega aliesema kuwa mageuzi katika sekta ya kilimo yatapatikana kupitia teknolojia hii ya kupima afya ya udongo na kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo hali itakayochochea ujenzi wa viwanda vya kuchakata na kuongezea thamani ya mazao.
“Ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kunachochea kasi ya maendeleo kwa kuibua teknolojia na ujuzi mbalimbali katika kuiletea nchi maendeleo, naipongeza kampuni ya Life Support System Tanzania (LSSL) kwa kuwekeza kwenye ketnolojia hii,” alisema Ulega Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa LSSL, Dkt.Edmond Matafu alisema magari manne yapo tayari pamoja na handheld soil scanner 100 ambazo zitatumiwa na maafisa ugani kwa ajili ya kuchukua sampuli za udongo katika maeneo ya vijiji kote nchini.
“Hii itasaidia kufanya zoezi la kupima afya ya udongo kwa wakati pasipo kuchelewa kipindi cha kulima ambapo itampa unafuu mkulima kujua mahitaji katika shamba lake ili aweze kupata tija katika uzalishaji mazao,” alisema Dkt. Matafu.
Aliongezea kuwa juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa kati na viwanda zitatekelezeka kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha vikwazo vyote vinavyokwamisha maendeleo vinatatuliwa ili maendeleo tunayoyatarajia yaweze kufikiwa kwa vitendo.
“Zoezi la kupima afya ya udongo litafanyika kote nchini kwani tumejipanga vizuri katika kutoa huduma hii kwa wakulima hivyo ushirikiano ndio kitu muhimu katika kufanikisha zoezi hili ambalo litakwenda kuinua hali ya uzalishaji zao nchini,” alisema Dkt. Matafu.
Uzinduzi wa Maabara ya kupima udongo kwa kutumia gari maalum ulishuhudiwa na Makamu Waziri wa Kilimo na Ubora wa Chakula kutoka Uholanzi, Bi. Marjolijn Sonnema, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania
Joroen Verheul, Katibu Mkuu Wizara ya Mifungo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini, Bw. Geoffrey Kirenga.