Wednesday, May 13, 2020

MHE.PROF. PALAMAGAMBA KABUDI AWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

  
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi awasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2020/2021. 

Wizara imeliomba Bunge liiidhinishie jumla ya Shilingi bilioni mia moja tisini na tisa, milioni mia saba hamsini, laki sita themanini na nne elfu (199,750,684,000) zikiwa ni fedha kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na  bajeti ya miradi ya maendeleo.
 

Akiwasilisha makadirio hayo, Mhe. Prof. Kabudi ameelezea mafaniko ambayo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeyapata katika kipindi hiki cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano 2015-2020.
            Mafanikio hayo ni: 
 * Ufunguzi wa Balozi mpya nane katika nchi za Qatar; Uturuki; Sudan; Cuba; Israel; Algeria; Jamhuri ya Korea; na Namibia;  
* Kuifanya lugha ya Kiswahili kutumika katika Jumuiya ya Kimataifa na nchi mbalimbali;
* Kufanikisha kufanyika kwa viwango vya juu Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Dar es Salaam mwezi Agosti 2019;
*Kuhamasisha watalii kuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii;
*Kufanikisha uenyekiti wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo mwezi Machi 2016 nchi yetu iliteuliwa kwa mara ya pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo;
*Kuratibu Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic (Africa - Nordic Foreign Ministers’ Meeting) uliofanyika kwa mafanikio makubwa mwezi Novemba 2019 jijini Dar es Salaam;
*Kufanikisha ujumuishwaji wa miradi ya Tanzania katika miradi ya kipaumbele ya miundombinu iliyoidhinishwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
*Kutekeleza Itifaki ya Umoja wa Forodha na Itifaki ya Soko la Pamoja za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
Mafanikio mengine ni pamoja na;
*Kuratibu upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato jijini Dodoma na upatikanaji wa mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 180 kutoka Benki hiyo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya pete katika jiji la Dodoma na
* Kushawishi nchi marafiki kutufutia madeni, kuyapunguza au kuweka masharti nafuu ya kuyalipa.

   
  

HOTUBA YA BAJETI 2020/202

Saturday, May 9, 2020

SERIKALI: DAWA YA COVID 19 KUTOKA MADAGASCAR NI KWA AJILI YA UTAFITI KWANZA


Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema kuwa dawa ambayo nchi ya Madagascar imeitoa kama msaada kwa Serikali ya Tanzania ni kwa ajili ya utafiti kwanza.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewaambia waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuwa dawa hiyo inayojulikana kaitaalamu kama "COVIDORGANICS" ni kwa ajili ya utafiti na siyo kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

"Huu mzigo (dawa) ni kwaajili ya kufanyiwa utafiti…….na kazi kubwa tunayoianza leo ni na wataalamu wetu wa afya ni kufanya utafiti," Amesema Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameongeza kuwa dawa hiyo siyo kwa ajili ya kugawa kwa wananchi, bali ni kwa ajili ya utafiti na mara baada ya utafiti kukamilika wataalamu wa afya watatoa maelekezo ya jinsi ya utumiaji wa dawa hiyo.

Aidha, dawa hiyo imegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza la dawa ni kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya COVID 19 kwa wale ambao hawajaambukizwa ugonjwa wa Corona. Kundi la pili ni kwa ajili ya matibabu kwa wananchi ambao tayari wameathirika na COVID 19.

"Dawa hii tuliyokuja nayo jana kutoka Madagascar mara baada ya utafiti kukamilika na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wetu wa afya itatumika kukinga wananchi ambao hawajaathirika na kutibu wale walioathirika," Prof. Kabudi

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa serikali Prof. Abel Makubi amesema kuwa mara baada ya kupokea dawa hiyo kazi ya kwanza ya ni kuanza utafiti ambao utaonesha kama dawa hiyo ni salama na haina madara kwa wananchi na pili utafiti wa kuangalia ubora wa kutibu au kupunguza makali ya COVID 19.

"Mara baada ya utafiti wa dawa hii kukamilika itatumika katika makundi matatu ambayo kundi la kwanza ni wagonjwa kutumia dawa ya kawaida, kundi la pili watapata dawa ya kawaida na hii iliyotoka Madagascar na kundi la tatu wagonjwa watatumia dawa ya kawaida na ile inayozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr)," Amesema Prof. Makubi

Prof. Makubi pamoja na mambo mengine, ametoa wito kwa watanzania kuchukua tahadhari katika kujikinga na ugonjwa wa COVID 19 na wasibweteke na lolote.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) Prof. Yunus Mgaya amesema kuwa Nimr imejipanga kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali hasa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kuhakikisha inafanya utafiti wa kina juu ya matumizi ya dawa hiyo. 

"Nimr inafanya tafiti mbalimbali za kupambana na ugonjwa huu wa COVID 19 na itaendelea kufanya tafiti hizo ili kuwasaidia watanzania," amesema Prof. Mgaya

Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu inalo jukumu lakuchunguza dawa au sumu zozote kwenye sampuli, kukadiria kwa usahihi kiasi cha dawa, umetaboli au sumu.

Drkt. Mafumiko ameongeza kuwa, kupitia utafiti wa dawa hiyo, ofissi yake kwa kushirikiana na wataalamu wa afya watatafsiri matokeo ya uchunguzi katika dawa hiyo kutoa maelekezo sahihi juu ya matumizi yake kwa mwananchi.

Mkutano huu ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), Mganga Mkuu wa serikali Prof. Abel Makubi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) Prof. Yunus Mgaya, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Tiba za Asili Dkt. Paul Mkama.   


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) dawa ambayo imetolewa na Madagascar leo Jijini Dae es Salaam



Mganga Mkuu wa serikali Prof. Abel Makubi akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dae es Salaam



Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Prof. Yunus Mgaya akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dae es Salaam



Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano  



Mkuu wa Kitengo cha Tiba za Asili Dkt. Paul Mkama akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati mkutano ukiendelea 




Wednesday, May 6, 2020

SERIKALI YAENDELEA KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZINAZOJITOKEZA MIPAKANI


 Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema changamoto zinazojitokeza katika mipaka mbalimbali ya Tanzania wakati wa usafirishaji wa bidhaa hususan katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 zinaendelea kutatuliwa kwa majadiliano.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert Ibuge ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania Nchini Zambia Mhe. Benson Keith Chali ili kuangalia namna ya kutatua changamoto mbalimbali za usafirishaji wa bidhaa hususani zile zinazotoka katika bandari ya Dar es Salaam kuelekea katika nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC.

Ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha janga la COVID – 19 unaosababishwa na virusi vya Corona changamoto mbalimbali zimejitokeza katika utoaji wa huduma za usafirishaji wa huduma na bidhaa mbalimbali na hivyo serikali inafanya jitihada za majadiliano na baadhi ya nchi katika mipaka ili kutatua changamoto zinazojitkeza na kuwezesha huduma ya usafirishaji kuendelea bila ya vikwazo.

Nae Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Mhe. Chali amemuahidi Balozi Kanali Ibuge kuwa Serikali ya Zambia imeshaanza kuzifanyia kazi changamoto zinazojitokeza. "Suala hili limeshaanza kufanyiwa kazi na kila kitu kitakuwa sawa hivi karibuni," amesema Balozi, Chali.  

Katika tukio jingine Balozi Kanali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi ambapo katika mazungumzo hayo wameongelea zaidi namna ya kushirikiana na kuwezesha kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa wawekezaji wadogo na wakati wa Tanzania na kuwa na ubia na wawekezaji wakubwa hususani katika kipindi hiki cha COVID – 19 na baada ya COVID – 19 ili kuunusuru uchumi wa Taifa kuanguka.

"Tumekubaliana kuongea ushirikiano katika sekta za afya, maji, maendeleo na uwekezaji …….kwa hili tunawashukuru sana UNDP kwa kazi wanayoifanya lakini pia hata katika ushirikiano wa kisera tumekuwa tukishirikiana nao jambo ambalo linazidi kuimarisha uhusiano wetu hasa katika wakati huu wa COVID - 19 kwani jambo hili linasaidia kunusuru uchumi wa taifa kuanguka," amesema Balozi, Kanali Ibuge. 

Katika hatua nyingine, Balozi Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Balozi wa Uingereza nchini Bi. Sarah Cooke pamoja na Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania Bw. Zlatan Milišić ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano hususani katika kipindi hiki cha janga la COVID – 19.

Tarehe 6 Aprili, 2020 ulifanyika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulijadili janga la COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona. Mkutano huo ulihusisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha,Viwanda,Biashara, Utalii, Mambo ya Ndani na Uchukuzi, kutoka nchi 16 wanachama wa SADC.  

Katika mkutano huo, Baraza la Mawaziri lilitoa mwongozo kuhusu Usafirishaji wa Bidhaa Muhimu na Huduma katika Nchi za SADC katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona. Mwongozo huu unatumika katika kipindi hiki unalenga kupunguza safari zisizo za lazima na kuwezesa usafirishaji wa bidhaa muhimu wakati huu wa janga la COVID - 19.



  Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge akimueleza jambo Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam

Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam



Balozi wa Zambia nchini Mhe. Benson Keith Chali akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge akiongea na Balozi wa Zambia nchini Mhe. Benson Keith Chali leo jijini Dar es Salaam



Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam



Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge akiongea na Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Zlatan Milišić wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam



Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bi. Christine Musisi akimuelezea jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam




Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na UShirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge akimfafanulia jambo Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bi. Christine Musisi